Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zambia: Wachina wakamatwa wakitoa mafunzo ya kijeshi kwa mgambo Livingstone
Polisi nchini Zambia wanawazuilia raia wawili wa Uchina waliokamatwa wakitoa mafunzo kwa jeshi la mgambo mwishoni mwa wiki.
Mmoja alikamatwa Jumamosi na mwingine Jumapili katika mji maarufu kwa watalii nchini humo Livingstone.
Mkurugenzi wa shirika kampuni ya huduma za usalama ya Alert Safety Security mjini Livingstone pia anazuiliwa, kamishna wa polisi wa mkoa wa kusini nchini humo Bonny Kapeso.
Alisema kampuni hiyo imekuwa likitoa mafunzo bila kibali kutoka kwa polisi na kwamba na kwamba sare wanazotumia zinafanana sana na zile zinazotumiwa na maafisa wa Mamlaka ya Taifa ya Mbuga na Wanyamapori.
Polisi walipata pia bunduki za rashasha, bastola na risasi.
Kampuni hiyo ya usalama haijazungumzia kisa hicho, wala washukiwa wenyewe.
Katika siku za karibuni, kumekuwepo na taarifa kuhusu kushiriki kwa raia wa China katika shughuli za kiusalama nchini Zambia na pia deni la taifa hilo.
Desemba mwaka jana, maafisa wa polisi nchini Zambia walifutilia mbali mpango wa kuwaajiri raia wanane wa Kichina kuwa polisi wa akiba nchini humo.
Walichukua hatua hiyo saa 24 baada ya kuzindua mpango huo kutokana na shutuma kutoka kwa raia.
Maafisa hao wapya walikuwa wamepewa jukumu la kupiga doria mjini Lusaka siku.
Lakini uamuzi huo ulizua hisia kali kutoka kwa raia hususan kutokana na agizo jipya lililotolewa mapema mwaka huo ambalo linapiga marufuku maafisa wa polisi kuoa wageni kutokana na sababu za kiusalama.
Raia wa Zambia wenye uraia wa mataifa mawili pia hawaruhusiwi kujiunga na kikosi cha polisi.
Dickson Jere, ambaye ni wakili, alisema kuwa uteuzi huo ulikiuka katiba ambayo inasema wazi kuwa, Mzambia yeyote aliye na uraia wa nchi mbili hawezi kujiunga na idara za usalama.
Msemaji wa polisi nchini Zambia Esther Mwata-Katongo, alitetea uteuzi huo wa polisi akisema kuwa kabla ya wao kuteuliwa walichunguzwa na watafanya kazi chini ya usimamizi wa polisi wa kawaida.