Priyanka Chopra: Mwigizaji nyota wa Bollywood afichua shela yake ya futi 75

Muda wa kusoma: Dakika 3

Kwanza Priyanka Chopra, mwigizaji nyota wa Bollywood na mwanamitindo pia, aligonga vichwa vya habari kwa kufunga ndoa wikendi na mwanamuziki Mmarekani, lakini sasa tena anatikisa mawimbi.

Kisha ni kitambaa cha shela ya gauni alilolivalia wakati wa harusi yao.

Amefichua maelezo kuhusu vazi hilo mwenye mtandao wa Instagram leo hii.

Gauni lake, ambalo ni matokeo ya ubunifu wa kampuni ya Ralph Lauren, lilikuwa na puleki za lulumizi milioni mbili, zikiwa zimeshonelewa kwa ustadi mkubwa.

Lakini shela nalo limewaacha watu vinywa wazi! Lilikuwa na urefu wa futi 75. Hizo ni sawa na mita 23. Shela hiyo ilikuwa nyeupe na laini na yenye kupitisha nuru na kumuwezesha anayetazama kuona kilichomo.

Jonas na Chopra ambao wameachana kwa umri kwa mwongo mmoja walichumbiana majira ya joto, baada ya kipindi cha mapenzi tele.

Walifunga ndoa wikendi katika jimbo la Rajasthan.

Shela hiyo ilikuwa ndefu sana kiasi kwamba ilihitaji kundi la watu kuibeba. Mtandaoni watu hawakuishiwa na maneno.

Baadhi waliifananisha na vitu vingine.

Wengine nao wakadokeza kwamba ilizidi sana shela ya Meghan Markle, mke wa mwanafalme wa Sussex Harry, ambaye alifunga ndoa miezi kadha iliyopita.

Kitambaa cha shela ya Markle kilikuwa na urefu wa futi 16.

Chopra alivalia vazi hilo la Ralph Lauren katika sherehe iliyoandaliwa katika bustani ya kasri la Umaid Bhawan katika jiji la Jodphur Jumamosi.

Sherehe hiyo iliongozwa na babake Jonas, Paul Kevin Jonas, ambaye ni mhubiri.

Sherehe ya harusi yao ambayo ilikuwa ya siku tatu, pia ilijumuisha sherehe ya Kihindi Jumapili ambapo wawili hao walikula kiapo cha uaminifu katika ndoa tena..

Akizungumza na mwandishi wa jarida la People, Chopra alisema kwamba anafurahia kwamba utamaduni ulibadilishwa kuwafaa.

Jonas, 26, na Chopra, 36, walichumbiana majira ya joto, si muda mrefu baada ya taarifa za mapenzi yao kuanza kuwa hadharani.

Baadaye walisema kwenye mahojiano kwamba walianza kuwasiliana kwa ujumbe mfupi Septemba 2016.

Walionekana pamoja hadharani katika hafla ya kutoa tuzo za sanaa ya Met Gala Mei 2017 na wote walikuwa wamevalia mavazi ya Ralph Lauren, na uhusiano wao ukaanza kugonga vichwa vya habari mwaka mmoja baadaye.

Chopra ni miongoni mwa wasanii wa Bollywood wanaolipwa pesa nyingi zaidi, na alishinda Miss World mwaka 2000.

Kufikia sasa, ameigiza katika zaidi ya filamu 50 za India.

Alianza kuigiza Marekani katika msururu wa filamu za Quantico na pia katika filamu za Ventilator, Baywatch na A Kid like Jake.