Mzozo wa Sudan: Matumaini mapya kwa wanamapinduzi wadogo

Makundi ya waandamanaji Khartoum

Chanzo cha picha, EPA

Maandamano ya raia kudai utawala wa kiraia yamerejea nchini Sudan katika kipindi kisicho chini ya mwezi mmoja baada ya jeshi kuingilia kati na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 100 na wengine wengi kujeruhiwa, kwa mujibu wa waandamanaji.

Katika miji mbalimbali maelfu ya watu waliingia mitaani wakitaka kukoma kwa utawala wa kijeshi.Mhariri wa BBC Africa Fergal Kean anatathimini umuhimu wa maandamano haya.

Katika siku ambazo hatua kali za kudhibiti maandamano ya tarehe 3 mwezi Juni zilichukuliwa, watu walilazimika kurejea kwenye makazi yao kwenye mahali salama.Lakini waliendelea kuwasiliana wenyewe kwa wenyewe, pia kuwasiliana na watu wengine nje ya Sudan.

Kulikuwa na hali ya hofu na mshtuko. Mauaji ya watu zaidi ya 100, sambamba na vitendo vya ubakaji, vimekuwa na athari kubwa.

Lakini nikiwa mwandishi wa habari wa kigeni mjini Khartoum nilikuwa nafahamu kuhusu mtandao mkubwa wa waandamanaji wa kuendelea na mapinduzi yao. Nilishangaa, majuma kadhaa baada ya mauaji, maandamano madogo madogo yalianza kando kando mwa miji.

Watu kama 100 hapa, 20 mpaka 30 pale, walikuwa wamenyanyua vitambaa juu na nilisikia spika zikitangaza maandamano ya amani.

Waandamanaji mjini Khartoum

Chanzo cha picha, EPA

Tangu kuanza kwa maandamano mwishoni mwa mwaka jana, mitandao ya intelijensia ya nchini humo iliweza kupenya mpaka kwenye makundi ya wanaharakati. Haikujalisha ni watu wangapi walikamatwa lakini mara zote kulikuwa na mtu aliyesubiri kuifanya kazi hiyo.

Lakini ni vyema kutazama mbinu za utawala.Baada ya maandamano yaliyosababisha kuangushwa kwa Omar al-Bashir mwezi Aprili, Jeshi lilirejesha kujiamini kwake. Mazungumzo yalisimama makusudi kuzuia utawala wa kiraia wa mpito.

Mgawanyiko kwenye Jeshi

Mbabe wa kivita Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ajulikanaye kwa jina Hemeti, aliibuka kama mtu muhimu akitumia vikosi vya kijeshi kutishia na kuwaua waandamanaji.

wakipata uungwaji mkono wa kifedha na kisiasa kutoka kwa Saudi Arabia na umoja wa falme za kiarabu, baraza tawala la kijeshi, lilihakikisha kuwa majenerali wanashika nafasi za juu za utawala.

Lakini kumekuwa na mgawanyiko miongoni mwa viongozi wa juu wa jeshi na kumekuwa na hali ya kutoridhishwa na utawala wa Hemeti. Lakini maafisa wa chini ambao walionekana kuwa tishio walidhibitiwa vikali.

Luteni Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo

Chanzo cha picha, AFP

Mapinduzi hayajakoma

Bado kuna dalili za kutokuwepo kwa uhakika. Zishuhudiwa mbinu za utawala mwishoni mwa juma lililopita. Risasi, gesi za kutoa machozi na kupigwa kwa watu waliokuwa wakiandamana kwa amani. Kulikuwa na vifo na wengine walijeruhiwa.

Lakini Hemeti haonekani kuwa kiongozi mwenye nguvu katika siku za baada ya tarehe 3 mwezi Juni. Kimataifa, upinzani ulifanikiwa kupeleka ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, pamoja na kuwepo kwa changamoto ya mtandao wa intaneti.

Umoja wa Afrika umeivua Sudan uanachama. Wapatanishi wa Marekani na Afrika wametembelea Khartoum majuma ya hivi karibuni. hatua hiyo ya upatanishi imeshindwa kuleta mabadiliko muhimu.

Jeshi limeshindwa kutimiza matakwa ya raia walio wengi ya kuwa sehemu ya chombo cha juu cha maamuzi.