Mchezaji wa Real Madrid Sergei Ramos amuoa Pilar Rubio

Umati wa watu ulikusanyika katika kanisa kuu la Seville nchini Uhispania Jumamosi 15, Juni 2019, kushuhudia sherehe ya harusi ya mchezaji soka wa Real Madrid -Sergio Ramos aliyekuwa akifunga pingu za maisha na mchumba wake wa muda mrefu Pilar Rubio, ambaye ni mtangaza Televisheni.

Sergio mwenye umri wa miaka 33-alikuwa nadhifu huku akiwa amevalia suti ya vipande vitatu nyeusi(three piece) iliyokuwa imeshonwa kwa mtindo wa aina yake pamoja na tai ya rangi ya kijivu iliyotulia huku bibi harusi mwenye umri wa miaka 41- akionekana kwa gauni lenye mvuto lililoiacha shingo na na mabega yake wazi kiasi cha haja.

Gauni lake refu lililogusa sakafu lililikuwa limerembeshwa kwa shanga na juu alikamilisha urembo wake kwa shela iliyowekwa nakshi.

Aliamua kusuka nywele zake na akaweka kibanio kikubwa cheusi, mtindo ambao ni wa kipekee ambao haujashuhudiwa katika harusi za watu maarufu.

Mrembo Rubio aliamua kuvalia heleni ndeefu zilizobuniwa na kampuni ya vipuli na mavazi ya bracelet na kidole chake cha kati kikapambwa na pete ya almasi.

Baada ya ibada ya harusi kanisani, wageni waalikwa 500 walikaribishwa kwa hafla kubwa kwenye makazi ya bwanaharusi yanayoitwa "Happiness of SR4" yaliyopo eneo la Seville.

Na kwa mujibu wa gazeti la Uingereza Daily Mail, wageni waliruhusiwa kuingia katika baada ya kuacha simu zao na vifaa vingine kama kamera au vinasa sauti.

Harusi iligubikwa na soka kwani nyota wengi wa soka walihudhuria kama vile mchezaji wa zamani wa Real Madrid David Beckham na mkewe Victoria Beckham, nyota wa sasa na wa zamani wa La Liga Jordi Alba, Luka Modric, Keylor Navas, Roberto Carlos na Alvaro Morata, pamoja na matador El Cordobes na wengine wengi.

Hata hivyo Cristiano Ronaldo hakuhudhuria kwani hakualikwa kwasababu ya kile kilichoripotiwa kuwa wawili hao walikosana wakati Ronaldo alipoondoka Real Madrid msimu uliopita kujiunga na Juventus kwa mkataba wa pauni milioni 100 .

Pia , Gerard Pique na Shakira hawakuhudhuria harusi ya Sergio kwa sababu ambazo hazikujulikana, licha ya kwamba alialikwa.

Bwana harusi aliamua kumzawadia bibiharusi onyesho la muziki wa bendi maarufu ya Australia AC/DC, inayopiga muziki wa ambayo alifahamu fika mkewe anaipenda sana.

Wawili hao wamekuwa wakiishi pamoja tangu mwaka 2012 na wanawatoto watatu wanaoitwa Sergio, Marco na Alejandro.

Katika mahojiano aliyoyafanya wakati wa harusi yake, Ramos alifichua kuwa siku yao ya harusi ilikuwa ni ya kipekee si kwao tu bali pia kwa watoto wao.

Nahodha huyo wa Real Madrid alinukuliwa akisema , "Ni wakati wa kipekee sana kwetu baada ya kuwa pamoja kwa muda mrefu na kuunda familia nzuri sana yenye watoto wadogo watatu ambao wanayajaza maisha yetu furaha na malengo''. Aliongeza," Tulihisi kuwa ulikuwa ni muda unaofaa na tulitaka watoto wetu waifurahie kwasababu walikuwa ni wadogo sio kitu ambacho wangekielewa sana ."

Baadhi ya wageni waliohudhuria harusi: