Brexit: Theresa May anakabiliwa na 'kura muhimu' kuhusu makubaliano yake

Chanzo cha picha, AFP
Wabunge Uingereza wanajitayarisha kupiga kura kwa iwapo kuunga au kutounga mkono mpango wa Theresa May wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya.
Kura hiyo inayotajwa kuwa "Kura yenye umuhimu" itafanyika baadaye leo wakati mjadala wa siku tano kuhusu Brexit ukikamilika.
Bi May amewataka wanasiasa kuunga mkono mpango wake au kuhatarisha "kuwavunja moyo raia wa Uingereza".
Lakini huku wabunge wake mwenyewe wakitarajiwa kujiunga na wa vyama vya upinzani kupiga kura dhidi ya mpango huo, inatarajiwa pakubwa kwamba mpango huo hautofaulu.
Wabunge pia watapata fursa ya kutoa mapendekezo ya marekebisho ambayo yanaweza kuunda upya mpango huo kabla ya kura kuanza 19:00 kwa saa ya GMT.

Chanzo cha picha, PA
Waziri mkuu aliwahotubia wabunge wake Jumatatu jioni katika jitihada za mwisho kujaribu kupata uungwaji mkono kwa mpango wake - unaojumuisha mpango wa kujitoa kwa misingi ya ambavyo Uingereza itajitoa kwenye Muungano wa Ulaya na tangazo la kisiasa kwa uhusiano wa siku zijazo.
Awali, katika bunge la wawakilishi, alisema: "Hauko imara kabisa lakini wakati historia itakapoandikwa, watu watatazama uamuzi wa bunge hili na watauliza, 'Je tuliwajibika kuhusu kura ya taifa hili kujitoa katika EU, tuliuchunga uchumi wetu, usalama na muungano au tuliwavunja moyo raia wa Uingereza?'"
Bi May pia alijaribu kuwashawishi wabunge kuhusu mpango wenye mbadala wenye mzozo wa kuepuka kurudishwa kwa ukaguzi wa mipakani kati ya Uingereza na Ireland.
Ametaja hakikisho jipya kutoka kwa EU kwamba mpango mbadala wa forodha unaopendekezwa utakuwa ni wa muda tu , na iwapo utaidhinishwa utadumu kwa "muda mfupi iwezekanavyo".
May atalihotubia bunge Jumanne asubuhi, kabla ya mjadala kuendelea mwendo wa mchana.

Lakini wabunge wengi wa Tory na wa Democratic Union wanapinga vikali mpango huo.
Takriban wabunge 100 wa Conservative na 10 wa Democratic Union huenda wakajiunga na chama cha Leba na vyama vingine vya upinzani kupiga kura dhidi ya mpango huo.
Mpango huo ulipata pigo kubwa katika bunge la Malodi Jumatatu usiku, wakati wabunge walipounga mkono hoja ya chama cha Leba kwa kura 321 dhidi ya 152.
Hatahivyo, wabunge watano wa Conservative ambao wamekuwa wakosoaji wa mpango wa kujitoa sasa wanasema wataiunga serikali mkono , pamoja na wengine watatu wa chama cha Leba na wa kujitegemea, Frank Field.
Mapendekezo kadhaa ya marekebisho yamewasilishwa na wabunge kwa mpango wa May kujaribu kuufanyia mageuzi bungeni.

Nini kitakachofanyika baada ya hapa?
Iwapo wabunge watapinga mpangu huu, Bi May ana vikao vya siku tatu tu kuweza kurudi bungeni na mpango mbadala.
Baadhi wanasema huenda akaelekea Brussels Jumatano kujaribu kushauriana zaidi na EU kabla ya kurudi tena katika bunge la wawakilishi kutoa taarifa kuhusu mpango mpya kufikia Jumatatu.
Hili baada ya hapo, huenda likapigiwa kura na wabunge.
Iwapo hili pia halitofaulu, kuna pendekezo lililowasilishwa na wabunge wakuu wa chama cha Conservative Nick Boles, Sir Oliver Letwin na Nicky Morgan wa "Mswada wa pili wa kujitoa katika Muungano wa Ulaya". Hili litawapa mawaziri wiki tatu za ziada kuja na mpango mwingine na kuupitisha bungeni.
Iwapo hili nalo bado halitofaulu, wanapendekeza kuipa kamati ya mashauriano jukumu la kuja na mpango wa kuafikiana utakaotokana na vyama vya upinzani pamoja na chama cha Conservative.
Pendekezo hili pia bado litahitaji kupigiwa kura bungeni.















