Chombo cha anga za juu cha China chafanikiwa kuotesha mbegu za pamba mwezini

Chanzo cha picha, AFP/CHONGQING UNIVERSITY
Mbegu ambazo zimepelekwa mwezini na chombo cha utafiti wa anga za juu cha Chang'e-4 zimechipua, mamlaka jijini Beijing zimethibitisha.
Hii ni mara ya kwanza kwa mmea wa kibaolojia kuchipuwa mwezini, na ni hatua inayofungua njia ya tafiti zaidi za kisayansi mwezini.
Chang'e 4 pia ndio chombo cha kwanza kutafiti sehemu ya mbali zaidi ya mwezi, ambayo haitazamani na uso wa dunia.
Chombo hicho kilitua mwezini Januari 3 kikiwa kimebeba vifaa vya kuchunguza jiolojia ya eneo hilo.
Mimea imekuwa ikioteshwa kwenye kituo cha kimataifa cha anga za juu lakini haijawahi kujaribiwa mwezini.
Uwezo wa kuotesha mimea mwezini itakuwa ni sehemu muhimu ya utafiti wa muda mrefu wa mwezi, na pia safari ya kuelekea Mars ambayo inakadiriwa kuchukua miaka miwili na nusu.
Hii inafungua milango ya uwezekano wa wanaanga kuweza kuzalisha chakula chao wenyewe wakiwa anga za mbali na kupunguza uhitaji wa kurudi duniani ili kufuata chakula.

Chombo hicho cha Uchina kilibeba udongo wenye mbegu za pamba, viazi na hamira.
Mimea hiyo imo ndani ya mabakuli yaliyofungwa. Mazao hayo yanatarajiwa kujitengenezea kinga na kujikuza katika mazingira yake itakayojitengenezea.

Je mwezi utaathirika?
Swali kuu linaloulizwa ni iwapo jaribio hilo la kuotesjha mimea litaleta madhara. Lakini utafiti huo ambao unafanywa kwa ushirikiano wa vyuo 28 vya Uchina unalenga kupata taarifa za namna gani viumbe hai vinavyotumia hewa na kuzalisha nguvu ya baianuwai (hasa mimea) vinaweza kukua mwezini.
Mimea hiyo iliyohifadhiwa vizuri imewekewa hewa, maji na virutubisho vingine vitakavyoisaidia kukua. Changamoto kubwa kwa wanasayansi wa Uchina ni kubadilika kwa hali ya hewa mwezini ambapo huwa baina ya -173C and 100C ama zaidi.
Wanasayansi wengi wanaamini kuwa uwezekano wa kuathiri mwezi ni mdogo kutokana na utafiti huo. Na pia wanasisitiza kuwa tayari kuna mifuko takribani ya 100 ya uchafu iliyoachwa na binadamu waliotua mwezini na chombo cha Marekani cha Apollo.

Fred Watson, mwananga kutoka Australia ameiambia BBC kuwa kuchipua huko kwa mbegu hizo ni habari njema.
"Hii inatueleza kuwa yawezekana kusiwe na shida kwa wanaanga kuzalisha chakula chao wenyewe mwezini katika mazingira salama."

Chanzo cha picha, CLEP
"Kuna umuhimu mkubwa sana katika suala hili, hususani kuutumia Mwezi kama kituo cha kurusha vyombo kwenda sayari ya Mars sababu Mwezi upo karibu na Dunia ," amesema Watson.
Profesa Xie Gengxin, ambaye ndiye msanifu mkuu wa utafiti huo amenukuliwa na gazeti moja la Uchina akisema wanalichukulia kwa umuhimu suala la kuishi anga za juu kwa siku za usoni.
"Kujifunza namna ambayo mimea inakuwa katika mguvu za mvutano wa asili ndogo kutatuwezesha kuweka msingi wa uwepo wetu wa baadae kwenye anga za juu.
Chombo hicho kilichukua siku 20 kutoka Duniani mpaka Mwezini na kimeshapiga picha 170 ambazo zimezituma duniani na zinafanyiwa kazi, shirika la habari la Xinhua linaripoti.














