Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani 'yashambulia mifumo ya Kompyuta ya silaha za Iran'
Marekani imeanzisha mashambulizi ya mtandao kwenye mifumo ya silaha za Iran siku ya Alhamisi wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipoachana na mashambulizi ya anga, Ripoti nchini Marekani zimeeleza.
Mashambulizi hayo ya mtandaoni yameharibu mifumo ya kompyuta inayodhibiti roketi na mitambo ya kurushia makombora, limeeleza gazeti la Washington Post.
Tukio hilo ni kulipiza kisasi tukio la kushambuliwa kwa ndege yake isiyo na rubani pia mashambulizi dhidi ya meli za mafuta ambazo Iran imedaiwa na Marekani kuziteketeza,New York Times imeeleza.
Marekani pia imeweka vikwazo ambavyo rais Trump ameeleza kuwa ''vikubwa''.
Amesema vikwazo vilikua vinahitajika kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyukilia na vikwazo vya kiuchumi vitaendelea mpaka pale Tehran itakapobadili uelekeo.
Mvutano kati ya Marekani na Iran ulijitokeza tangu Marekani ilipojiondoa kwenye mkataba wa nyukilia wa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani na kuiwekea vikwazo vilivyotikisa uchumi wa Iran.
Juma lililopita, Iran ilisema itaongeza viwango vilivyowekwa kwenye mkataba ule kuhusu mradi wa nyukilia.
Trump alisema hataki vita na Iran, lakini alionya kuwa Iran itakabiliwa na ''uharibifu'' ikiwa mzozo utatokea.
Mashambulizi ya mtandaoni yameleta athari gani?
Mashambulizi yalipangwa kwa majuma kadhaa, vyanzo vimeviambia vyombo vya habari nchini Marekani ikaelezwa kuwa ni njia ya kulipa kisasi mashambulizi ya mabomu dhidi ya meli za mafuta kwenye Ghuba ya Oman.
Mashambulizi haya yamelenga mifumo ya silaha zinazotumiwa na majeshi ya nchi hiyo, yaliyoshambulia ndege isiyo na rubani ya rubani siku ya Alhamisi juma lililopita.
Kwa pamoja Washington Post na AP zimeeleza kuwa mashambulizi ya mtandao yameharibu mifumo.New York Times limesema ililenga kuzima mifumo hiyo kwa muda.
Siku ya Jumamosi duru za kiusalama za Marekani zilionya kuwa Iran ina mpango wa kufanya mashambulizi ya mtandaoni pia dhidi ya Marekani.
Chrostopher Krebs, Mkurugenzi shirika la usalama na miundombinu ya kiusalama nchini Marekani amesema ''hila za mashambulizi'' zinaelekezwa na utawala wa Iran na mawakala wake dhidi ya viwanda vya Marekani na mashirika ya kiserikali.
Iran pia imekuwa ikijaribu kudukua mifumo ya meli za kijeshi za Marekani, Washington Post limeripoti.
Trump amesemaje?
Hajasema chochote kuhusu ripoti za mashambulizi ya mitandaoni.Siku ya Ijumaa alisema ameacha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran kwa sababu aliambiwa kuwa raia 150 watapoteza maisha.
Siku ya Jumamosi alisema alikua na mazungumzo ya wazi na raia wa Iran.
''kama Iran inataka kuwa taifa linalostawi...ni sawa kwangu, ''Trump alisema. ''Lakini hawatafikia hilo kama wanafikiri kuwa katika kipindi cha miaka mitano au sita watakuwa na silaha za nyukilia.
''Tuifanye Iran kuwa nzuri tena,'' aliongeza, akirejea kampeni yake ya mwaka 2016 wakati wa uchaguzi wa urais.
Vikwazo hivyo ni vipi?
Ununuzi wa noti za Marekani unaofanywa na Iran.
Biashara ya dhahabu na vyuma vingine
Graphite, aluminium, chuma, mkaa na programu zinazotumiwa katika sekta ya viwanda
Ubadilishanaji wa fedha unaohusishwa na sarafu ya Iran
Vitendo vinavyohusishwa na ulipaji madeni ya Iran
Sekta ya magari ya Iran
Vikwazo hivyo viliathiri uchumi wa nchi hiyo- kwa sababu ililenga sekta yake kuu wa mafuta, na benki.
Vikwazo vilizuia makampuni ya Marekani kufanya biashara na Iran, lakini pia makampuni ya kigeni au nchi kufanya biashara na Iran.
Hali hii ilifanya kuwe na upungufu wa bidhaa zinazoingia nchini Iran kutoka nje.