Benki ya Dunia inasema viwango vya elimu vimeshuka Uganda na Tanzania

wanafunzi wa shule ya msingi Uganda

Ripoti mpya ya hali ya elimu Barani Afrika iliyotolewa na Benki ya dunia imeziorodhesha nchi za Uganda na Tanzania katika kundi la pili la mataifa yenye kiwango cha juu cha watoto wanaoachia katikati masomo ya shule ya msingi.

Mkuu wa Benki ya dunia wa masuala ya elimu katika kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Sajitha Bashir amesema mataifa yaliyo katika eneo la kusini mwa jangwa la sahara, kwa miaka 25 iliyopita yameangazia zaidi kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya msingi.

Hata hivyo amesema ipo haja ya mataifa hayo kuimarisha mpango huo kwa kuwasaidia watoto hao kujifunza mengi zaidi kuliko masomo ya msingi ya kawaida.

''Kuwapeleka watoto shule pekee haitoshi. Mfumo wa elimu sharti izingatie mambo muhimu katika jamii ambayo mara nyingi hayajumuishwi katika masomo ya kawaida ya msingi. Bila ya kuzingatia suala hilo viwango vya elimu katika eneo la kusini mwa jangwa la sahara vitaendelea kushuka'' Bi Bashir alisema.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo,waziri wa elimu wa Uganda, Bi. Janet Museveni alisema machafuko yaliyoshuhudiwa nchini humo miaka ya 1960 hadi mwisho wa miaka1980 ziliharibu kabisa mifumo ya elimu.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni na waziri wake wa elimu Janet Museveni
Maelezo ya picha, Rais wa Uganda Yoweri Museveni na waziri wake wa elimu Janet Museveni

Bi Museveni ameongeza kuwa ilichukua nchi hiyo takriban miongo miwili kukabiliana na changamoto hizo.

''Tumeanza hivi karibuni kuimarisha viwango vyetu vya elimmu na safari hiyo haijakuwa raihisi kwetu''

Uganda ilijivunia kuwa na elimu nzuri katika kanda ya Afrika Mashariki. Viongozi wengi wamesomea hapa. Cha kusikitisha ni kwamba sasa ripoti hii imetuorodhesha katika kundi la pili. Tuliharibu nchi yetu wakati majirani zetu walikuwa wakiimarisha mifumo yao ya elimu.Tunaomba wahisani watakaotusaidia katika safari yetu ya kufikia kiwago cha elimu kinachohitajika duniani''

Mataifa yaliyorodheshwa katika makundi ya 2, 3, na ya 4 yanapambana kufikia kiwango kinachohitajika duniani cha 50% ya watoto kujiunga na shule.

Moja ya masuala muhimu ni lugha ya inayotumika kufunza au kutathmini uelewa wa mwanafuzi.

Katika mataifa ambayo watoto wanasomeshwa kwa lugha asilia kiwango cha uelewa kiko juu.

Kwa nini iwe hivyo?

Mataifa ya eneo la kusini mwa jangwa la sahara yaliyoorodheshwa katika kundi la 2 na la 3, yanakabiliwa na changamoto kubwa kuwasomesha watoto kutoka gredi ya kwanza hadi ya tisa.

Kuacha shule mapema au kumaliza masomo ya msingi na ya sekondari hakuhusiani kwa vyovyote na kuimarika kwa viwango vya elimu.

Tanzania

Chanzo cha picha, ROBERTO SCHMIDT

Kuna baadhi ya mataifa yaliyokuwa na changamoto nyingi miaka 25 iliyopita lakini yamejikakamua na kujitoa katika kundi la mataifa yaliyo na idadi kubwa ya watoto wanaoachia katikati masomo ya msingi.

Mataifa ya eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara yafanye nini kuimarisha elimu na kupunguza ukosefu wa usawa katika elimu?

Kujibu swali hili utafi huo ulizingatia vigezo vinavyofanya kazi mataifa yaliyo na uchumi mdogo yale yenye uchumi wa kadri.

Pia ilichambua tafiti za hivi karibuni kutathnini usawa wa elimu kati ya watoto wavulana na wasichana.

Licha ya kupungua kwa penge la usawa katika elimu ya wavulana na wasichana bado mataifa mengi ya eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara bado yanakabiliwa na changamoto hasa katika kiwango cha elimu ya shule ya upili.

Katika mataifa mengi ya Afrika ndoa za utotoni zimewazuia watoto wasichana kufika kiwango cha shule ya upili.

kufikiri

Chanzo cha picha, TONY KARUMBA

Nini kifanyike

Watunzi wa sera wameshauriwa kutumia lugha maalumu kuwafunza watoto shuleni.

Baadhi ya nchi huwa na lugha zaidi ya moja za kufundishia.

Kwa mfano, nchini Tanzania, elimu ya msingi na elimu ya watu wazima hutolewa kwa lugha ya kiswahili.

Lakini elimu ya sekondari na ya chuo kikuu hutolewa kwa Kiingereza.

Hata hivyo serikali ya Tanzania iko mbioni kuelekea zaidi kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya kufundishia kati ngazi zote.

Nchini Kenya na Uganda lugha ya kufundishia ni Kiingereza isipokuwa kwa baadhi ya masomo.

Nchi ya Rwanda ilibadili lugha yake ya kufundishia kutoka Kifaransa hadi Kiingereza.

Nchi nyingi za Ulaya zinatumia lugha za nchi zao kama lugha za kufundishia.

watoto wa shule ya msingi Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images

Mengine ya kuzingatia ni pamoja na

  • Kujenga shule karibu na maeneo ya vijijini.
  • Kubuni mpango wa kusomesha kwa zamu hasa shule za mijini zinazokabiliwa na idadi kubwa ya wanafunzi.
  • Kufanyia marekebisho mitaala wa masomo. Mitaala inayotumwa kufundisha masomo ya shullle ya upili katika nchi nyingi za kusini kwa jangwa la sahara zilibuniwa miaka ya 1970.
  • Kuongeza idadi ya madarasa za katika shule za msingi zilizopo
  • Kuhakikisha shule zinatenga sehemu za kujisaidia kwa watoto wa kiume na wakike. Ukosefu wa vyoo na maji umetajwa kuwa chanzo cha wasichana kugoma kuenda shuleni
  • Kutumia teknolojia ya kisasa kuimarisha mafunzo na mfumo wa elimu