Ajali ya Ethiopia Airlines: Mwathiriwa akataa fidia kutoka Boeing

John karanja

Mwanamume mmoja aliyepoteza familia yake ya watu watano katika ajali ya ndege ya Boeing ilioanguka nchini Ethiopia anasema kuwa yeye na familia za waathiriwa wengine wa mkasa huo hawatakubali fidia inayotolewa na kampuni hiyo ya ndege.

Boeing inasema kuwa itatoa $100m kwa miaka kadhaa kwa serikali za mtaa na mashirika yasio ya kiserikali kuzisaidia familia na jamii zilizoathirika na ajali hiyo ya ndege aina ya 737 MAX nchini Indonesia na Ethiopia.

Malipo hayo yatakayotolewa kwa miaka kadhaa hayatokani na kesi iliowasilishwa mahakamani baada ya ajali hiyo ambayo ilisababisha vifo vya takriban watu 346.

''Fedha hizo zinalenga kusaidia elimu na maisha ya familia na mipango ya jamii'', ilisema Boeing.

Lakini John Quindos Karanja aliyepoteza vizazi vitatu vya familia yake ambayo iliabiri ndege hiyo ya Ethiopia Airlines ikielekea nchini Kenya alipinga wazo hilo.

Anasema kwamba familia zote zilizopo Kenya na Ethiopia zina kundi moja la WhatsApp ambalo waliliidhinisha siku chache baada ya ajali hiyo.

Karanja anasema kwamba familia hizo hazijapata mawasiliano yoyote rasmi kutoka kwa Boeing na ziligundua habari hizo kutoka kwa vyombo vya habari.

Anasema kwamba familia zote zimechukua msimamo wa kutoshawishiwa na pendekezo lolote ambalo halijatolewa na mahakama ya haki.

Makaburi ya watu wa familia ya Karanja

Karanja anasema kwamba familia hizo zina habari kwamba kampuni hiyo imekodisha kundi la mawakili ambao wametumwa nchini Kenya na Ethiopia kujaribu kuwarai kusuluhisha tofauti zilizopo nje ya mahakama.

Amesema hawatakubali hilo na ameongeza kwamba Boeing haina hisia na ni kama inatafuta njia ya mkato kusuluhisha tatizo hilo.

Mkewe Karanja , Ann Wangui Karanja, mwanawe wa kike Carol Karanja na watoto watatu wa Carol Karanja - kwa majina Ryan Njoroge, Kellie Pauls na mtoto wa miezi tisa Rubi Pauls walikuwa wameabiri ndege hiyo.

Walikuwa wakisafiri kuelekea Kenya kutoka nchini Canada ambako Carol Karanja na watoto wake walikua wakiishi.

Anne Wangui Karanja alikuwa anarudi nyumbani baada ya kuzuru nchini Canada ambapo alikua amewatembelea wajukuu wake na mwanawe ambaye alikuwa akifanya kazi kama mhasibu katika kampuni moja ya nishati.

Ajali hiyo ya mwezi Machi ilikuwa ya pili kuhusisha ndege ya Boeing aina ya 737 Max katika kipindi cha muda wa miezi mitano.

Ndege kama hiyo iliokuwa ikimilikiwa na kampuni ya ndege ya Indonesia carrier Lion Air, ilianguka katika bahari ya Jakarta mnamo mwezi Oktoba 2018.

Wachunguzi wa ajali za ndege wameangazia zaidi mfumo wa kudhibiti ndege hiyo na kampuni ya Boeing imekuwa akishirikiana na wathibiti kuweka mfumo mpya.

Ndege ya kampuni ya Ethiopia Airlines

Chanzo cha picha, JONATHAN DRUION

Ndege ya Boeing aina ya 737 Max imezuiwa tangu mwezi Machi huku kukiwa hakuna tarehe ya ni lini itaruhusiwa kupaa tena.

Dennis Muilenberg , mwenyekiti na afisa mtendaji wa Boeing alisema katika taarifa yake siku ya Jumatano kwamba: Tunaomba radhi kwa maisha yaliopotea katika ajali zote mbili na kwamba maisha yaliopotea yataendelea kuwa mzigo katika roho zetu na mafikra yetu kwa miaka kadhaa. Jamii na marafiki wa waathiriwa wana huruma zetu na tunatumai kwamba tulichotoa kitasaidia katika kuleta faraja, alisema.

Nomi Husain , wakili anayetoka katika jimbo la Texas nchini Marekani anayewakilisha baadhi ya waathiriwa wa ndege aina ya ET 302 alisema kuwa malipo hayo ya Boeing hayafikii hata kidogo kile ambacho familia za waathiriwa wamepotoza.

Aliambia mwandishi wa maswala ya uchukuzi wa BBC Tom Burridge kwamba baadhi ya wateja hawana haja na fidia ya kifedha wakati huu na kwamba Boieng huweka mbele faida badala ya usalama ili kuuza ndege yao , matamshi ambayo watengenezaji wa ndege hiyo wameyakana.

Boeing yashtakiwa kwa ajali ya Shirika la Ndege la Ethiopia

Ethiopia

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mabaki ya ndege ya Ethiopia katika eneo la ajali.

Kampuni ya Boeing imefunguliwa mashtaka nchini Marekani na familia ya mmoja ya abiria waliofariki kwenye ajali ya Shirika la Ndege la Ethiopia.

Ndugu wa Jackson Musoni, ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa na raia pekee wa Rwanda aliyekuwemo kwenye ajali hiyo, wanadai kuwa ndege sampuli ya Boeing 737 Max zinamapungufu ya kiusanifu katika mifumo yake ya kujiendesha.

737 Max

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ndege aina ya Boeing 737 Max za shirika la Southwest zikiwa zimeegeshwa uwanja wa ndege jimboni California baada ya kutolewa katazo la kupaa.

Ndege zote 371 zinazomiikiwa na mashirika mbalimbali za aina ya 737 Max zimepigwa marufuku kuruka toka ilipotokea ajali hiyo, ambayo ilikuwa ni ya pili kwa sampuli hiyo ndani ya miezi mitano. Ajali ya kwanza ilitokea mwezi Oktoba 2018 nchini Indonesia na kuua watu wote 181 waliokuwamo ndani.

Boeing yatangaza maboresho

Boeing

kampuni hiyo ya ndege ilitangaza kuufanyia marekebisho mfumo wa udhibiti (MCA) ambao unahusishwa na ajali zote mbili.

Kama sehemu ya kuboresha ndege hizo, Boeing itaweka mfumo wa onyo kulingana na viwango ,ambao awali ulikua si wa lazima.

Ndege zilizopata ajali za makampuni ya Lion Air ya Indonesia na Ethiopian Airlines, hazikuwa na mfumo wowote wa kuashiria ajali, ambao lengo lake ni kuwaonya marubani wakati mtambo wa uongozaji wa safari ya ndege unapotoa taarifa kinyume na matarajio.

Boeing imesema makampuni hayatakuwa yakitozwa pesa za ziada kwa ajili ya kuweka mfumo huo wa usalama wa ndege.

Boeing

Lakini bado haijajulikana ni lini ndege hizo zilizozunuiwa kusafiri kote duniani mwezi huu zitaruhusiwa kupaa.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Boeing kukubali kuwa kulikuwa na mapungufu ya kiufundi kwenye ndege hizo.

Shinikizo kubwa la kimataifa dhidi ya ndege hizo lilianza mara tu baada ya ajali ya Ethiopia kutokea.

Nchi kadhaa, ikiwamo za Jumuiya ya Ulaya, Canada, Uchina na Rwanda zilipiga marufuku ndege hizo kupaa kwenye anga za mataifa hayo.

Mikasa mibaya zaidi ya Ndege Afrika

Majanga
Majanga

Uraia wa waliofariki kwenye ajali ya Ndege Ethiopia

  • Kenya 32
  • Canada 18
  • Ethiopia 9
  • Italia 8
  • Uchina 8
  • Marekani 8
  • Uingere 7
  • Ufaransa 7
  • Misri 6
  • Ujerumani 5
  • India 4
  • Slovakia 4
  • Australia 3
  • Uswizi 3
  • Urusi 3
  • Wakomoro 2
  • Uhispania 2
  • Poland 2
  • Israeli 2
  • Ubelgiji 1
  • Indonesia 1
  • Somalia 1
  • Norway 1
  • Serbia 1
  • Togo 1
  • Msumbiji 1
  • Rwanda 1
  • Sudan 1
  • Uganda 1
  • Yemen 1