Claudia Wanjiru: Makovu yangu ndiyo urembo wangu, hayanizuii kuwa mwanamitindo

Claudia Wanjiru

Chanzo cha picha, VIN ARTS

    • Author, Faith Sudi
    • Nafasi, BBC Swahili

Claudia Wanjiru ni mwanamtindo mwenye makovu usoni. Makovu hayo aliyapata baada ya kunusurika mkasa wa moto akiwa mwanafunzi wa darasa la saba.

Kabla ya mkasa huo, Claudia alikuwa na ndoto ya kuwa mwanamitindo, ndoto ambayo amehakikisha ameitimiza licha ya kuwa na makovu usoni.

"Tulipokuwa kwenye hoteli tukiwekewa chakula, jiko la gesi lililipuka na mafuta yakanimwagikia usoni. Nilianza kukimbia nikitafuta maji".

Alichukuliwa kisha akapelekwa hospitalini. Alikuwa ameungua kwa asilimia kumi na nne usoni. Alikaa hospitalini kwa muda wa miezi mitatu. Hali hii ilifanya maisha yake kubadilika sana, hata kukosa marafiki.

"Baada ya kuungua, watoto ambao walikuwa wadogo kuniliko kwa umri, walikuwa wananiogopa, na wale ambao walikuwa wa rika langu, walikuwa wananicheka, wananitania. Nikiwa shuleni, nilikuwa napata barua za matusi na mwalimu akitupatia zoezi la kufanya kwa makundi, hakuna mtu alikuwa ananikubali tufanye naye pamoja," anasema.

Maelezo ya video, Claudia Wanjiru: Mimi bado mrembo na makovu yangu

Hali hii ilipelekea Claudia kukumbwa na msongo wa mawazo kwa sababu ya jinsi ambavyo watu walimtendea na kumsema.

"Watu walisema kwamba nilijaribu kubadilisha rangi ya ngozi yangu lakini dawa hizo zikakataa kufanya kazi. Wengine wakasema kwamba niko na Ukimwi. Nilikuwa najipendekeza kwa watu ili nipate marafiki, na mtu ambaye alikuwa anakubali kuwa rafiki yangu ana lengo fiche."

Wakati alipokosa marafiki, upweke ulimzidi, na ikamlazimu kutafuta njia za kujipunguza machungu.

Claudia Wanjiru

Chanzo cha picha, VIN ARTS

"Nilihisi hakuna mtu ananipenda, wazazi wangu na dada yangu mdogo pekee ndio walionipenda na ambapo wazazi wa mtu lazima wampende, hata ukimuuwa mtu, mzazi wako bado atakupenda tu."

Msongo wa mawazo ulipomzidia, Claudia akaiga tabia ya kujikata kutoka kwa filamu ambayo anasema kuwa ilikuwa na msichana ambaye alikosa marafiki, na akawa anajikata ili kutoa machungu ya upweke.

Machungu ambayo yanamuathiri hadi leo, kwani aliyasimulia kwa machozi.

"Nilianza kujikata kata kwenye mikono na miguu, kwa sababu nilikuwa natafuta njia yoyote ya kusaidiwa, nilifikiria wazazi wakiona wataniuliza eeh Claudia nini inaendelea?.. ama walimu ama mtu yeyote tu. Lakini walimu wangu walipoona, wakasema kwamba mimi nimeingia kwenye ushirikina na mambo ya kishetani. Watu ambao nilifikiria watanielewa, wao ndio hawakunielewa kabisa".

Kujaribu kujitoa uhai

"Nilijaribu kujitoa uhai kwa kuweka jiko katika chumba changu na kufunga mlango na madirisha, lakini sikufa, nikajua Mungu ameniokoa.

"Nilijua kwamba mungu amenipatia nafasi nyingine na kuwa kama Mungu ananipenda si lazima nipendwe na mtu kwa kuwa yeye ndiye aliyenipatia maisha haya, ni yeye ndiye aliniweka huku duniani."

Aliponusurika baada ya kujaribu kujitoa uhai, mwanafunzi huyu wa chuo kikuu cha JKUAT akaamua kujikubali na kujitahidi kuafikia ndoto yake ya kuwa mwanamtindo.

"Nikaanza uwanamitindo, ili niwasaidie wasichana wengine ambao pengine wanazuiwa kushiriki katika uwanamitindo kwa sababu ni wanene ama ni wafupi, atakaponiona kisha asome historia yangu atajua kwamba kuna matumaini kwa kuwa nimeafikia ndoto yangu licha ya yale nimepitia."

Amejaribu kwenda katika mashindano ya uwanamitindo lakini kila wakati mawakala humbagua.

"Kuna wakati ambapo nilienda kujisajili katika mashindano ya uanamitindo lakini wakala huyo akanizuia mlangoni na kuniambia "ni ya wanamitindo pekee walioruhusiwa kuingia," anasema.

Alijua ni kwasababu ya makovu yake.

Licha ya kukataliwa na mawakala, Claudia ambaye pia anajitambulisha kama 'Vanilla Afrika' kwa jina lake la kisanii, hakukata tamaa na kwa usaidizi wa wanafunzi wenzake, yeye hupigwa picha katika mazingira tofauti na kuziweka katika mtandao wa Instagram.

Claudia Wanjiru

Chanzo cha picha, VIN ARTS

Makovu yao pia yamemkosesha mchumba, kwa sababu hajui malengo yao huwa gani.

"Mvulana ambaye nilikuwa namchumbia, kila wakati tukikosana, ananikumbusha juu ya alama zangu usoni ananiambia anavumilia kuwa na mimi kwa sababu hakuna mtu mwingine anayeweza kunipenda na alama hizo."

Hata hivyo msichana huyu anaelezea urembo kulingana na anavyotambua.

"Urembo ni tabia, ni kumsaidia mtu, kumheshimu mtu, urembo ni utu... Hii ndiyo maana ya urembo, kwasababu mtu anaweza kuwa na sura ya kupendeza, lakini hana tabia za kupendeza.

"Kama mimi mwenyewe niko na hizi alama, najiambia kwamba mimi ni mrembo, kwasababu si alama zinanipatia jina, alama ni ngozi tu, kila mtu anayo."