Utafiti wa Lancet: Si lazima usubiri kwa muda mrefu baada ya kupoteza ujauzito

Chanzo cha picha, Dorothy Stephen
Tatizo la mimba kuharibika na kutoka kabla ya umri wake unaotakiwa kukamilika, limekuwa likiwasumbua wanawake wengi.
Mara nyingi wanawake wanaojipata katika hali hiyo hushauriwa kusubiri kwa angalau mwaka mmoja kabla ya kupata ujauzito tena.
Hata hivyo hakuna ushahidi wa kimatibabu unathibitisha ushauri huo.
Utafiti wa kimatibabu uliyofanywa kuhusiana na suala hilo na kuchapishwa katika jarida la Lancet unaashiria kuwa hakuna haja ya mwanamke kusubiri kwa muda mrefu baada ya kupoteza ujauzito.
BBC imezungumza na Dorothy Stephen ambaye aliwahi kupoteza mimba ili kubaini ilimchukua muda gani kupata ujauzito mwengine.

Chanzo cha picha, Dorothy Stephen
Bi Dorothy anasema alipatwa na tukio la kupoteza ujauzito wa miezi mitano mwaka 2013.
''Nilijiona na dalili ambazo si za kawaida nikaenda kumuona daktari akanipima na kuniambia kuwa sio tatizo''
Alirudi nyumbani na kuendelea na shughuli zake za kila siku kwa sababu daktari alimhakikishia kuwa kila kitu kiko shwari.
''Nilikuwa na safari ya kwenda mikoani na nilitumia ndege lakini nilipofika kule nilikuwa nikienda nilijisikia maumivu makali sana'', alisema Dorothy

Chanzo cha picha, Getty Images
Alilazimika kuenda kliniki mara kwa ya pili ambapo alifahamishwa kuwa yuko katika hali mbaya na kwamba anahitaji matibabu ya dharura.
''Nilizalishwa lakini mtoto alifarika saa moja baadae kwasababu viungo vyake ya kusaidia kupumua vilikua havijakua tayari kufanya kazi''
Dorothy anasema tukio hilo lilimfanya kukumbwa na hisia za majonzi na uwoga kwa muda mrefu.
Alihofia huenda akapoteza tena ujauzito hali ambayo ilimfanya kukaa kwa karibu mwaka mmoja.
Daktari alimpatia ushauri wowote?
''Nilishauriwa na daktari nimpumzike kwa muda na kwamba nikipata ujauzito ni hakikishe nafika kliniki kwa uchunguzi wa karibu''
Licha ya ushauri huo alikaa karibu mwaka kabla mmoja kabla apate ujauzito tena.

Chanzo cha picha, Huw Evans picture agency
Bi Dirothy anasema kuwa alipata ujauzito tena mwaka 2015 lakini anasema alikuwa na wasiwasi kuanzia mwanzo wa ujauzito hadi alipojifungua.
''Miezi mitatu ya kwanza nilikuwa hatari kwangu kwasababu nilikua napata dalili hatarishi''
Daktari wake alimhudumia kwa karibu na hatimaye alijifungua salama na anasema mtoto wake ambaye sasa ana miaka mitatu, amemfanya asahau majonzi aliyopata wakati alipopoteza mimba yake ya kwanza.
Nini husababisha mimba kuharibika?
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ya uzazi kuna sababu nyingi zinazosababisha mimba kuharibika kisha kutoka.
- Umri mkubwa-kwa kawaida, mwanamke anapofikisha umri wa miaka 35 au zaidi, misuli ya mji wake wa uzazi hulegea na kupungua nguvu za kuweza kuhimili na kutunza kiumbe kinachokuwa ndani ya mji wa uzazi. Kulegea kwa misuli hii husababisha mimba kutoka kwa urahisi.
- Magonjwa-wanawake wanaosumbuliwa na magonjwa kama kisukari, unene kupindukia,malaria kali, magonjwa ya zinaa na mengineyo huwa katika hatari kubwa ya mimba zao kutoka.
- Hitilafu za kizazi-baadhi ya wanawake huwa na mfuko wa mimba ambao muundo wake siyo wa kawaida. Wanawake wenye tatizo hili, huwa na hatari kubwa ya mimba zao kuharibika kabla ya kutimiza umri wa miezi tisa.
- Maambukizi ya bakteria au fangazi-maambukizi hayo husababisha misuli ya kizazi kushambuliwa na kisha kupoteza uwezo wake wa kuhifadhi ujauzito, jambo ambalo husababisha mimba kutoka.
- Sababu nyingine ni pamoja matumizi ya pombe kali, uvutaji sigara, matumizi ya dawa za kulevya, kemikali, matatizo ya kurithi na kadhalika.













