Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akanusha uwepo wa tishio jijini humo

Muda wa kusoma: Dakika 2

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekanusha taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwamba kuna tishio la mashambulizi jijini Dar es Salaam.

Jana usiku, Ubalozi wa Marekani ulitahadharisha umma juu ya fununu za uwepo wa mipango ya kushambuliwa eneo la kifahari la Masaki, jijini Dar es Salaam.

Tangazo hilo lilisambaa kila kona ya mitandao ya kijamii nchini humo kwa haraka.

Japo ubalozi huo umesema kuwa hauna uthibitisho wa moja kwa moja juu ta sambulio hilo, umewataka wananchi kuchukua tahadhari.

Kwa mujibu wa Makonda, tahadhari hiyo imezua taharuki kubwa kwenye jamii.

"...ukweli ni kwamba jiji letu lipo shwari na kila mtaa, kila kata na kila wilaya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kama kawaida. Niwatoe hofu walio kwenye mahoteli na wageni kwenye jiji letu ya kwamba hakuna tishio." amesema Makonda.

Kiongozi huyo pia ameonekana kuelekeza lawama kwa ubalozi wa Marekani, na kuwataka wakazingatia Katiba na Sheria za Tanzania kwa kuwa kuna vyombo maalumu vya kutangaza kama kuna hali ya hatari.

"Hakuna taarifa yoyote iliyotoka katika ofisi yangu wala mamlaka ya kitaifa kwa maana ya mheshimiwa Rais (John Magufuli). Ni hakika na bayana ya kwamba jiji letu lipo shwari,"amesisitiza Makonda.

Kauli ya Makonda inakinzana na ya Mkuu wa Polisi wa nchi hiyo, Inspekta Jenerali Simon Sirro ambaye amelieleza gazeti la Mwananchi kuwa walipata fununu za shambulio kabla ya ubalozi wa Marekani.

Sirro amenukuliwa akisema: "hiyo ni taarifa kama taarifa nyingine, inaweza kuwa ya kweli au uongo, lakini sisi kama vyombo vya ulinzi huwa hatupuuzi jambo''.

Raia wanasema nini?

Tangazo la Makonda limepokewa kwa hisia tofauti, japo kuna ambao wamemuunga mkono wengi wanaonekana kumpinga kwa kukanusha moja kwa moja tahadhari hiyo ya Marekani.

Watuamiaji wengi wa mitandao ya kijamii wanaonekana kushawishika na uzoefu wa Marekani katika masuala ya usala na kusema mamlaka za Tanzania hazitakiwi kupuuzia tahadhari hiyo.

Makonda amechapisha video ya ujumbe wake kwenye mtandao wake wa Instagram, na moja ya watu wanaomfuatilia kwa jina la albino_decutest aliandika ujumbe huu: "Wao wamewatangazia Wamarekani wenzao, na tayari Wamarekani wote waliopo nchini wameshachukua tahadhari. Ili sisi wabongo (Watanzania) tangazo lako wewe na (IGP) Sirro ndio yanatuhusu..."

Kuna ambao wamemshauri Makonda naye kuchukua tahadhari kufuatia onyo hilo la Wamarekani.

Wapo wanaoamini kuwa tahadhari ya Marekani si kitu bali propaganda zinazolenga kuchafua taswira ya Tanzania.

Mtumiaji wa Instagram kwa jina la pastor_mwamaso ameandika chini ya video ya Makonda kuwa: "huu ni uhujumu wa kisayansi wametengeneza wasiwasi na kutuwa na imani kwa wageni/watalii. Hapa unadhani wataamini lipi waache lipi. Hii ni dharau kwa nchi. Waziri wa mambo ya ndani achukue hatua."

Mtumiaji mwengine wa Instagram, kwa jina la gelgojoes hata hivyo anasema suala la propaganda lisizue taarifa hiyo kufanyiwa kazi: "...tunaongelea usalama wa raia. Tunajua inaweza kuwa propaganda ya wazungu but (lakini) hawa Wamarekani walishawahi kutoa security alert (tahadhari ya kiusalama) Kenya na baada ya hapo mfululizo wa mashambulio ya al Shabab. Sasa swali ni kwamba attacks (mashambulizi) ikitokea, upo tayari kurudi hapa mtandaoni. Mimi nashauri serikali ishirikiane na Wamarekani kutuweka salama."