Laurent Gbagbo: Mahakama ya ICC yamuachilia huru rais wa zamani wa Ivory Coast

Laurent Gbagbo

Chanzo cha picha, AFP

Mahakama ya kimataifa ya ICC imemuachilia huru aliyekuwa rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo.

Alishtakiwa na makosa ya uhalifu dhidi ya binaadamu kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi zilizowaacha takriban watu 3000 wakiwa wameuawa huku watu 500,000 wakiwachwa bila makao katika uchaguzi uliozongwa na utata wa 2010.

Bwana Gbagbo alikamatwa 2011 katika eneo la kujifichia la Ikulu ya rais na wanajeshi wa UN pamoja na wale wanaoungwa mkono na Ufaransa waliokuwa wakimuunga mkono mpianzani wake Alassane Ouattara.

Alikuwa rais wa kwanza wa zamani kushtakiwa katika mahakama ya ICC.

Je Gbagbo alishtakiwa na mashtaka gani?

Ghasia hizo za mwaka 2010 nchini Ivory Coast ambayo ndio mzalishaji mkubwa wa Cocoa duniani , zinajiri baada ya bwana Gbagbo kukataa kukubali kwamba alikuwa amepoteza katika uchaguzi huo uliozongwa na utata kwa mpinzani wake bwana Outtara.

Majaji wa mahakama ya ICC waliamuru siku ya Jumanne kwamba alikuwa hana kesi ya kujibu kwa sababu upande wa mashtaka ulikuwa umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.

Wametaka aachiliwe mara moja.

Jaji Cuno Terfusser aliyekuwa akiendesha kesi hiyo alisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kwamba hotuba za Gbagbo zilihusisha ama hata kuamrisha madai ya uhalifu uliotendeka.

Wafuasi wa Gbagbo walisherehekea katika maeneo ya umma kufuatia tangazo hilo.

Wakati wa ghasia hizo kulikuwa na ghasia mbaya ambazo zilisababisha mauaji katika mji wa Abidjan uliopo kusini , huku mamia wakiuawa katika mji wa Magharibi wa Duekoue.

Waendesha mashtaka walimshutumu bwana Gbagbo na mashtaka manne ya uhalifu dhidi ya binaadamu , mauaji, ubakaji pamoja na dhulma nyengine za kingono pamoja na vitendo vya kikatili.

Alikana mashtaka hayo ambayo alisema kuwa yalichochewa kisiasa.

Waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wanaopinga kuachiliwa kwa Gbagbo

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wanaopinga kuachiliwa kwa Gbagbo

Je ni pigo kwa ICC?

''Wakati kesi yoyote inayohusisha mauaji ya halaiki inapoanguka katika ICC , inaharibu umaarufu wa mahakama hiyo .

Kulingana na Mark Kersten , mwanzilishi wa haki katika mzozo, aliambia mwandishi wa BBC Anna Holligan.

Wafuasi wa bwana Gbagbo

Chanzo cha picha, AFP

Wengi wana wasiwasi kwamba mahakama hiyo inaonekana kuwa taasisi ambapo waasi pekee wanaweza kushtakiwa , aliongezea.

Kesi zilizoanguka katika mahakama hiyo ni pamoja na ile ya aliyekuwa makamu wa rais wa DR Congo Jean Pierre Bemba na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Kwa upande mwengine uamuzi huo unaonyesha uhuru ulio na majaji hao na inakuwa vigumu kwa wale wanaoogopa mkono mrefu wa ICC kusema kwamba mahakama hiyo ni silaha ya upendeleo na yenye lengo ya kuwalenga viongozi wa Afrika.