Mama bandia wa taifa akamatwa Nigeria baada ya madai ya rais bandia kuibuka

Chanzo cha picha, Punch
Mwanamke aliyetumia uongo kuingia makao ya rais wa Nigeria na kudaiwa kutelekeleza ulaghai wa kibiashara amekamatwa.
Kikosi cha kumlinda rais kilisema Amina Mohammed alidanganya kuwa yeye ni mke wa gavana wa jimbo la Kogi ili apate kuruhusiwa kuingia makao ya rais kwenye mji wa Abuja.
Kisha anadaiwa kuwaalika watu kuingia makao hayo na kuwafanya waamini kuwa walikuwa wamealikwa na mke wa rais.
Peter Afunanya, msemaji wa shirika la ujasusi nchini Nigeria linalofahamika kama Department of State Security (DSS) aliwaambia wandishi wa habari kuwa sakata hiyo ilitokea wakati mke wa rais Aisha Buhari alikuwa nje ya nchi Novemba mwaka 2017.
Mfanyabiashara tajiri Alexander Chika Okafor, ambaye alialikwa kwenda makao hayo na Bi Mohammed, alimlaumu kwa kumlaghai dola 414,000 akidanga kuhusu mali fulani mjini Lagos.
"Uchunguzi umeonyesha kuwa mke wa rais hakufahamu njama hiyo ya ulaghai," Bw Afunanya alisema.
Bi Muhammed alitumia fursa kuwa watu kama wake wa magavana, na maafisa wa vyeo fulani hawapitii ukaguzi kwenye milango ya makao hayo," aliongeza

Chanzo cha picha, AFP
Mwandishi wa BBC mjini Abuja anasema kisa hicho kilichotokea katika makao ya rais ambayo pia yanajulikana kama Aso Rock ni cha kushangaza kwa kuwa yanalindwa na kikosi cha DSS na pia polisi.
Wale wote wanaofanya kazi humo wana vitambulisho vikiwemo vya elektroniki na wageni wote huandikishwa kabla ya kuingia.
Mwezi Septemba DSS ilimkamata mmoja wa wasaidizi wa mke wa rais kwa madai kuwa alichangisha fedha kwa njia ya ulaghai.
Rais Muhammadu Buhari ambaye anataka kuchaguliwa tena mwezi Februari aliiangia madarakani akiahidi kuwa angepambana na janga kubwa la ufisadi lilaloikumba Nigeria.
Uvumi wa kifo cha Buhari
Wakati huo huo Rais Muhammadu Buhari amekana uvumi kuwa alikuwa amekufa na nafasi yake kuchulikuwa na mtu anayemfanana
Baadhi ya watu wanadhani kuwa alibadilishwa, "lakini huyu ni mimi," Buhari alisema.
Uvumi kuwa mwili wake ulikuwa ni wa mtu mwingine kwa jina "Jibril" kutoka Sudan ulisambaa sana kwenye mitandao.
Buhari 75, ambaye anataka kuchaguliwa tena Februari mwaka ujao amekuwa mwenye afya mbaya tangu aingie ofisini mwaka 2005.
Alichukua likizo ya miezi mitatu kupata matibabu nchini Uingereza mwaka 2017.
Alifichua baada ya kurudi nchini Nigeria kuwa hakuwai kuwa mgonjwa kiasi hicho lakini hakufichua alikuwa anaugua nini. Anasisitiza kuwa sasa ana afya nzuri.












