Wavulana kumi wamekufa katika ajali ya moto nchini Uganda

moto katika bweni la wavulana nchini Uganda
Maelezo ya picha, Moto huo umetokea katika eneo la wilaya ya Rakai

Shambulizi La uchomaji moto bweni la wavulana Kusini mwa Uganda limesababisha wavula 10 kufa na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya.

Taarifa zinaeleza kuwa moto huo ulianza asubuhi ya jana katika jingo moja linalohifadhi wanafunzi wengi katika shule ya sekondari ya St Bernard iliyoko mjini Rakai.

Maafisa wa polisi wamearifu kuwa milango ya bweni hilo ilikuwa imefungwa na kufuli, na hivyo kukwamisha wanafunzi wengi zaidi wakiwa ndani.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Henry Nsubuga, amelielezea tukio hilo la moto kuwa ulikuwa mkali sana na mtekelezaji alitumia nguvu kubwa.

Ben Nuwamanya, mkuu wa kituo cha polisi cha karibu, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu watatu wamekamatwa kwa kuhusika na tukio hilo , akiwemo mlinzi wa shule hiyo, wote waliokamatwa wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi na kuisaidia polisi.

Amethibitisha kuwa wanafunzi wengine ishirini wako hospitalini wakiendelea na matibabu kutokana na hali zao kuwa mbaya, huku akionya kuwa huenda idadi ya vifo ikaongezeka.

Msemaji wa polisi nchini humo Patrick Onyango ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba mamlaka nchini humo zinachunguza ajali hiyo endapo wanafunzi wa zamani wanahusika na uchomaji huo wa shule.

Naye kiongozi wa serikali ya mtaa, Gerald Karasira, amesema kwamba watu wanaoishi karibu na shule hiyo walijaribu kuuzima moto huo kwa kutumia mchanga ,maji na hata kuondoa baadhi ya matofari ya bweni hilo ili kuwanusuru wavulana hao ingawa zoezi hilo halikuwa rahisi kutokana na milango ya bweni hilo kufungwa na pia kukabiliwa na changamoto ya moshi mzito kwenye eneo la tukio.

Endapo tungekuwa na kikosi cha zima moto katika wilaya yetu, pengine tungeweza kuokoa maisha ya watoto hao na mali pia, alinukuliwa mwenyekiti huyo wa serikali ya mtaa wakati akizungumza na waandishi habari.

Wilaya ya Rakai ambapo shule hiyo ipo, iko karibu kilomita 280 (sawa na maili 170) kusini mwa mji mkuu wa Uganda ,Kampala na pia ni karibu na mpaka wa Tanzania na Uganda.

Idadi ya viongozi wakuu serikalini, wakiwemo waziri wa elimu, waziri wa ulinzi walisafiri hadi katika shule hiyo ili kujionea uharibifu uliofanywa na moto huo.