Operesheni ya usalama yaidhinishwa Zanzibar kukabiliana na uhalifu

Chanzo cha picha, GULSHAN KHAN
Operesheni ya kupambana na uhalifu imeanzishwa katika mkoa wa mjini magharibi Zanzibar.
Lengo ikiwa ni kuzuia matukio mbalimbali makubwa ya uhalifu ikiwemo ugaidi.
Operesheni hii inafanyika pia wakati baadhi ya miji mikubwa katika eneo la Afrika mashariki ikiimarisha ulinzi, kutokana na kukumbwa na matukio ya uhalifu ikiwemo tishio la ugaidi.
Mkuu wa mkoa wa mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud ameiambia BBC operesheni hiyo ya kupambana na uhalifu imegawanywa katika makundi mengi, ikiwemo uhalifu katika viashiria vyovyote vinavyohusisha masuala ya ugaidi.
Hili linafanyika kwa kukagua maficho mbalimbali ikiwemo misitu, mapango, maeneo ya mikoko, katika maeneo ya Pwani, na mengineyo yanayoweza kuwa maficho kwa wahalifu.

Chanzo cha picha, ayoubmahmoud_
Operesheni hio pia imewagusa madereva wa piki piki ambao wanafanya biashara kinyume na sheria.
Katika siku za hivi karibuni usafiri huo umehusishwa na matukio ya ujambazi na ukabaji ikiwemo kushajihisha biashara ya ukahaba kutokana na baadhi ya abiria wanaowabeba ambao wanatuhumiwa kwa vitendo hivyo.
Zaidi ya piki piki 80 zimekamatwa mpaka sasa kufuatia operesheni hiyo.
Kuhusiana na matukio ya mauaji, karibu watuhumiwa 12, wamekamatwa ambao wanadaiwa kufanya matukio hayo ya uhalifu katika mikoa mingine ya Tanzania bara.

Chanzo cha picha, DEA / G. COZZI
Huku wengine wakiwa tayari wamepelekwa katika mikoa wanayodaiwa kutenda uhalifu huo.
Mkuu huyo wa mkoa wa mjini Magharibi, amesema operesheni inayofanyika sasa ni kwa ajili ya kuchukua tahadhari za kiusalama ili kujikinga na matukio ya uhalifu, ikiwemo ugaidi.
''Waswahili wanasema kwamba unapoona mwenzako ananyolewa na basi wewe unachopaswa ni kutia maji.., Wenzetu wa nchi ya jirani tumeona nini kinatokea kwa upande wa makundi haya ya al Shabaab nasisi hapa tusijione kama tuko dunia nyingine...'' amesema Ayoub Mohammed Mahmoud.

Amesema mkoa wa mjini Magharibi ndio mkoa wa mama wa visiwa vya Zanzibar, hivyo ipo sababu ya kujikinga na sio kusubiri mpaka yatokee.
Operesheni hii ya kuondoa uhalifu katika mkoa wa Mjini Magharibi ilianza February 2, mwaka huu.
Taarifa Nyingine:
Visiwa vya Zanzibar kwa kiasi kikubwa uchumi wake umekuwa ukitegemea sekta ya Utalii, hali inayofanya kila mwaka kupokea maelfu ya wageni wanaokuja kutembelea visiwa hivi kutoka maeneo mbalimbali ya dunia.
Hali hiyo pia imefanya vijana wengi kutoka maeneo mbalimbali nje ya visiwa hivyo, kuingia visiwani humo kusaka ajira hususan katika sekta zinazohusiana na masuala ya utalii.












