Hezron Mogambi: Je, pendekezo jipya la kugawa raslimali litasaidia kupunguza ufisadi Kenya?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Hezron Mogambi
- Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi
Baada ya kuripotiwa kwa msururu wa visa vya ufisadi katika kaunti mbali mbali nchini Kenya, tume ya kugawa raslimali nchini Kenya (CRA) imetoa mapendekezo yanayolenga kuhakikisha matumizi bora ya fedha na uwajibikaji kwenye kaunti zote 47 za Kenya.
Pendekezo hili ambalo litakuwa mbinu ya tatu kutumika kugawa raslimali kwa kaunti nchi Kenya iwapo litapitishwa na Seneti, linachukua msimamo wa kuzingatia kufadhili sekta mahususi. Pendekezo hili ambalo sasa linaelekezwa kwa umma kutoa maoni yake kabla ya kupelekewa kwa kwa bunge la seneti ili kujadiliwa.
Tofauti na mbinu zilizotumiwa hapo awali ambapo idadi ya watu, ukubwa wa kaunti, hali ya umaskini na usawa wa ugawaji, pendekezo la sasa ambalo ni la tatu tangu mwaka wa 2010, zaidi ya kuzingatia idadi ya watu, hali ya umaskini na ukubwa wa kaunti, linafungamanisha vipengele vya ugawaji pesa na utoaji huduma.
Kulingana na Tume ya kugawa Raslimali Nchini Kenya (CRA), mfumo huu utatumika katika kugawanya Sh335 bilioni ambazo zimepangiwa kaunti 47 katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020.
Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, utaratibu wa ugawaji fedha miongoni mwa kaunti 47 unafaa kuangaliwa upya kila baada ya miaka mitano ingawa ulidurusiwa miaka mitatu baada ya katiba ya Kenya ya mwaka wa 2010 ambayo ilileta mfumo wa kaunti nchini Kenya.
Katika pendekezo hilo, CRA imeeleza kuwa ingependa kugawa pesa miongoni mwa kaunti katika misingi ya mahitaji ya kila kaunti ili kuhakikisha usawa na haki, kuwasaidia maskini kuwafikia wengine waliopiga hatua, pamoja na kuzingatia matokeo ya matumizi na uwekezaji wa awali.
"Fomula hii inapendekeza makadirio ya matumizi kulingana na huduma zilizogatuliwa. Ni tofauti na zile za awali, huku fomula inayopendekezwa sasa ikilenga kuupa uzito uhusiano uliopo kati ya majukumu ya kikatiba ya kaunti na pesa zinazotumwa kwa kaunti mbali mbali," mwenyekiti wa CRA Jane Jane Kiringai alieleza jijini Nairobi kuhusu pendekezo hilo jipya.
Pendekezo ya CRA lilitayarishwa likiwa na nia ya kuboresha utoaji huduma, kuhakikisha maendeleo ya kuichumi na kuharakisha na kuzawadi usimamizi bora wa kifedha katika kaunti mbali mbali.
Itakumbukwa kwamba mkaguzi mkuu wa matumizi ya pesa za serikali nchini Kenya amekuwa akizishutumu kaunti kwa ufisadi na utumizi mbaya wa pesa za umma. Ripoti ya Tume ya Maadili na ufisadi nchini Kenya ya mwaka uliopita inaeleza kuwa utoaji tenda, uajiri, na huduma nyingine kwenye kaunti za Kenya unahusisha ufisadi wa kiwango cha juu.
Kulingana na pendekezo jipya, utoaji huduma katika sekta ya afya imepewa uzito ama alama asilimia 15. CRA ilijumuisha wagonjwa wasio na bima, wanaolazwa kwenye hospitali na wale wanaopokea huduma na kuondoka kama vigezo vya kufikia asilimia hii.
Katika sekta ya kilimo, tume ilifikia mahitaji ya matumizi kwa kuzingatia idadi ya jumla ya wakaazi ama familia kuhusiana na uhitaji wa ushauri wa huduma za kilimo na usalama wa chakula ili kufikia asilimia 10 inayopendekezwa. Pendekezo hili lina maana kuwa kila familia inatengewa shilingi 4.
Maji yamepewa uzito wa asilimia 3 kama huduma za miji. Majukumu mengine yote ya kaunti yamepewa asilimia 18. Kuhusiana na huduma nyingine na maendeleo sawia, CRA imependekeza barabara (aslimia 3), Ardhi (asilimia 8) Umaskini (asilimia 15) kama kiashirio. Pia, CRA itazizawadi kaunti kwa ukusanyaji wa ushuru na matumizi mema ya raslimali chini yake.Iwapo pendekezo la CRA litapitishwa na bunge la seneti, kaunti zitapewa Shilingi 20 kwa kila Shilingi 100 itakazokusanya ushuru.
Hata ingawa serikali za kaunti zina uwezo wa kuamua jinsi ya kutumia pesa zilizopewa na serikali kuu, CRA inapendekeza masuala mengi ya kuzingatia katika matumizi ya pesa hizo katika pendekezo hili jipya. Pendekezo hili la tatu linaeleza kuwa raslimali zinafaa kutumiwa kulingana na majukumu yaliyogatuliwa huku pesa nyingi zikiendea sekta ya afya na kilimo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pendekezo hili la kufadhili sekta mahususi limepingwa na baadhi ya wadau ambao wameapa kuhakikisha kuwa linakataliwa katika bunge la seneti wakati litakapojadiliwa.
Hata hivyo, mwenyekiti wa CRA, Jane Kiringai anatumai kuwa pendekezo la tume yake litapelekea matumizi na usimamizi mzuri wa raslimali pamoja na kuhakikisha kuwa ni miradi inayofaa tu inapewa kipau mbele na kaunti. Aidha, pendekezo hili litazifanya kaunti kuzingatia mbinu za kukusanya ushuru kwani zile zitakazokusanya vizuri zitazawadiwa.
Mombasa kupunguziwa
Pendekezo hili la kugawa pesa kwa kaunti likitumika, Nairobi itapokea Sh335.67 bilioni kati ya pesa zilizotengewa kaunti ambazo ni Sh17 bilioni, nyongeza kutoka kwa Sh16 bilioni za sasa. Nakuru itachukua nafasi ya pili ikichukua nafasi ya kaunti ya Kilifi, ikiwa imepewa Sh11.7 bilioni, kutoka Sh9.45 bilioni. Kaunti ya Turkana, ambayo hapo awali ilikuwa kaunti ya pili kupata pesa nyingi zaidi katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018, itachukua nafasi ta tatu katika mapendekezo haya ikipenekezewa Sh11.69 bilioni.
Kaunti ya Kakamega inachukua nafasi ya nne ikiwa imetengewa Sh11.3 bilioni. Kaunti nyingine ambazo zina raslimali kama vile Meru zitapanda kwa Sh1.33 bilioni, Kisumu (Sh688 milioni) na Kiambu (Sh699 milioni), miongoni mwa kaunti nyingine. Ikiwa pendekezo hili litapitishwa na bunge la seneti, kaunti kama vile Mandera zitapunguziwa pesa ambazo zitapokea kwa Sh1.3 bilioni, Lamu kwa Sh1.09 bilioni, Isiolo (Sh145 milioni), Wajir (Sh514 milioni), Tana River (Sh285 milioni), Kilifi (Sh1.43 bilioni), na Kwale (Sh1.02 bilioni).
Ikizigatiwa mgao wa pesa kwa usawa na haki, Lamu ndio kaunti kaunti ya kwanza, huku kila mkaazi akipokea angalau Sh34,972. Ikifuatwa na Isiolo kila mkaazi Sh27,445 na Marsabit Sh24,069.
Hata hivyo, kaunti zenye idadi kubwa ya idadi ya watu zinapata mgao wa chini wa pesa kwa kila mkaazi. Katika kaunti ya Nairobi ikiwa na idadi ya watu wapatao 3.1 million kulingana na takwimu za 2009, kila mkaazi akipata Sh5,032 kama mgao kwa kila mmoja wao ikifuatwa na Kiambu Sh5,772 ikiwa na watu wapatao 1.6 milioni.
Tayari magavana kutoka kaunti ambazo mgao wao wa pesa utapungua wameshutumua pendekezo hilo la CRA wakiwemo Ali Roba (Mandera), Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi).

Uchanganuzi wa jinsi CRA inavyopendekeza kugawanya pesa kwa kaunti mbalimbali na vipengele inavyotumia kunaonyesha kuwa vipengele hivyo ni halisi kulingana na uchanganuzi wa mahitaji ya matumizi badala ya idadi ya watu na ukubwa wa kaunti kama ilivyokuwa katika fomula zilizotumiwa hapo awali.
Ni wazi kwamba ingawa idadi ya watu inapewa uzito zaidi ya vipengele vingine katika kuamua mahitaji ya pesa, jambo hili limegawanywa ili kuhakikisha kuwa masuala mahusisi ya huduma zinazotolewa yamehusishwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni wazi pia kuwa tofauti zinazozuka kila mara kuhusiana na idadi ya watu nchini Kenya kisiasa, bila shaka kutoka na pingamizi kubwa kuhusiana na kipengele chenyewe kwani data itakayotumiwa na CRA kuamua masuala haya pia ni changamoto nyingine.
Pia, mpango huu uliopendekezwa unatoa mgao sawa wa asilimia 20 kwa kila kaunti kwa kuzingatia kipengele na ukweli kwamba kuna baadhi ya huduma ambazo gharama yake ni sawa katika kaunti zote nchini.
Aidha, msingi wa umaskini umebakia katika asilimia 15. Wachanganuzi na wahakiki wa kiuchumi wanasema kuwa pendekezo hili halitoi hamasa kwa ukuaji katika kaunti lakini CRA inasema kuwa nia hasa ya pendekezo hili ni kusawazisha ukuaji sawa kote nchini Kenya.
Kuboresha huduma
Suala la ukubwa wa kaunti pia limekuwa tata kama kipengele cha ugawaji pesa miongoni mwa kaunti kwani wengi wamekuwa wakihoji kuwa pesa zinatolewa kwa mahitaji na huduma kwa watu wala si ardhi.
Hata hivyo, ni bayana kuwa katika kaunti kubwa, masafa yana gharama zake katika utoaji huduma. Pia, pendekezo hili linatoa asilimia 2 kwa kaunti zitakazokusanya ushuru ipasavyo. Hili litasaidia kaunti zenye raslimali na ukusanyaji bora na kutafuta mbinu mbadala katika kuhakikisha kuwa serikali za kaunti zinakusanya ushuru kwa yakini.
Hata ingawa ni bayana kuwa pendekezo hili litakuwa na changamoto zake katika utekelezaji, ni wazi kwamba ni hatua nzuri katika kuboresha huduma kwenye kaunti mbali mbali na kuhakikisha kuwa raslimali adimu zinatumika ipasavyo. Hata hivyo, wajibu wa kuhakikisha kuwa ufisadi unapunguzwa bado litabaki kwa viongozi katika ngazi hizo, na pia kitaifa.
Prof. Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: [email protected]












