Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Usawa wa kijinsia: Bunge la Kenya limeshindwa kupitisha muswada wa usawa wa kijinsia
Bunge la Kenya limeshindwa kupitisha muswada wa usawa wa kijinsia ambao ulikua unapania kuongeza idadi ya wanawake katika nyadhifa za uongozi,mjadala haukuendelea kutokana na bunge kukosa idadi toshelezi ya wabunge.
Lengo la mswada huo ni kuhakikisha kuwa taasisi zote nchini Kenya zinaafikia hitaji kikatiba ya kuwa na theluthi mbili ya jinsia.
Hii ni mara ya nne muswada huo umeshindwa kupitishwa bungeni kutokana na idadi ndogo ya wabunge.
Lengo la mswada huo ni kuhakikisha kuwa taasisi zote nchini Kenya zinafikia hitaji la kikatiba la kuwa na theluthi mbili ya jinsia na kunapania kuongeza idadi ya wanawake katika nyadhifa za uongozi.
Shirikisho la wabunge wanawake nchini (KEWOPA) ambalo liliwasilisha mswada huo sasa lilitegemea uungwaji mkono wa kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale kuwashawishi wanaume wenzake kuidhinisha mswada huo.
Ili mswada huo uidhinishwe kuwa sheria unahitaji kuungwa mkono na angalau wabunge 233.
Mwezi Februari mwaka 2017, mswada kama huu uliyowasilishwa na seneta Judith Sijeny ulishindwa kupitishwa baada ya kushindwa kufikia idadi ya wabunge wanaohitajika kuuidhinisha.
Visa vya kuahirishwa kwa mjadala na kutopigiwa kura kwa mswada kuhusu utekelezwaji wa takwa la Katiba ya Kenya kuhusiana na usawa wa kijinsia kunaonyesha jinsi suala la jinsia lilivyo na changamoto nyingi.
Kwa sasa bunge la kitaifa lina wanawake 75, kati ya hao 22 wamechaguliwa , sita wameteuliwa na wengine 47 wamechaguliwa kama waakilishi wa wanawake.
Hii ina maana kuwa bunge la Kenya linahitaji wabunge 41 wa kike ili kufikia 117, ama theluthi moja, ya wabunge 349.
Bunge la seneti kwa upande mwingine lina wanawake watatu waliyochaguliwa na wengine 18 waliyoteuliwa.
Hii ina maana kwamba ili kufikia idadi inavyoeleza katiba, bunge la sasa linahitaji kuwateua wanawake wengine 53.
Katiba ya Kenya ilitoa maelekezo na kutoa nafasi kwa wanawake 16 katika bunge la seneti na viti 53 katika bunge la kitaifa pamoja na wanawake 47 wanaowakilisha kaunti 47 za Kenya.
Sababu za kihistoria zilatajwa kuwa changamoto kubwa kwa wanawake kuchaguliwa katika nafsi za uongozi.
Bado kuna changamoto za kila aina zinazowatatiza wanawake na kuwafanya kutoshiriki na kupata nafasi za uongozi wa kisiasa.
Wadadisi wa kisiasa wanasema kuwa changamoto hizo haziwezi kushughulikiwa mara moja.
Kwanini kuna walakini?
Kwa mujibu wa mchambuzi wa siasa za Kenya Profesa Hezron Mogambi kuna sababu kadhaa ambazo zilifanya marekebisho ya kikatiba kuwa na walakini na huenda yasifaulu hata siku zijazo.
''Katiba ya Kenya haikuwazia pendekezo la kupanua bunge la Kenya kwa kuongeza idadi ya wabunge ili kufikia hitaji hili la masuala ya kikatiba kuhusu jinsia.''
Profesa Mogambi anaongeza kuwa kubadilisha katiba wakati ambapo kinachohitajika ni sheria ya bunge ni kwenda kinyume ya katiba yenyewe.
Kifungu cha 27(6) cha katiba ya Kenya kinahitaji kuwa mipango yoyote ikiwemo ile ya kisheria na hatua na sera nyingine zenye nia ya kusawazisha hali zichukuliwe na serikali.
'' Ipo haja kushughulikia masuala ya kihistoria ambayo yamekwamiza ufikiaji wa usawa kwa watu na makundi mbali mbali.'' anasema bwana Mogambi.
Baadhi ya wanawake, kwa sababu ya sababu fulani, wameweza kuzichukua nafasi zote zilizowahi kutolewa na hali hii kwa niaba ya wale waliotengwa kama ilivyoelezwa na kifungu 27 cha katiba ya Kenya ili kwamba mahitaji ya theluthi mbili ya kijinsia ndiyo ya kipekee yanayohitaji kushughulikiwa.
Ikiwa sheria ya uajiri nchini Kenya itabadilishwa kushughulikia hitaji la kijinsi la theluthi mbili katika masuala ya uajiri katika sekta ya umma, nchi ya Kenya itapiga hatua kubwa katika harakati za kushughulikia masuala ya kijinsia na wanawake kwa jumla.