Upi mustakabali wa mahusiano ya Tanzania na EU?

Chanzo cha picha, IKULU TZ
Kwa miaka kadhaa, Tanzania imekuwa ikionekana ndio taifa pendwa na jamii ya kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Tanzania, ukilinganisha na majirani zake, kwa miongo kadhaa imekuwa nchi ya amani na utulivu. Ukuaji wake wa demokrasia na siasa umekuwa wa kupigiwa mfano. Kutokana na hayo hata ukuaji wake wa uchumi pia umekuwa ukisifiwa.
Kutokana na hali hiyo, nchi ya Tanzania ikajikuta inaunda ushirika mkubwa na mataifa ya Magharibi, na baadhi ya vyombo vya habari vya mataifa jirani yake ikaiita kwa kingereza 'darling of the West' ikimaanisha kipenzi cha mataifa ya magharibi.
Kutokana na uhusiano huo, Tanzania imekuwa ikifaidika kwa misaada ya kifedha na mikopo ya kimaendeleo ambayo imekuwa ikisukuma pakubwa miradi ya ujenzi wa miundominu, afya na elimu pamoja na sekta nyengine.
Kwa hali inavyoendelea hivi sasa, ni dhahiri kuwa uhusiano wa pande hizo mbili unapitia katika wakati mgumu.
Jana Alhamisi, Jumuiya ya Ulaya (EU) ilitoa tamko ambalo limetamka dhahiri kuwa mahusiano baina ya Umoja huo na Tanzania si mazuri.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mwakilishi Mkuu wa EU Federica Mogherini imeeleza kuwa katika miaka ya hivi karibuni EU na nchi wanachama wake wamekuwa wakishuhudia kuminywa kwa uhuru wa kijamii nchini Tanzania kwa kuwekwa vikwazo katika shughuli za taasisi zisizo za kiserikali, vyombo vya habari na vyama vya siasa.
EU inasema haki za binaadamu na utawala wa sheria umekuwa ukikandamizwa mara kwa mara. EU pia inasikitishwa juu ya kuzorota kwa haki za wapenzi wa jinsia moja.

Chanzo cha picha, AFP
"Katika muktadha huu, mamlaka za Tanzania zimekuwa zikimpa shinikizo la mara kwa mara balozi wa EU. Hali hiyo imemlazimisha balozi kuondoka na kuitwa kwa majadilino. Hali hii haiendani na tamaduni ya majadiliano baina ya pande hizi mbili na EU inasikitishwa sana juu ya hilo. EU inazitaka mamlaka za Tanzania kujiepusha kutoa mashinikizo na vikwazo kwa wanadiplomasia."
Balozi wa EU nchini Tanzania Roeland van de Geer, yupo Brussles,Ubelgiji toka wiki iliyopita kwa majadiliano na wakuu wake.
Taarifa hiyo pia imesema EU pamoja na nchi wananchama wake wamekubaliana kufanya tathmini ya kina juu uhusiano wake na nchi hiyo.
"Tutaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo kutoka sekta za jamii, siasa uchumi na asasi za kiraia. Pia tutahuisha majadiliano yetu na serikali ya Tanzania tukitarajia kuendelea kushirikiana kwa manufaa na kuaminiana."

Tayari nchi ya Denmark ambayo ni mwanachama wa EU imechukua hatua kali kuzui msaada wa kifedha kwa Tanzania.
Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa nchi hiyo Ulla Tornaes ametangaza kusitishwa kutolewa kwa krone milioni 65 ($9.8 milioni) ambazo zilikuwa ni msaada kwa Tanzania baada ya kutolewa "kauli zisizokubalika dhidi ya wapenzi wa jinsia moja" kutoka kwa mwanasiasa mwandamizi.
Mwezi uliopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitangaza operesheni dhidi ya wapenzi wa jinsia moja kwa kutaka watu wawaripoti polisi watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Makonda pia alitangaza kamati maalum ambayo pamoja na shughuli nyengine ingeliangazia suala hilo la wapenzi wa jinsia moja.
Serikali hata hivyo ilijitenga na kauli hiyo ya Makonda kwa kudai alikuwa akitoa mtazamo wake na si sera rasmi ya nchi.












