Mo Dewji: Bilionea wa umri mdogo aliyetekwa kwa siku tisa arejea nyumbani salama Tanzania

Mfanyibiashara Mo Dewji

Chanzo cha picha, Getty Images

Mo Dewji, bilionea Mtanzania aliyetekwa na watu wasiojulikana Alhamisi wiki iliyopita, amerejea nyumbani salama.

Katika ujumbe ulioandikwa kwenye ukurasa wa Twitter wa kampuni yake, amesema: "Namshukuru Mwenyezi Mungu nimerudi salama nyumbani. Nawashukuru Watanzania wenzangu na watu wote kote duniani kwa dua na sala zao. Nashukuru mamlaka zote, ikiwemo Jeshi la Polisi, zilizofanya kazi ya kuhakikisha narudi salama."

Ujumbe huo umeandikwa saa tisa na robo alfajiri, na umeelekezwa kwamba umeandikwa kutoka Dar es Salaam.

Maelezo ya video, Mo Dewji aliporudi nyumbani

Waziri wa Muungano na Mazingira Tanzania Januari Makamba naye ameandika kwenye Twitter kwamba: "Mohammed Dewji amerudi salama. Nimezungumza naye kwa simu dakika 20 zilizopita. Sauti yake inaonyesha yu mzima bukheri wa afya. Shukrani kwa wote kwa dua na sala. Naenda nyumbani kwake kumuona muda huu."

Afisa mkuu wa polisi wa kanda ya Dar es salaam Lazaro Mombasasa

Kulingana na afisa mkuu wa polisi wa kanda ya Dar es salaam Lazaro Mombasasa aliyetembelea nyumbani kwao Dewji kuthibitisha kurejea kwake nyumbani, amesema watu waliomkamata walikuwa na lafudhi ya mojawapo ya lugha za mataifa ya Afrika Kusini. Aliongezea kwamba hatua hiyo imethibitisha wazi kwamba waliomteka sio Watanzania.

''Nataka kuuthibitishia umma wa Tanzania kwamba nimefika nyumbani kwa akina Mo Dewji nimeongea naye niko na kikosi cha makachero hapa na ndugu yetu ni mzima kama IGP alivyozungumza na umma kwamba jeshi la polisi litaendelea na uchunguzi ili kuhakikisha kwamba tunampata muhusika akiwa mzima.

Mo Dewji

Mo Dewji ambaye alionekana mchovu alimshukuru mwenyezi mungu na serikali ya rais Pombe Magufuli pamoja na Watanzania kwa kumuombea.

''Namshkuru mwenyezi mungu , serikali ya Magufuli na IGP , ahsanteni mimi ni mzima nawashukuru Watanzania wote kwa kuniombea.

Babake Mo alivimbia vyombo vya habari kwamba mwendo wa saa nane alifajiri walipokea simu ya Mo kwamba yuko salama na moja kwa moja wakaelekea katika eneo la Gymkhana ambako alikuwa amewachwa na watekaji wake.

''Tumshukuru mwenyezi Mungu kwamba tumempata salama na anaendelea vizuri. Walikuwa wamemuacha pale na kuondoka. Lakini alikuwa hajafungwa na yuko sawasawa. Tunawashukuru Watanzania wote na rais''.

Wakati huohuo Gari ambalo linaaminika kutumika katika kumteka bilionea Mohammed Dewji, Mo limepatikana kando ya viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam ambapo bilionea huyo aliachiwa huru.

Jana, Mkuu wa polisi Tanzania IGP Simon Sirro alisema gari hilo, Toyota Surf, liliingia Tanzania likitokea nchi jirani mnamo Septemba mosi 2018.

Sirro hakusema gari hilo lilitokea nchi gani, lakini kutokanana na namba zake za usajili AGX 404 MC, BBC ilifanya uchunguzi na kugundua ni nambari za usajili za nchi ya Msumbiji iliyopo kusini mwa Tanzania.

Hata hivyo, gari hilo hii leo limeonekana likiwa na namba za usajili wa Tanzania T 314 AXX. Bado haijafahamika namba hizo za usajili wa Tanzania ni feki ama la.

Hakuna mtu aliyekamatwa, na bado haijulikani watu waliomtelekza Mo eneo hilo walitumia usafiri gani kutoroka.

Mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania Simon Sirro

IGP Simon Sirro amewaambia waandishi wa habari kuwa waliomteka Mo Dewji walifanya hivyo kwa lengo la kujipatia pesa.

Sirro amesema bilionea Mo aliwapa nambari ya simu ya baba yake mzazi mzee Gulam ili waongee nae juu ya hilo lakini hawakupiga simu wakihofia kunaswa na polisi.

"Mohammed Dewji amesema watekaji hao walikuwa na wasiwasi sana..." amesema Sirro na kuongeza, "...walimwambia wanataka pesa, alipowauliza shilingi ngapihawakusema. Aliwapa nambari ya simu ili waongee na baba yake lakini waliogopa kwa sababu wanafahamu ulinzi wetu ni imara na tungewakamata."

Kamanda Sirro amesema watu hao waliokuwa wakimshikilia Mo walikuwa watatu, wawili walikuwa wakiongea Kingereza na mmoja akiongea Kiswahili kidogo.

Mkuu wa polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa awali alisema Mo alibainisha kuwa lafudhi za watu waliokuwa wakimshikilia ni kama za watu wa mataifa ya kusini mwa Afrika.