Mizani ya Haki: Idara ya mahakama Kenya inaimarika ama imelemewa?

Jaji mkuu David Maraga wa Kenya amemshutumu inspekta jenerali wa polisi Joseph Boinet Chief kwa kukataa wito wa kuimarisha usalama wa majaji na mahakama
Maelezo ya picha, Jaji mkuu David Maraga wa Kenya ameahidi kupunguza kesi zilizorundikana mahakamani
    • Author, Hezron Mogambi
    • Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi

Karibu kwa mfumo wa haki nchini Kenya ambapo msemo kuwa, kuchelewesha haki ni kumnyima haki mtu, ina ukweli ingawa kumekuwepo juhudi za kuboresha hali ya kutatua mizozo nchini.

Juhudi za kuhakikisha kuwa mfumo wa haki nchini Kenya unafanya kazi kwa muda ufaao na kuhakikisha kuwa kuna haki umekuwa ukipigwa jeki na shughuli mbali mbali za mashirika ya kila aina.

Itakumbukwa kuwa zaidi ya juhudi za Benki ya Dunia kupitia kwa mradi wa kuhakikisha uboreshaji wa huduma zinazotolewa na idara ya mahakama, maagizo ya jaji mkuu David Maraga mwanzoni mwa mwaka huu kuwa kesi ambazo zimekuwepo mahakamani kwa zaidi ya miaka mitano zinafaa kukamilishwa kufikia mwisho wa mwaka huu pia ni muhimu.

"Ni katika mazingira ambapo haki inawafikia wanyonge na mkondo wa sheria kuwalinda mafukara, ndipo sisi kama nchi, tunaweza kusema kuwa katiba yetu ina uwezo wa kuhakikisha usawa na haki," Jaji Maraga alisema.

Kupunguza mrundikano wa kesi

Takwimu za idara ya mahakama zinaonyesha kuwa idadi za kesi ambazo zimekuwepo mahakamani kwa zaidi ya miaka mitano katika mahakama kuu zilipungua kutoka 48,173 mwaka wa 2016 hadi kufikia 35,836 mwishoni mwa mwaka uliopita.

Kwa jumla, idadi za kesi ambazo hazikuwa zimeshughulikiwa ilipungua kwa asilimia 7 mwaka wa 2017.

Kesi nyingi ambazo hazijashughulikiwa katika mahakama za mahakimu ambako karibu nusu-asilimia 49.5 nt - ya kesi za jinai zilichukua zaidi ya mwaka mmoja na miezi mine kukamilisha.

Naibu Jaji mkuu Kenya Philomena Mwilu (Katikati)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Naibu Jaji mkuu Kenya Philomena Mwilu (Katikati)

Kwa upande mwingine, kesi za jinai zingineweza kukamilishwa tu kwa haraka iwapo mshtakiwa angepatikana kuwa na hatia.

Kwa jumla, kesi ambazo hazijashughulikiwa katika idara nzima ya mhakama nchini Kenya ni 315,378 katika mwaka wa 2016/17, kutoka idadi ya awali ya 344,659 mwaka uliotangulia, kulingana na ripoti za idara ya mahakama nchini Kenya.

Kinachoshangaza na kusikitisha zaidi ni kuwa kati ya kesi hizi ambazo hazijashughulikiwa, moja kati ya sita ama kesi 52,352 zimekuwemo kwenye mfumo wa idara ya mahakama bila kushughulikiwa kikamilifu kwa zaidi ya miaka 10 tangu ziorodheshwe mahakamani, hali ambayo ilikuwepo mwaka uliotangulia.

Theluthi moja ama kesi 66,214 bado haziamuliwa katika kipindi cha kati ya miaka mitano hadi miaka 10, theluthi moja au kesi 113,766 zilikuwa hazijaamuliwa kwa kati ya miaka miwili hadi mitano na robo moja au kesi 83,046 zilikuwa zimekaaa katika mfumo wa mahakama kwa kati ya mwaka mmoja hadi miwili.

Itakumbukwa kuwa kufikia mwaka wa 2016, kesi asilimia 30.66% zilikuwa zimekwama kwenye mfumo wa mahakama nchini Kenya kwa zaidi ya miaka mitano, kesi 13 zikiwa zimekwama kwenye mahakama kwenye mahaklama kuu kwa miaka 40, nyingine 81 zikiwa zimekwama kwenye mahakama ya rufaa.

Katika mahakama za chini hasa za hakimu, kesi asilimia 30% za kesi za madai zikiwa zimekwama kwa zaidi ya miaka mitano huku kesi zamakosa ya asilimia 23.5% zikiwa zimekwama kwa kati ya miaka miwili na mitano.

Uchunguzi uliofanywa na idara ya mahakama yenyewe ulionyesha kuwa tatizo hili lilisababishwa na maafisa wa idara, mawakili na walalamishi.

Kesi kuahirishwa mara kwa mara

Kucheleweshwa kwa kesi kulisababishwa na mahakama kuwa likizo(asilimia 22.4), kutokuwa tayari kwa pande zote mbili katika kesi(asilimia 19.1), kutokuwa tayari kwa askari polisi na maafisa wa uangalizi (asilimia 18.3) na kutokuwa tayari kwa mawakili ( asilimia 11).

Kuahirishwa kwa kesi kila mara - sababa kuu ya kucheleweshwa kwa kesi - ilipatikana kutokana na mawakili kutokuwa tayari kuendelea na kesi kwa sababu mbalimbali, kutokuwepo kwa pande zote mbili wakiwemo walalamishi na washtakiwa kukataa mashtaka.

Kadhalika, kuna faili ya polisi kutokuwepo mahakamani, makubaliano kati ya pande zote mbili kuahirisha kesi, waendesha mashtaka kutokuwepo mahakamani, shahidi wa kitaalamu kutokuwepo mhakamani, kubadilishwa kwa ushahidi, pande zote mbili kutaka kuelewa nje ya mahakama kati ya baadhi ya sababu.

Ripoti ya idara ya mahakama ya mwaka wa 2014, ilipendekeza kuwa utaratibu uwepo kuhusiana na uhamisho wa majaji na mahakimu pamoja na mafunzo kwa maafisa wa idara ya mahakama, kuboresha uhusiano na ushirikiano kati ya na baina ya wadau mbali mbali katika sekta ya haki kama vile mawakili, polisi, waendesha mashtaka, na mafunzo kwa maafisa wa idara ya mahakama kuhusu usimamizi wa kesi ili kukamilisha kesi kwa haraka iwezekanavyo.

Pendekezo kuu la ripoti hiyo yenye mada, "The Criminal Justice System Audit Report", iliyochapishwa mwaka wa 2017 na idara ya mahakama kupitia kwa National Council on the Administration of Justice (NCAJ), ni kwamba mfumo wa haki nchini Kenya, kwa kiasi kikubwa, unawaonea maskini na kuwapendelea matajiri.

Dereva wake amepigwa risasi na kujeruhiwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Naibu jaji Mkuu wa Kenya Philomena Mwilu

Ripoti hii inaeleza kuwa maskini wengi walikamatwa na polisi, wakashtakiwa na kufungwa ikilinganishwa na matajiri.

Kuhusiana na walioshtakiwa na makosa madogo madogo, ripoti hiyo ilieleza kuwa kulikuwepo na changamoto za utekelezaji wa maelekezo ya katiba kuwa wale walioshtakiwa na kupatikana na makosa ambayo kifungo chake hakizidi miezi sita au wanaweza kutoa faini tu, hawafai kuwa mikononi mwa polisi kwa zaidi ya siku mbili.

Mikataba ya utenda kazi

Itakumbukwa kuwa mahakimu na majaji nchini Kenya walitia saini ya utendakazi katika mwaka wa kifedha wa 2015-2016 na kutoka mwezi wa Juali 2015, wanahitajika kujaza fomu za kuonyesha jinsi walivyofanya kazi hasa kuhusiana na kushughulikia.

Sifa za kuonyesha utendakazi mwema katika kesi zinategemea kumaliza kesi kwa haraka, na maadili katika kushughulikia faili za kesi pamoja na mahitaji mengine.

Sifa hizi zinaonyesha utendakazi mwema pamoja na idadi na ubora wa kesi zilizoshughulikiwa ikizingatiwa kuwa baadhi ya kesi huhitaji muda zaidi ikilinganishwa na zingine.

Pia, kuna uchanganuzi wa kina wa mizani hii inyotumika kwani wakati mwingine haihusiani na takwimu ambazo mahakimu na majaji hutoa kuhusu kesi ambazo wamezishughulikia.

Sehemu ya 30 ya sheria inayohusu swala hili inaeleza kuwa kila jaji atatia saini mfumo wa kanuni na taratibu za idara ya mahakama, ufuatiliaji wake utasimamiwa na jaji msimamizi.

Kwa sababu ya hali hii, idara ya mahakama ilitenga wakati maalum wa kushughulikia kesi za zamani na kuamua kuhusu kesi hizi pamoja na kuanzisha mfumo wa kusimamia kesi na utendakazi katika idara nzima.

Benki ya dunia ndiyo iliyoanzisha mpango wa kuboresha utendakazi wa idara ya mahakama kupitia kwa mradi wa Judicial Performance Improvement Project (JPIP) ambapo Benki ya dunia ilitoa mkopo wa US$120 million wa miaka sita ili kuboresha usimamizi wa mahakamani, muundo msingi mafunzo kwa wafanyikazi wa idara ya mahakama, na usimamizi kwa jumla.

Mahakama ya juu ilitoa uamuzi wa kihistoria kwa kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi
Maelezo ya picha, Mahakama ya juu ilitoa uamuzi wa kihistoria kwa kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa rais mwaka jana

Kwa sasa, mahakama 100 zinaendelea kujengwa kote nchini kama njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa haki inawafikia wengi- mahakama 30 zikifadhiliwa na benki ya dunia kwa kima cha Sh12 bilioni na zingine 70 zikifadhiliwa na serikali ya kitaifa.

Itakumbukwa kuwa utendakazi wa idara ya mahakama unategemea uwekaji wa stakabadhi. Katika misingi hii, kuhakikisha kuwa stakabadhi zote za mahakama na shughuli za mahakama zote zinawekwa kwenye mifumo ya tarakilishi kama njia ya kuhakikisha uhuru na uwajibikaji wa mahakama.

Kuwapiga msasa majaji na mahakimu

Hili halitakuwa jambo geni bali litakuwa likienda sambamba na mfumo wa mabadiliko katika idara ya mahakama, mfumo ambao unatambua teknolojia kama njia mojawapo ya uwezeshaji na udumishaji haki katika idara ya mahakama.

Aidha, hali hii itasaidia wafanyikazi katika idara ya mahakama katika utendakazi wao, kusiaidia uzingatiaji wa maadili katika stakabadhi za idara na kupunguza mwanya wa ufisadi kwenye idara nzima.

Madai ya ufisadi na rushwa dhidi ya majaji na wafanyikazi wengine wa idara ya mahakama yameendelea kujitokeza , hali ambayo imepelekea wengi kudai kuwa kuna haja kubwa ya kuwa waangalifu kuhusiana na tabia na utendakazi wa maafisa wote wa idara ya mahakama hasa kuhusiana na taratibu za usimamizi wa fedha, uhasibu na ununuzi wa bidhaa na huduma.

Kuhusiana na majaji, inasikitisha kujua kuwa mfumo wa kuwapiga msasa majaji uliofanywa na bodi ya majaji na mahakimu na mchakato mzima wa kuwateua majaji, bado kuna madai ya ufisadi katika idara ya mahakama.

Hali hii imepelekea pendekezo la kuwapiga msasa maafisa wote wa idara ya mahakama. Aidha, hakuna uchanganuzi uliofanywa kuhusiana na athari za mchakato wa kuwapiga msasa na kuwateua maafisa wa idara ya mahakama wakiwemo majaji.

Hili linaonyesha kuwa kuna haja ya kujifunza kuhusiana na suala hili pamoja na taratibu nyingine ambazo zinaweza kuboresha hali katika idara hii muhimu.

Prof Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: [email protected]