Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
New York Times lashutumiwa kwa kuchapisha picha za maiti katika shambulio Kenya
Gazeti la New York Times limeshutumiwa vikali kwa kuchapisha picha za miili ya watu waliopoteza maisha katika shambulio la hoteli ya kifahari ya DusitD2 jijini Nairobi.
Wahalifu wenye silaha za moto na mabomu walivamia viunga vya hoteli hiyo Jumanne saa 9 alasiri.
Gazeti hilo lenye makao makuu yake nchini Marekani limechapisha picha za marehemu wakionekana dhahiri kuwa na matundu ya risasi kwenye miili yao na kulowa damu.
Wakenya walimimina hasira na kukirihishwa kwao kwa hatua hiyo ya NYTimes kwa kuandika ujumbe katika mitandao ya kijamii ikwemo Twitter.
Baadhi hata walilinganisha namna walivyoripoti matukio ya uhalifu nchini Marekani tofuati na walivyofanya kwa mkasa huu Kenya.
Wameeleza kwamba hatua ya gazeti hilo ilikosa heshima.
Baada ya shutuma hizo kushika kasi, uongozi wa gazeti hilo ulitoa taarifa ya kujitetea wakisema lengo lao ni "kuonesha uhalisia wa tukio zima japo picha zinaweza kuwa za kuogofya."
Wameendelea kufafanua kwamba wao hufanya vivyo hivyo wanaporipoti matukio kama hayo kwengineko duniani.