Mzozo Sudan :Vikosi vya usalama vyalaumiwa kushambulia waandamanaji

Jeshi la nchini Sudani limekemewa kutokana na mashambulizi yake dhidi ya waandamanaji mjini Khartoum, hatua iliyosababisha watu 30 kupoteza maisha.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametaka uchunguzi ufanyike akisema ametamaushwa na ripoti kuwa maafisa walifyatua risasi hospitalini.

Marekani na Uingereza zimesema ni ''tukio la kikatili''.

Sudan imekua chini ya utawala wa kijeshi tangu Rais Omar al-Bashir alipopinduliwa mwezi Aprili.

Viongozi walioongoza vuguvugu la kutaka utawala wa kiraia kuongoza nchi hiyo, wamesema wamesitisha mawasiliano na serikali ya mpito ya kijeshi na kufanya mgomo.

Vikosi vya usalama vilifika maeneo ambayo watu walikua wakiandamana, mapema Jumatatu na sauti za risasi zilisikika kwenye picha za video.

Vikosi vya usalama Sudan

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Katika taarifa yake iliyosomwa kwa njia ya televisheni ya taifa, Jeshi limeeleza masikitiko yake kwa namna hali inavyozidi kuwa mbaya na kusema kuwa operesheni ilikua imewalenga ''wanaotia dosari hali ya usalama na wahalifu''.

Jeshi limesema kuwa limekuwepo kwa ajili ya kulinda raia.

Awali, wanaharakati wamesema vikosi vya usalama waliizunguka hospitali moja mjini Khartoum na kufyatulia risasi hospitali nyingine.

Kamatikuu ya madaktari wa Sudan, walio karibu na waandamanaji wamesema watu 30 akiwemo mtoto wa miaka minane wa,meuawa, na idadi ya waliopoteza maisha inatarajiwa kuongezeka.

Mamia ya watu wamejeruhiwa.

Waandamanaji wakiwasha moto kuvizuia vikosi vya usalama

Chanzo cha picha, AFP

Baadhi ya wakazi wamekilaumu kikosi cha Rapid Support Forces, kilichokuwa kikipambana kumsaidia Bwana Bashur kubaki madarakani na kushiriki kwake kwenye mzozo wa Darfur magharibi mwa Sudan ulioanza mwaka 2003.

Wakati huo wakifahamika kwa jina ''Janjaweed'', wanamgambo hawa walitekeleza mauaji.

Nini kilifuata?

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka mamlaka za Sudan kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya wale waliohusika.

Taarifa yake imelaani matumizi ya nguvu kuwatawanya waandamanaji, na kushtushwa na ripoti kuwa vikosi vya usalama kufyatua risasi kwenye hospitali.

Shirika la habari la Sudan limesema mwendesha mashtaka ameunda kamatai kufanyia uchunguzi matukio hayo.

Chanzo ni nini?

Waandamanaji wamekua wakikita kambi nje ya jengo la makao makuu ya jeshi tangu tarehe 6 mwezi Aprili, siku tano kabla ya kuangushwa kwa utawala wa Bashir.

Mwezi uliopita, waandaaji na majenerali watawala walikubaliana kuhusu muundo wa serikali mpya na muda wa mpito wa miaka mitatu kuelekea kwenye utawala wa kiraia.

Hawajaweza kuamua kuhusu ni upande upi hasa kati ya raia au jeshi kuchukua nafasi nyingi zaidi.

Wanawake wakiandamana

Chanzo cha picha, AFP

  • 19 Disemba 2018 - Maandamano yaliibuka baada ya kupanda kwa gharama za mafuta na mkate kutangazwa.
  • 22 Februari 2019 - Rais Bashir aivunja serikali.
  • 24 Februari - Maandamano yaendelea wakati vikosi vya usalama wakipambana na waandamanaji.
  • 6 Aprili - Wanaharakati wanaanza kuweka kambi makao makuu ya jeshi, wakiapa kutoondoka mpaka Rais Bashir atakapoondoka madarakani.
  • 11 Aprili - Jeshi latangaza kuwa bwana Bashir ameondolewa madarakani lakini watu wataka utawala wa kiraia.
  • 20 Aprili -Mazungumzo kati ya vikosi vya kijeshi na wawakilishi wa raia yaanza.
  • 13 Mei- Ufyatuaji risasi nje ya makao makuu ya jeshi yasababisha vifo vya watu sita.
  • 14 Mei - Jeshi na raia walitangaza makubaliano ya kuunda serikali ya mpito ya miaka mitatu.
  • 16 Mei-Mazungumzo yaahirishwa wakati Jeshi lilipotaka waandamanaji waondoe vizuizi
  • 3 Juni - Wanaharakati watangaza kusitishwa kwa mazungumzo na jeshi , wakilishutumu kusambaratisha makusanyiko yao.