Ingomanshya: Wapiga ngoma wanawake Rwanda waliothubutu kukaidi utamaduni

Wanawake katika mkoa wa kusini mwa Rwanda wamejiweka pamoja na kuanzisha kundi la kupiga ngoma za kitamaduni.
Kundi hilo limekuwa kivutio kikubwa kwa kutumbuiza katika tamasha mbali mbali nchini humo na hata barani ulaya na Marekani.
Hii ni licha ya kwamba katika utamaduni wa wanyarwanda ilikuwa mwiko kwa wanawake kupiga ngoma za kiasili.
Ngoma hizo zinasakatwa na akina mama kutoka kundi lijulikanalo kama ''Ingomanshya'' katika mji wa Huye kusini mwa Rwanda
''Ingomanshya'' lilianzaje?
Mpigaji ngoma Regina Nyiranshimiyimana, anasema ni kundi ambalo linajumuisha wanawake zaidi ya 20.
Lilianzishwa kama mashirika mengine lakini wao wakijihusisha na kazi ya kutumbuiza katika tamasha mbali mbali na kuingiza pesa.
"Mwaka 2008 ndio mwaka niliotoka nje nikaenda kupiga ngoma Senegali, nilifurahi sana nikasema kumbe nisikatike nguvu, hii kazi itanifikisha mbali.

Nikaendelea kupiga ngoma nyuma ya huo mwaka nikaenda nchi mbali mbali, nilienda Uingereza, Ufaransa, Amerika hivi karibuni, hadi Sweeden nimeenda kutokana na hii kazi ya kupiga ngoma. Ninapata pesa za kusaidia familia yangu," Regina ameiambia BBC.
Kawaida katika tamasha za kitamaduni nchini Rwanda mlio wa ngoma ndo unaokamilisha sherehe, na ngoma hupigwa bila kuchanganywa na nyimbo yoyote, lakini pia kunakuwepo na tamasha la ngoma peke yake na kuwa na utamu wa aina yake.
"Kwanza mimi nikiwa napiga ngoma lazima niwe na furaha tena nisikie jinsi ile ngoma inaingia kwenye roho mpaka inaingia kwenye damu yani unajiachilia.
Sasa mimi nikisha furahi na yule anaye nitazama anasikia mdundo ule wa ngoma na yeye sasa anaanza kusikia kwa roho mpaka kwa damu," Regina anasema.

Tangu zamani ilikuwa mwiko kwa mwanamke nchini Rwanda kupiga ngoma lakini kundi la akina mama la Ingomanshya, wanasema lazima wanawake wafuate maendeleo.
"Kutokana na raisi wetu ametambua uhuru kwa wanawake na si tukasema acha tupige ngoma.
Ndio wengi wanasema ni kunyume, huwezi kuona mwanamke anapangilia nyumba anatembeza gari au anaingia jeshini haiwezekani ni maendeleo. Na hii kupiga ngoma si ni tamaduni tu? Hapana sikuhizi ngoma ni kazi," anasema bi Regina.












