Hezron Mogambi: 'Wakati umefika kwa kila mmoja wetu kuwa mshirika katika vita hivi dhidi ya ufisadi'

Waandamanaji katika jiji kuu la Kenya, Nairobi

Chanzo cha picha, AFP/GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wanaharakati waandamanaji katika jiji kuu la Kenya, Nairobi
    • Author, Prof Hezron Mogambi
    • Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi

Huku vita dhidi ya ufisadi vikichacha nchi Kenya na maafisa wakuu wa serikali wakifikishwa mahakamni kujibu mashtaka, madai kuwa vita hivyo vinachukua mwelekeo wa kikabila yamezua mjadala nchini Kenya.

Katika siku za hivi karibuni, maafisa wakuu serikalini wakiwemo makatibu, wabunge, na maafisa wanasimamia mashirika ya seiklai wamefikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa ufisai katika mashirika wanayoyasimamia jambo ambalo limezua taharuki.

Hata hivyo, kuanza kuingizwa kwa siasa katika vita hivi ndio hatua ambayo imeanza kuonekana siku za hivi karibuni na kuzua mjadala huku makundi ya kidini yakidai kuwa zaidi ya shilingi za Kenya bilioni mbili huibwa kutoka kwa serikali kila siku.

Naibu Rais wa Kenya William Ruto akitoa maoni yake amekuwa akisisitiza kuwa vita dhidi ya ufisadi havifai kuingizwa siasa bali kuachiwa taasisi ambazo zimepewa jukumu hilo na katiba ya Kenya.

"Kuingizwa siasa kwa uchunguzi na mashtaka kutoka kwa watu ambao si mashahidi, wachunguzi ama viongozi wa mashtaka au majaji kunahujumu vita dhidi ya ufisadi," Naibu Rais alisema.

Maoni haya yemonekana na wengi nchini Kenya kuwa yenye kuwatetea maafisa wakuu kutoka jamii yake ambao wameshikwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi.

Waandamanaji

Chanzo cha picha, AFP/GETTY IMAGES

Msimamo huu wa Naibu Rais wa Kenya unatokea wakati baadhi ya washirika na wandani wake wanapopinga kushikwa kwa baadhi ya wakuu wa mashirika ya serikali kwa sababu ya ufisadi katika mashirika waliokuwa wakiziongoza.

Madai yamezuka sasa kwamba msukumo huo wa kuwakamata wanaoshukiwa kwa ufisadi unalenga maafisa wakuu wanaotoka kwa jamii ya Wakalenjin katika serikali.

Baadhi ya viongozi kutoka bonde la ufa ambao ni washirika wa Naibu Rais William Ruto wamedai kuwa kundi linaloongoza vita dhidi ya ufisadi linatumiwa vibaya kuwalenga wataalam kutoka jamii ya Wakalenjin.

Baadhi ya wachanganuzi nchini Kenya wanadai kuwa maafisa hao wakuu wamejikuta katikati ya vita vya kisiasa— kwa kuwa wao ni njia rahisi ya kumfikia kiongozi wao, Bwana Ruto.

Ikikumbukwa kuwa siasa za Kenya zina msingi ya kikabila, jinsi wataalamu kutoka jamii ya Kalenjin wanaoongoza mashirika ya serikali watakavyokuwa wakishikwa ndivyo azma ya Bwana Ruto ya kuwa Rais wa Kenya itakavyokuwa inatiwa doa.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametupilia mbali madai haya ya wanasiasa wa Bonde la Ufa kuwa vita dhidi ya ufisadi vinavyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta vinalenga watu wa jamii fulani.

Bwana Odinga amesema madai hayo hayana msingi kwani vita hivyo vinalenga watu binafsi ambao ni lazima wawajibike.

Alieleza kuwa watu wanapopata nafasi za kazi kwenye serikali, wanapata kama watu binafsi, na wakiiba, wanafanya hivyo kama watu binfasi.

Odinga amewaonya wale wote walioiba mali ya umma kujitayarisha kwa wakati mgumu kwa kuwa vita dhidi ya ufisadi havitalegezwa hadi wezi wote wa mali ya umma watakaposhikwa na kufungwa.

Uhuru Kenyatta

Chanzo cha picha, Alamy

Maelezo ya picha, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amewaonya viongozi kutoingiza siasa katika mapambano dhidi ya ufisadi

Rais Uhuru Kenyatta naye amekuwa akisisitiza na kuwaonya viongozi kuwa vita dhidi ya ufisadi vitaendelea na havifai kuingizwa siasa.

Amenukuliwa mara kadhaa akizungumzia suala hili tangu mwaka uanze na hasa baada ya kuamua kushirikiana na kiongozi wa upizani Raila Odinga.

"Hivi si vita vyangu dhidi yao, hivi ni vita dhidi ya uovu huo ambao unawafanya watu wetu wakose kazi na huduma za kimsingi. Ni uovu unaofanya Kenya kutoendelea na kupanga kwa kizazi kijacho," Rais Kenyatta alieleza mnamo Novemba.

"Hatutarudi nyuma katika vita dhidi ya ufisadi. Vita dhidi ya ufisadi veyenyewe havimlengi mtu ama kabila."

Katika maadhimisho ya siku ya Jamhuri nchini Kenya, Rais Kenyatta aliwataka Wakenya wote kuwa macho na kuviripoti visa vyovyote vya ufisadi kwa polisi.

Aliwataka wanahabari na wanaharakati wa kijamii kushirikiana katika kuvifichua visa vya ufisadi nchini kama njia ya kupigana dhidi ya ufisadi.

Rais Kenyatta sasa amewataka Wakenya wote kuripoti visa vya ufisadi kwa tume ya ufisadi na maadili, vyombo vya habari, na mashirika ya kijamii .

"Wakati umefika kwa kila mmoja wetu kuwa mshirika katika vita hivi dhidi ya ufisadi. Ni wakati wa kusema yametosha, awe polisi wa kawaida, gavana, karani ama waziri, jaji au mwanasiasa ," Rais Uhuru alisema akiwahutubia Wakenya siku kuu ya Jamhuri.

"Hakuna mtu yeyote ambaye akiwa afisni ana haki ya kuitisha hongo kutoka kwako ama kutumia vibaya kile ambacho wewe na mimi tumetoa jasho kutengeneza. Nimewaonyesha kwamba nimejitolea kwa jambo hili lakini sasa nataka kuona kujitolea kwenu.Msichoke kufanya yaliyo mema"

Wanaharakati wanamtaka Rais Kenyatta achukue hatua
Maelezo ya picha, Wanaharakati wanamtaka Rais Kenyatta achukue hatua

Vita hivi vya maneno nchini Kenya kuhusu vita dhidi ya ufisadi vinakuja wakati ambapo wakuu wa mashirika mengi wanaposhukiwa kuwa na ufisadi wakishikwa na kufikishwa mahakamani.

Maafisa wakuu wa mashirika ya serikali ikiwemo makatibu wa wizara mbalimbali wakuu wa mashirika ya serikali wameshikwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya ufisadi.

Kuna hofu kuwa vita vya maneno kuhusu ufisadi vimeanza kuchukua mkondo wa kisiasa na huenda juhudi hizo zikasabaratika kama ambavyo imekuwa ikitokea miaka ya nyuma.

Katika hatamu za Rais Moi na Rais Kibaki, vita dhidi ya ufisadi vilisambaratishwa na siasa nyingi jambo ambalo lilipelekea mashirika mengine kuanguka kifedha.

Katika muktadha huu, kuwepo katika nyadhifa za seikali kumechukuliwa kama njia rahisi ya kujipatia mali kwa urahisi na kuwa tajiri na kuonyesh wengine kupitia kwa magari ya kifahari, majumba makubwa ya kifahari, kutoa pesa nyingi kwenye michango na mengine ya kujitanua.

Matamshi ya wanasiasa kutoka bonde la ufa kwa mfano, yanaweza kuchukuliwa kuwa ni yenye lengo la kuleta uhasama wa kikabila miongoni mwa jamii mbali mbali.

Kiongozi wa mashataka ya umma, Noordin Haji na mkurugenzi wa idara ya makosa ya jinai George Kinoti, wamepongezwa pakubwa kwa mwamko mpya dhidi ya ufisadi.

Bwana Haji na mwenzake sasa wanawalenga wakuu serikalini na vigogo wengine wenye uwezo nchini Kenya.

Noordin Haji
Maelezo ya picha, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma nchini Kenya Bw Noordin Haji

Viongozi hawa wawili wamevutia uungwaji mkono na Wakenya wengi na kinachosubiriwa sana ni kushtakliwa na kufgnwa kwa wakuu wa mashirika ya serikali watakaopatikana na makosa ya ufisadi.

Itakumbukwa kwamba kwa muda mrefu, vita dhidi ya ufisadi nchini Kenya vimekuwa vikitatizwa na siasa za ukabila wakati viongozi wa mashairika na wakuu wengine wa serikali wanapokuwa wakifuata kutaka kujibu maswali. Mara nyingi wamekuwa wakijificha chini ya mwavuli wa jamii zao na kusema kuwa jamii zao "zinalengwa" na hivyo kuwashirikisha wanajamii wao katika kujitetea.

Hali hii imeifanya nchi ya Kenya kutatizwa pakubwa na ufisadi kufikia kupoteza mamilioni ya pesa kila mwaka jambo ambalo limepelekea umaskini mkubwa na matatizo mengine kama ukosefu wa ajira kwa vijana.

Ukosefu huu wa ajira kwa vinana wengin wa Kenya umkuwa tatizo sugu na kusababisha ukosefu wa usalama, suala ambalo ni chamgamoto kwa nchi nzima.

Takwimu zinaonyesha kuwa ripoti za mkaguzi mkuu wa matumizi ya pesa za serikali katika miaka mitano iliyopita, Wakenya hupoteza shilingi trilioni moja kila mwaka kwa ufisadi.

Hii ina maana kuwa katika mika mitano iliyopita, Kenya huenda imepoteza kiasi cha trilioni 5 za Kenya kupitia kwa wafisadi, taratibu mbovu za serikali zinazovuja, na wafanyikazi wa serikali walio wafisadi.

Dhahiri ni kuwa, vita dhidi ya ufisadi nchini Kenya vinapaswa kuendelea bila upendeleo wowote ikiwa Kenya inategemea kupiga hatua kimandeleo.

Hata hivyo, kwa kuwa siasa za Kenya zina misingi ya kikabila, itakuwa vigumu kuyatenganisha mawili haya maana wanasiasa ndio husukuma magurudumu ya ufisadi.

ProfMogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: [email protected]