Dermophis donaldtrumpi: Kiumbe anayeishi baharini na nchi kavu apewa jina Donald Trump

Chanzo cha picha, EnviroBuild / Getty Images
Kiumbe anayeweza kuishi baharini na katika nchi kavu amepewa jina la Rais wa Marekani Donald Trump, ingawa huenda kiongozi huyo asitake kuhusishwa na kiumbe huyo kutokana na sifa zake.
Amfibia huyo huwa anafukia na kuficha kichwa chake mchangani anapokabiliwa na hatari, jambo ambalo pengine limewashawishi wahusika kumpa kiumbe huyo jina la Trump kutokana na kiongozi huyo kukana kwamba shughuli za viwanda na za kibinadamu zinachangia mabadiliko ya tabia nchi.
Kiumbe huyo pia ni kipofu, hawezi kuona.
Mnyama huyo ambaye amepewa jina Dermophis donaldtrumpi, aligunduliwa katika eneo la Panama, na alipewa jina hilo na mkuu wa kampuni ya EnviroBuild ambaye alikuwa amelipa $25,000 (£19,800) kwenye mnada kupata fursa ya kumpa jina kiumbe huyo.
Kampuni hiyo imesema inataka kuhamasisha watu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.
"[Dermophis donaldtrumpi] huathiriwa sana na mabadiliko ya tabia nchi na kwa hivyo ni kiumbe aliye katika hatari ya moja kwa moja ya kuangamia kutokana na sera ya somo wake kuhusu mazingira," mwanzilishi mwenza wa EnviroBuild, Aidan Bell, amesema kupitia taarifa.

Chanzo cha picha, EnviroBuild
Kiumbe huyo mdogo ni wa aina ya caecilian, ambao ni viumbe watelezi wanaofanana na minyoo au nyoka, na huishi sana chini ya ardhi.
Bw Bell amesema tabia za kiumbe huyo zinashabihiana sana na za Trump.
"Kupuuza mambo (sawa na kuficha kichwa mchangani) humsaidia Donald Trump kukwepa maafikiano kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabia nchi," amesema.

Chanzo cha picha, Abel Batista / Rainforest Trust UK
Wanasayansi duniani wanakubaliana kwamba mabadiliko ya tabia nchi yanasababishwa na shughuli za kibinadamu.
Lakini Bw Trump, ambaye utawala wake umekuwa ukiendeleza matumizi ya mafuta yanayotokana na kaboni, amewatuhumu wanasayansi hao kwa kuwa na "ajenda ya kisiasa" na kutilia shaka kwamba binadamu wanahusika katika ongezeko la joto duniani.













