Ufaransa inauliza: Unaweza kukitegua kitendawili hiki kwenye jiwe?

Chanzo cha picha, AFP
Kijiji kimoja huko magharibi mwa Ufaransa kimetangaza zawadi ya €2,000 kwa yeyote atakayeweza kutegua ujumbe uliokwangurwa kwenye jiwe katika ufukwe wa bahari.
Mpaka sasa hakuna aliyefanikiwa kutoa maana ya ujumbe huo wa mistari 20 ya maandishi, uliogunduliwa miaka 20 iliyopita.
Jiwe hilo lenye urefu wa mita moja lipo kwenye pango dogo linaloweza kufikiwa tu wakati maji yanakupwa karibu na kijiji cha Brittany - Plougastel.
Katika herufi za kawaida za Kifaransa baadhi huwa kinyume au juu chini. Na pia kuna baadhi zenye mtindo wa herufi - Ø za Scandinavia.

Chanzo cha picha, AFP
Miaka miwili inaonekana - 1786 na 1787 - tarehe inayoonyesha umri wa maandishi hayo kuwa kabla ya mapinduzi Ufaransa. Kuna picha ya mashua iliyo na mchoro wa 'sacred heart' - mchoro wa kopa ulio na msalaba.
Lakini wengi wameshindwa kuyafasiri maandishi hayo na hata wasomi kutoka eneo hilo. Baadhi wanadhani aliyeandika hakusoma kikamilifu.
Na herufi zinahusiana na maneno ambayo mwandishi aliyasikia tu.
Katika sehemu moja, herufi zinasoma: "ROC AR B … DRE AR GRIO SE EVELOH AR VIRIONES BAOAVEL".
Sehemu nyingine: "OBBIIE: BRISBVILAR ... FROIK … AL".
Fikra moja ni kwamba maandishi hayo yanahusiana na ujenzi wa vituo vya ulinzi wa jeshi la majini karibu na enoe hilo. Ngome na ghala la silaha ambayo masalio yake yanaonekana - zilijengwa katika eneo hilo katika miaka ya 80 kulilinda eneo la Bay of Brest. Hadi 1783 Ufaransa ilikuwa katika vita na Uingereza.

"Tumewauliza wanahistoria na wana akiolojia kutoka eneo hili, lakini hakuna aliyeweza kufumbua historia ya jiwe hili," anasema Dominique Cap, Meya wa Plougastel.
"Kwa hivyo tumefikiria pengine kwengineko duniani huenda kukawa na watu walio na utaalamu tunao uhitaji. Badala ya kulipuuzia, tukasema hebu tuanzishe shindano."
Ombi hilo kwa umma "The Champollion Mystery at Plougastel-Daoulas" - ni kutoa heshima kwa Jean-François Champollion, mwanafasihi aliyefumbua ujumbe kwenye jiwe la Rosetta nchini Misri katika karne ya 19.
Wakati shindano litakapofungwa Novemba mwishoni mwa mwaka, jopo litachagua maelezo yalio bora ya ujumbe huo wa siri.
Huenda pia ukavutiwa na:













