Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Elimu: Kasoro zagunduliwa kwenye vitabu vya shule Kenya, wa kulaumiwa nani?
Utaratibu wa mitaala mipya ya elimu barani Afrika hata duniani kote ni jambo la lazima kuwepo kutokana na mabadiliko ya yanajitokeza kila siku.
Wataalamu wa elimu wanasema kwamba umuhimu mkubwa wa kuithinisha kwa mitaala mipya kwa sababu tekinolojia imebadilika sana, uwezo wa watoto pia umebadilika na hata utendaji wa kazi au ajira zimebadilika hivyo hata elimu yetu inapaswa kubadilika.
Dkt John Mugo Mkurugenzi wa asasi ya Uwezo ambayo inaangazia masuala ya elimu ya watoto kuanzia umri wa miaka 6 mpaka 16 katika maeneo ya Afrika mashariki anasema kuwa kuna ulazima kwa kila taifa kukaa chini na kuja na mikakati ya namna ambavyo wanaweza kutekeleza mabadiliko haya katika ubora unaohitajika.
Pamoja na kuwa utekelezaji wa mabadiliko ya mitaala unatendeka lakini ukosoaji kutoka kwa jamii husika bado ni changamoto.
Wakenya kukosoa mtaala mpya wa elimu
Mbadiliko ambayo yamefanywa katika vitabu vya shule ya msingi nchini Kenya yamekosolewa vikali na umma kwa kudaiwa kuwa baadhi ya maudhuhi hayafai kwa watoto, afisa elimu aliiambia BBC.
Kitabu kimoja kilionekana kusifia maisha ya starehe ya mwanasiasa wa uongo ambaye alikuwa na helikopta yake mwenyewe,meli pamoja na magari.
Kitabu kingine ambacho ni cha Kiingereza kinaonyesha wanawake waliobeba mizigo mizito sokoni wakati wanaume wanakunywa bia na nyama choma.
Hata hivyo mkurugenzi wa idara ya maendeleo ya mitaala nchini Kenya Julius Jwan amedai kuvihakiki tena vitabu vyote vipya ili vile ambavyo havijakidhi vigezo kuondolewa.
Uamuzi ambao umekuja mara baada ya waziri wa elimu wa nchini Kenya Bi. Amina Mohamed kusisitiza suala la ubora wa vitabu kupewa kipaumbele.
Aidha jambo ambalo Dkt Mugo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya elimu nchini Kenya anaona kuwa limekosewa na inaonekana wazi kuwa waandishi ndio changamoto.
Vitabu vinachapishwa kwa haraka na hata vyuo ambavyo vimewekwa na serikali vinapaswa kuwa na wakaguzi wa serikali ambao wanahakiki kazi hizo kwa umakini.
Mitihani imebadilika na mafunzo ya walimu inapaswa kubadilika na walimu wanapaswa kujengewa uwezo wa kumfundisha vizuri mtoto.
Dkt Mugo alisisitiza kuwa ni jukumu la serikali kuwekeza zaidi na mafunzo ya madili yanapaswa kutolewa.
"Kosa limetendeka kweli lakini ni namna gani tunaweza kuzuia lisijirudie ,Ushirikishwaji ulikuwa mdogo kwa wadau husika haswa wazazi na walimu.
Mzazi kusikia tu kwenye vyombo vya habari au kuletewa barua kununua vitabu vipya hiyo haitoshi," Dkt Mugo anaeleza .
Aidha hali hii ya kukosolewa mitaala haijatokea Kenya tu hata Tanzania katika kipindi cha nyuma ilikutana na makosa ya kiuchapishaji ambayo jamii ilikosoa vikali.
Meneja wa programu kutoka mtandao wa elimu Tanzania(TEN/MET) Nichodemous Shauri amedai kwamba kwa mtunzi kuandika kuhusu utajiri wa mwanasiasa wa kusemekea ni maudhuhi ambayo hayajengi uzalendo na wala hayapingi ufisadi .
"Hata kwa upande wa Tanzania uchapishwaji wa vitabu vipya ulikosolewa pia na umma haswa katika picha na hii inatokana na kutozingatia maadili.
Hakuna uwekezaji wa kutosha ambao umewekwa kwa ajili ya marekebisho haya ya mitaala .
Hakuna mgawanyo mzuri ambao umewekwa, kuna ulazima wa kutenganisha majukumu; yaani wawepo watu wale ambao wataangazia utunzi, wengine wawe katika uchapishaji na kuwe na chombo ambacho kinahakiki ubora.
Kuna ulazima kazi hii iwe na ushindani kwa kutangazwa tenda ambayo malipo yanatolewa baada ya kazi kuhakikiwa kuwa ni nzuri.
Tanzania ilipitia changamoto kama hiyo na sababu ilikuwa fedha za ufadhili
Ushindani unaweza kusaidia ubora wa kazi kuwa mzuri.
Mitaala lazima ibadilike lakini ni kwa namna gani inabadilishwa hilo ndilo suala la msingi.