AFCON 2019: Misri na Zimbabwe kukata utepe wa mashindano makubwa zaidi ya Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Wenyeji Misri wanaingia dimbani usiku wa leo dhidi ya Zimbabwe katika mechi ambayo itafungua ukurasa mpya wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).
Ni mashindano ya kwanza kufanyika katika kipindi hiki cha katikati ya mwaka, sawia na majira ya joto Barani Ulaya, ambapo ligi zote zipo mapumzikoni.
Pia ndio mashindano ya kwanza kutanuka na kushirikisha timu 24.
Misri ilikabidhiwa jukumu la kuandaa mashindano hayo mwezi Januari mwaka huu baada ya Cameroon kupokwa nafasi hiyo kwa sababu za kiusalama na kusuasua kwa maandalizi.
Misri ama maarufu kama Mafarao ndio mabingwa wa kihistoria wa Afcon kwa kulinyakua kombe hilo mara saba.
Lakini mara ya mwisho wamelinyakua mwaka 2010, na wamepoteza fainali iliyopita mwaka 2017 kwa kufungwa na Cameroon.
Hivyo, mechi ya leo usiku ni ya muhimu sana kwao, ni mwanzo wa safari wanayotumaini itaishiakwa furaha ya kutetea ufalme wao.
Mohamed Salah ndio mchezaji bora, kinara na maarufu zaidi katika kikosi cha Misri.
Kuna wengine watatu, ambao pia wanacheza mpira wa kulipwa England, kiungo wa Arsenal Mohamed Elneny, beki wa West Brom Ahmed Hegazi na Ahemd Elmohamady ambaye ni beki wa Aston Villa.
''Salah sasa ni miongoni mwa wachezaji watatu bora ulimwenguni'' amesema Elmohamady , ''Hili ni jambo kubwa sana na itatusaidia kupata ushindi katika mashindano haya ya kombe la Afrka.''
Mechi ya leo itachezwa katika uwanja wa Kimataifawa Cairo ambao umekuwa ukitumika kwa mara chache sana kwa kipindi cha miaka nane iliyopita kutokana na sababu za kiusalama.
Hii itakua ni mara ya tano kwa Misri kuwa wenyeji wa mashindano haya. Wamenyakua kombe hilo mara tatu katika miaka waliyoandaa 1959,1986 na 2006 huku wakishika nafasi ya tatu mwaka 1974, mabingwa wakiwa DRC.
Zimbabwe wanacheza katika michuano hii kwa mara ya nne lakini hawajawahi kuvuka ngazi ya makundi.

Chanzo cha picha, AFP
Mashinado ya mwaka 2017 walimaliza wakishika mkia baada ya kushindwa kushinda hata mchezo mmoja.
Kikosi chao pamoja na wachezaji wengine kina nyota kama beki wa Nottingham Tendayi Darikwa na Alec Mudimu ambaye anachezea ligi kuu ya Wales.
Michuano hii hapo awali ilikuwa ikifanyika mwezi Januari na Februari na kusababisha migongano na klabu kadhaa barani Ulaya ambapo walitakiwa kuwaachia wachezaji wa Afrika waje yumbani kushiriki michuano hii.
Kutokana na hilo mwaka 2017 shirikilisho la Mpira Barani Afrika waliamua mashindano hayo kufanyika mwezi Juni na Julai kuanzia mwaka huu.















