Kwa nini mikate imekuwa chanzo cha migogoro

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC Swahili, Tanzania
Nchini Sudan kumeshuhudiwa maandamano ya wanaopinga kuongezeka kwa bei ya mkate. Maandamano hayo yamefika mpaka magharibi mwa jimbo la magharibi mwa Darfur ambapo mmoja wa waandamanaji ambaye ni mwanafunzi.
Aliuawa baada ya makabiliano baina ya polisi waliokuwa wakitumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakitumia mawe, kuchoma matairi na kufunga barabara.
Sokomoko hii imekuja baada ya serikali kuondoa punguzo la bei hivyo kusababisha ongezeko la bidhaa za vitu ikiwemo mkate.
Pengine wengi hapa wanaweza kushangaa na kujiuliza kwamba inakuaje watu wanaingia barabarani na kufanya maandamano, kisa tu kupanda kwa bei ya mkate?
Kwa baadhi yetu tulioko katika nchi za Afrika, hasa Afrika Mashariki, mara nyingi, tumezoea kupima ugumu wa maisha kwa kupanda pengine kwa bei ya mafuta ya petroli au dizeli.
Hivyo, kupanda kwa bei ya mkate, kwa kiasi fulani kunaweza kusitushughulishe kabisa. Lakini kwa nchi za kiarabu, hali ni tofauti kabisa.
Waarabu, chakula chao kikuuni mkate. Mkate unaweza kuliwa mtupu kama mkate, au unaweza kuwa ni sehemu ya chakula, pengine na mchuzi wa nyama au hata mbogamboga.
Muhimu ni kwamba, mkate ni chakula kinachoshika nafasi ya kwanza katika maisha ya Waarabu, na mkate unagusa watu wa matabaka mbalimbali, haijalishi ni tajiri au maskini.
Kwa maana hiyo, kipimo na maisha kuwa magumu au mepesi, kwa wenzetu ni kupitia mkate na jinsi gani chakula hicho kinapatikana.
Mathalan, katika nchi za Kiarabu ambazo niliwahi kuishi kwa muda mrefu zaidi ni Libya.
Kama ilivyo kwa nchi nyingine za Kiarabu, kwa Walibya, mkate nao ulikuwa na thamani ileile. Ilikuwa ni jambo la kawaida kupita katika barabara kuu za mjini Tripoli, kama vile Awwal Septemba, na kuona vipande vya mkate vimetundikwa au vimewekwa katika madirisha ya nyumba.
Mfano wa barabara ya Awwal Septemba ni kama vile Samora Avenue ya Dar es Salam, au Oxford Circus ya London. Yaani, ni barabara iliyokuwa na maduka yenye vitu vya thamani na bei ghali, lakini pia ilikuwa ni barabara rasmi ambayo wageni na viongozi mbalimbali walikuwa wakipitishwa, akiwemo mwenyewe aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo wakati huo, Kanali Muammar Gaddafi.

Chanzo cha picha, AFP/Getty
Nimetoa mfano wa barabara hiyo, kwa sababu ya umuhimu wake, basi bila shaka, mimi na wewe tusingetaraji katu kuona vipande vya mkate barabarani kwa jinsi mitaa hiyo inavyotakiwa kuwa nadhifu.
Hiyo ilikuwa ni sura ya kawaida katika mazingira ya Libya, kuona vipande vya mkate vimewekwa madirishani.
Kwangu mimi ambaye nilikuwa mgeni na utamaduni ule, nilipata kumuuliza mmoja wa wenyeji wangu na mfanyakazi mwenzangu, Sami Mohammed. "Ya muhandis," nilianza kumuita na baadaye kumuuliza kwa nini hali iko hivyo. Yeye ni mhandisi aliyebobea katika mambo ya kompyuta, hivyo sote tulizoea kumwita kwa wadhifa wake.
Sami, alianza kwa kunielezea umuhimu wa mkate katika maisha yao Walibya, na kuongeza kwamba, kwa umuhimu huo, wao walibya, wanauheshimu sana mkate, kiasi kwamba, mtu hawezi kutupa mkate ovyo ovyo.
Ikitokea kwamba, mtu ameona kipande cha mkate barabarani, popote pale alipo, hata kama yuko kwenye gari, basi sharti ashuke akiokote na kukihifadhi kwa kukiweka juu ya dirisha.
Sami aliendelea na kunitolea mfano kwamba, sio wao pekee yao, bali hata Gaddafi mwenyewe angefanya hivyo hivyo.
Bila shaka, ingawa hapa niliona kama ametia chumvi, lakini nikajua alikuwa na maana ya kunionyesha ni jinsi gani mkate ulivyo na thamani kwao.
Nikiwa bado nimestaajabishwa na jinsi Walibya wanavyothamini chakula hicho, katika uchunguzi wangu pia nilikuja kubaini kuwa, mkate nchini humo, ndio chakula pekee cha bei rahisi kabisa kulivyo vyote.
Robo dinari kipindi kile, nazungumzia mwaka 2005, ndio ilikuwa fedha ndogo kabisa nchini humo. Lakini ukitaka kujua thamani ya fedha hiyo, ingia sehemu inayouzwa mikate, maarufu 'kushaa' au kwa maana nyingine tuliyoizoea, 'bakery'.
Basi utatoka na fuko la mikate, kwani dinari moja ni sawa na mikati kumi ile midogo midogo ya duara.
Kwangu mimi ambaye nilikuwa na familia ndogo kipindi kile, nilikuwa siihitaji mikate kumi, kwa sababu ningeichukua yote, basi ni chakula cha takriban siku tatu au nne, na mikate inavyozidi kukaa ladha inapotea.
Maisha yalikuwa mepesi kwa sababu upatikanaji wa mikate na bei yake ilikuwa rahisi, hivyo kufanya maisha ya Walibya kuwa mazuri yenye mlo wa uhakika.
Kuhusu hilo la maisha kuwa mepesi, nakumbuka siku nyengine tofauti, katika mazungumzo na kijana wa ki-Libya, Miftah Bilheed.
Tulikuwa katika mazungumzo ya kawaida tu, hata sijui ilikuaje, mara tukajikuta tunazungumzia maisha.
Miftah alinipa takwimu zisizo rasmi na sijui alizipata wapi, lakini alinihakikishia huku akipiga kifua konde, kuonyesha uhakika wa maneno yake, kuwa sio rahisi Libya ya wakati huo, mtu kulala bila kula.
"Keif yaani," nikashangazwa na habari hiyo na kumuuliza, inakuaje Miftah? Akanijibu huku akitabasamu, "Ukiwa na njaa na huna fedha za kununua chakula, nenda 'bakery' yoyote au hoteli yoyote, omba chakula, utapewa chakula."

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Nilipigwa na butwaa, nikabakia mdomo wazi. Wakati ule, nikiwa maelfu ya maili kutoka nyumbani, nikakumbuka pia ukarimu uliokuwepo katika baadhi ya maeneo ya nchi za Afrika Mashariki, hasa maeneo ya mwambao wa pwani. Nikakumbuka jinsi zamani watu waliweka futari nje katika mwezi wa Ramadhani ili kutoa fursa kwa wageni na wapita njia nao kutabaruku. Ingawa utamaduni huu hivi sasa umepotea.
Lakini migogoro inayosababishwa na ukosefu au kupanda kwa bei ya mikate haijaanza leo wala jana.
Mambo haya yana historia ndefu katika maisha ya binadamu.
Kana kwamba historia wakati mwengine inajirudia. Wengi wanamfahamu Marie Antoinette, aliyekuwa malkia wa mwisho wa Ufaransa kabla ya Mapunduzi ya nchi hiyo.
Katika moja ya nukuu zake maarufu bibie huyu, ni pale alipoambiwa kuwa wananchi wake hawana mikate ya kula. Naye, kwa wepesi kabisa, akajibu, "waambie wale keki kama hawana mikate."
Utawala wake na mumewe haukudumu.












