Mahakama ya Uswisi imesitisha hukumu ya IAAF dhidi ya Caster Semenya

Caster Semenya

Chanzo cha picha, Getty Images

Caster Semenya hatahitajika kutumia dawa za kupunguza kiasi cha homoni kushiriki mashindano baada ya mahakama ya Uswisi kusitisha kwa muda hukumu iliyotolewa na shirika la riadha duniani (IAAF)

Bingwa wa Olimpiki wa mbio za mita 800, 28, mwezi uliopita alishindwa kesi katika mahakama ya usuluhishi wa migogoro michezoni(Cas) alipokua akipinga hatua ya kupunguza kiasi cha homoni kwa wakimbiaji wakike

Hukumu hiyo ingewaathiri wanawake wanaoshiriki mbio za mita 400 mpaka maili.

''Nina matumaini kuwa baada ya rufaa kwa mara nyingine nitaweza kukumbia nikuwa huru,'' Alisema.

''Ninashukuru majaji wa Uswisi kwa uamuzi wao.''

Baada ya uamuzi wa mahakama ya usuluhishi wa migogoro michezoni, Caster Semenya alikata rufaa kwenye mahakama ya Uswisi, akieleza nia yake ya kutetea ''haki za binaadamu''.

Caster Semenya

Chanzo cha picha, Getty Images

Wakili wake Dokta Dorothee Schramm amesema: ''Mahakama imemuwekea ulinzi wa muda Caster Semenya.

''Hii ni kesi muhimu kwa kuwa italeta matokeo mazuri katika kuzingatia haki za binaadamu linapokuja suala la wakimbiaji wanawake.''

Katika hukumu yake awali Cas ilibainisha kuwa sheria mpya zilizotolewa na IAAF kwa wakimbiaji wa kike wenye homoni kwa kiwango kisicho cha kawaida ni za kibaguzi, lakini ikahitimisha kuwa hatua hiyo ilikua ''lazima, na yenye muhimu, wa kueleweka na wa uwiano kwa ajili ya kulinda maadili ya wanariadha wanawake ".

IAAF imesema bado haijapokea nakala yeyote kuhusu uamuzi mpya wa mahakama ya Uswisi.

  • 31 Julai 2009: Semenya akiwa na miaka alishinda mbio za mita 800 na kujishindia medali ya dhahabu kwenye African Junior Championships.
  • Agosti 2009: Semenya alifanyiwa kipimo cha jinsia yake kabla ya michuano ya dunia ya Berlin, hakujua sababu ya vipimo hivyo lakini aliambiwa na rais wa shirikisho la riadha Afrika Kusini Leonard Chuene kuwa ni kipimo cha kawaida.
  • 19 Agosti 2009: Semenya anashinda mbio za mita 800 na kushinda medali ya dhahabu akivunja rekodi aliyoiweka mwezi Julai.Baada ya ushindi taarifa kuhusu kipimo cha jinsia zikavuja kwenye vyombo vya habari.
  • Novemba 2009: Kuna ripoti kuwa kipimo cha Semenya kimeonyesha kuwepo kwa homoni za kike na za kiume, lakini majibu hayakuwekwa hadharani.
  • 6 Julai 2010: Semenya aliruhusiwa kushiriki michuano na IAAF tena.
  • 22 Agosti 2010: Semenya anashinda michuano ya IAAF Berlin mita 800.
  • 11 Agosti 2012: Semenya anashinda mbio za mita 800 na kupata medali ya fedha michuano ya Olimpiki ya London.Lakini baadae alikabidhiwa medali ya dhahabu baada ya mshindi wa awali kutoka Urusi Mariya Savinov kufungiwa maisha kwa kosa la kukiuka sheria ya udanganyifu michezoni.
  • Julai 2014: Mkimbiaji wa mbio fupi wa India Dutee Chand, anazuiwa kushiriki baada ya kipimo cha homoni kubaini kuwa ana vichocheo vinavyopatikana kwa wanaume.
  • 23 Machi 2015: Chand anaanza mapambano ya kisheria dhidi ya vipimo vya jinsia vya IAAF.
  • 27 Julai 2015: Chand anaruhusiwa kushiriki michuano:Mahakama ya Cas inazuia kwa miaka miwili sheria ya IAAF kuwataka wakimbiaji wa kike kunywa dawa za kupunguza kiwango cha homoni.
  • 20 Agosti 2016: Semenya anashinda mbio za mita 800 na kupata medali ya dhahabu katika mbio za Olimpiki za mjini Rio, lakini uamuzi wa kumruhusu kushiriki mbio hizo ulihojiwa na wakimbiaji wengine.
  • 19 Juni 2018: Semenya anasema atapambana kisheria dhidi ya sheria hizo 'sizizo za haki'.
  • 18 Februari 2019: Kesi yaanza kusikilizwa kwenye mahakama ya utatuzi wa migogoro michezoni Cas.
  • 1 Mei 2019: Semenya anashindwa kesi.
  • 29 Mei 2019: Semenya kukata rufaa mahakama kuu ya nchini Uswisi.
  • 3 Juni 2019:Mahakama ya Uswisi yasitisha sheria ya IAAF kwa muda, wameeleza mawakili wake.