Mo Dewji: IGP Sirro aapa kuwanasa waliomteka Mo wakiwa hai au wamekufa

IGP Simon Sirro

Polisi nchini Tanzania wamesema watafanya kila wawezalo kuwatia nguvuni watu waliomteka na kumshikilia bilionea Mohammed Deji, Mo, kwa siku tisa.

Mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro amewaambia waandishi wa habari hii leo Oktoba 20 kuwa kuachiwa kwa Mo ni mwanzo wa kuwanasa wahalifu hao na kjuahidi kuwapata wakiwa wazima au wamekufa.

"Mbio ukizianza sharti uzimalize. Huu ni mwanzo tu. Hao wahalifu wanaotaka kuchafua jina la nchi yetu lazima tuwatie nguvuni."

Sirro amesema upelelezi umeimarishwa kwa kushirikiana na mtandao wa polisi wa kimataifa Interpol.

"Nataka niwaambie (wahalifu) yawezekana wananisikiliza hivi sasa kuwa, popote watakapoenda tutawanasa. Wakienda Afrika Kusini tunao, Kenya tunao, Uganda tunao hata Msumbiji, popote pale tutawakamata maana tayari tunaushirikiano na wenzetu."

IGP Sirro amesema taarifa za kiupelelezi alizozitoa jana juu ya gari lilotumika kumteka Mo Dewji Alhamisi ya wiki iliyopita na dereva aliyekuwa analiendesha lilipoingia Tanzania limesukuma watekaji hao kuogopa na kumwachia huru Mo.

"Tayari tunamjua dereva, tunamjua mmiliki wa gari...tumeweka wazi picha za gari. Wkaona hawana namna zaidi ya kumwachia tu. Lakini kama nilivyosema nitawapata na kuwagonga na sheria wakiwa wazima au wametangulia mbele ya haki (wamekufa)."

Kuchoma gari moto

Gari lilochomwa

Jana kamanda Sirro alionesha picha za gari aina ya Toyota Surf akisema wanaamini ndilo lilitumika kumteka Mo kutokana na picha za CCTV.

Gari hilo lilikuwa na namba za usajili za AGX 404 MC, BBC ilifanya uchunguzi na kugundua ni nambari za usajili za nchi ya Msumbiji iliyopo kusini mwa Tanzania.

Kwamujibu wa polisi gari hilo tena hii leo lilitumika kumtoa Mo kwenye eneo ambalo alikuwa anashikiliwa mpaka eneo la Gymkhana ambapo walimtelekeza mishale ya saa nane usiku. Mo inadaiwa alitumia simu ya moja ya walinzi katika eneo la karibu kumpigia simu baba yake na kufuatwa kisha kutoa taarifa polisi.

Mo Dewji quote

Sirro amesema mara baada ya kumuachia, wahalifu hao walijaribu kuharibu ushahidi kwa kulichoma gari hilo lakini ilishindikana.

"Mkienda pale eneo la tukio mtaliona hilo gari, kuna madumu ya mafuta, walijaribu kuliwasha moto lakini ikashindikana."

Polisi wanaarifu kuwa walikuta ndani ya gari hilo bunduki moja na bastola tatu zilizokuwa na jumla ya risasi 32.

Watekaji walitaka pesa

Mo Dewji

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Sirro pia amewaambia waandishi wa habari kuwa waliomteka Mo Dewji walifanya hivyo kwa lengo la kujipatia pesa.

Sirro amesema bilionea Mo aliwapa nambari ya simu ya baba yake mzazi mzee Gulam ili waongee nae juu ya hilo lakini hawakupiga simu wakihofia kunaswa na polisi.

"Mohammed Dewji amesema watekaji hao walikuwa na wasiwasi sana..." amesema Sirro na kuongeza, "...walimwambia wanataka pesa, alipowauliza shilingi ngap ihawakusema. Aliwapa nambari ya simu ili waongee na baba yake lakini waliogopa kwa sababu wanafahamu ulinzi wetu ni imara na tungewakamata."

Kamanda Sirro amesema watu hao waliokuwa wakimshikilia Mo walikuwa watatu, wawili walikuwa wakiongea Kingereza na mmoja akiongea Kiswahili kidogo.

Mkuu wa polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa awali alisema Mo alibainisha kuwa lafudhi za watu waliokuwa wakimshikilia ni kama za watu wa mataifa ya kusini mwa Afrika.