Jordan Kinyera: Asomea uwakili ili kukomboa ardhi ya familia yake Uganda

Raia mmoja wa Uganda ambaye alikuwa na umri wa miaka sita pekee wakati babake alipopoteza ardhi yao katika kesi moja hatimaye ameikomboa ardhi hiyo miaka 23 baadaye baada ya kuwa wakili.

Jordan Kinyera alipitia miaka 18 ya elimu na mafunzo ya kisheria kabla ya kuichukua kesi hiyo kama wakili.

Siku ya Jumatatu , mahakama ya juu ilitoa uamuzi wa mwisho ambao uliipendelea familia yake.

Bwana Kinyera aliiambia BBC kwamba kupotea kwa ardhi hiyo ya familia kulibadilisha maisha yake wakati alipokuwa na umri wa miaka sita.

''Nilifanya uamuzi wa kuwa wakili baadaye maishani lakini uamuzi huo ulishinikizwa na kesi ya ardhi yetu nilipokuwa katika harakati za kuwa mtu mzima , hali na maudhi ambayo familia yangu ilipitia wakati wa kesi hiyo na jinsi ilivyowaathiri'', Bwana Kinyera alisema.

Babake alishtakiwa na majirani zake kufuatia mgogoro wa ardhi hiyo mwaka 1996 huku kesi hiyo ikicheleweshwa mahakamani kwa zaidi ya muongo mmoja.

''Babangu alikuwa amestaafu, hivyobasi hakuwa na raslimali. Alikuwa hapati fedha zozote. Alikuwa amekata tamaa na hakuna kitu kibaya kwa binadamu kukata tamaa na kushindwa kufanya chochote'. Hicho ndicho kilichonipatia shinikizo kubwa''

Bwana Kinyera aliambia BBC kwamba alimfurahia babake ambaye anasema kuwa hajawahi kupanda hata mbegu moja ama hata kuanzisha ujenzi wowote katika kipindi cha miaka 23 iliopita.

''Babangu ana umri wa miaka 82 sasa na hawezi kuitumia ardhi hiyo . Na sasa ni sisi watoto kuendelea kutoka pale ambapo babangu alituachia''.

Migogoro ya ardhi nchini Uganda imesheheni. Kulingana na shirika la haki za kisheria Namati, huathiri kati ya asilimia 33-50 ya wamiliki wa aradhi.

''Raia wengi wa Uganda ambao hurudi katika maeneo yao ya mashambani baada ya kuhudumu miaka kadhaa katika kambi hujipata katika mizozo ya ardhi'' , bwana Kinyera aliambia BBC.

Anawakilisha baadhi ya wateja katika kesi hizo.

Swala hilo ni kubwa mno hali ya kwamba tawi zima la mahakama ya juu huangazia mizozo ya ardhi pekee.