Rais Magufuli amelizindua rasmi Daraja la juu la Mfugale Tanzania

Rais wa Tanzania John Mafuguli ameizindua rasmi barabara ya juu ya Tazara iliyopewa jina rasmi la daraja la juu la Mfugale Tanzania.
Barabara hiyo ni ya kwanza ya juu katika historia ya nchi hiyo, inayounganisha sehemu kuu ya mji huo na maeneo makuu ya kiuchumi nchini kama uwanja mkuu wa ndege wa Julius Nyerere, Bandari na hata barabara inayoelekea Viwandani.
katika ufunguzi huo rasmi, raisi Magufuli ameonya juu ya matumizi mabaya ya daraja hilo na amewataka watanzania kuwa makini ili kuepuka ajali.
Kadhalika ameagiza kamera za ulinzi zifungwa kwenye daraja hilo la juu mara moja.
Amewataka wataalamu kuwa wazalendo hasa wale wa Stiglers Gourge , ambao wametoa mapendekezo anayosema si ya kizalendo na wasikubali kutumika kwa maslahi ya wageni.
Kuna mchanganyiko wa hisia kufuatia kukamilika na kuanza kutumika kwa bara bara hiyo.
Kwa baadhi inakuja kama ahueni kuu kutokana na msongamano mkubwa wa magari na kero la foleni zinazo shuhudiwa kila siku mjini.

Chanzo cha picha, Reuters
Ali mkaazi wa mji aliyefika katika uzinduzi huo hii leo, amesema, 'Usafiri utakuwa umerahisika, wananchi tutakuwa tumepata fursa, na mambo ya foleni yatakuwa yamepugua, kwenda kazini zilikuwa zinatupa shida sana'.
Barabara hiyo inajumuisha njia nne na daraja. Kwa kupunguza tatizo la msongamano na foleni inatarajiwa kuongeza muda wa watu kufanya kazi badala ya mwingi wanaopoteza wanapokwama barabarani.
Hili linatazamwa na serikali kama kufungua njia kwa wananchi kuukuza uchumi wa nchi.

David Masanja mkaazi mwingine mjini Dar Es Salaam naye anaeleza, 'Kulikuwa na shida kubwa sana, tulikuwa tunapoteza fedha nyingi sana kwasababu muda wa kwenda kazini ulikuwa ni mwingi sana. Sasa kufika kazini tutakuwa tunaenda na kufika kwa wakati na tutaongeza tija'.
Kadhalika kuna wanaokosoa mradi huo kutokana na fedha zilizotumiwa kwa ujenzi huku wengine wakigusia ukubwa kwa kumithilisha na barabara nyingine za juu zilizojengwa katika nchi jirani.
Ujenzi wa barabara ya juu ya Tazara unatajwa kugharimu takriban $ milioni 42.
Injinia Mfugale na mchango kwa daraja
Injinia Mfugale ambaye daraja hilo la juu limepewa Jina lake, ameelezea sifa za daraja na namna alivyopata changamoto katika kufanikisha kuidhinishwa kwa mkataba wa ujenzi wa daraja hilo ikiwemo hata kuambiwa asirudi nchini na rais Magufuli ambaye kwa wakati huo alikuwa waziri wa ujenzi.

'Ukiwa waziri wa ujenzi ulinituma Japan kwenda kuweka sahihi mkataba wa kazi hiyo, lakini tulikuwa hatujapata mkandarasi.
'Na ulinielekeza kuwa nisirudi huku mpaka niwe nimesaini mkataba.
Na nilipoiambia Japan nimeambiwa na nchi yangu nisirudi, wakasema viza yako imeisha, kwa hiyo ni lazima urudi, nikasema ninaweza nikakaa hata railway stesheni, ili mradi kama mkimbizi lakini tenda hii tutafute namna ya kufanya daraja hili lijengwe.
Mfugale ameeleza kwamba hapo ndipo walipofikia hatua ya manunuzi inayotajwa kuwa 'Selective tendering', wakachagua wakandarasi wanaofaa na mkataba ndipo uliposainiwa mnamo Oktoba 15, mwaka 2015.

Barabara ya juu ya Tazara ilifunguliwa tangu Septemba 15 kuruhusu waendesha magari kuijaribu kuelekea uzinduzi huu leo.
Raia katika mji wa Dar Es salaam wanatarajiwa kumiminika kuanzia hivi asubuhi katika barabara hiyo ya juu kushuhudia ufunguzi rasmi wa muundo mbinu huo nchini.
Hata hivyo serikali Tanzania inasema huu ni mwanzo tu kwani ina mpango wa kujenga madaraja mengine kama hayo kwenye maeneo mengine ya makutano ya barabara ili kupunguza foleni.
Miongoni mwa walioizuru barabara hiyo wakati mradi ukielekea kukamilika ni Waziri mkuu Kassim Majaliwa.
Majaaaliwa amenukuliwa akisema kwamba serikali inapanga kuzindua barabara nyingine saba kama hizo mjini Dar Es Salaam katika kukabiliana na msongamano na foleni kubwa za magari.

Ujenzi wa barabara ya juu ya Tazara ulianza Octoba 2016, kwa udhamini kamili wa serikali ya Japan.
Kwa sasa serikali ya nchi hiyo inaendelea na mradi mwingine wa madaraja ya juu katika barabara nyingine Morogoro kwenye makutano ya Kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo.
Wasifu wa Mhandisi Patrick Mfugale
Patrick Aron Nipilima Mfugale Alizaliwa katika eneo la Ifunda huko Iringa.
-Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Consalata Fathers Primary School mjini Iringa
-1975 Alimaliza elimu yake ya shule ya upili katika shule ya upili ya Moshi.
-1977-Mfugale aliajiriwa katika wizara ya ujenzi
-1983 alijipatia shahada yake ya kwanza katika chuo kikuu cha Rocky nchini India
-1991 Mfugale alisajiliwa kama muhandisi mtaalam.
-1992- Aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa barabara za mikoa.
-1994-1995-Alipokea shahada yake ya pili katika chuo kikuu cha Loughborough, Braunshweig nchini Uingereza
-2003-Alipokea tuzo ya Distinguished Engineering Accomplishment.
-Aliteuliwa kuwa muhandisi mkuu wa madaraja nchini Tanzania wakati huohuo na akiwa masomoni nchini Uingereza mwaka 1995 alitafiti na kutengeneza mfumo wa madaraja nchini.
-Alitengeza mfumo wa usimamizi wa madaraja kwa jina Tanzania Bridge Management System
-2014- Alisajiliwa kuwa muhandisi mshauri na kuwa mwanachama wa chama cha wahandisi Tanzania.
-Ametumia muda wake mwingi kama mtaalamu wa madaraja .
Alibuni daraja la Magarasi lenye mita 178 kwa shilingi za Tanzania milioni 300.
-Baadhi ya madaraja alioweza kujenga ni:
Daraja la Mkapa Rufiji
Daraja la Umoja linalounganisha tanzania na Moxzambique huko Ruvuma.
Daraja la Rusumo huko Mara
Daraja la Kikwete huko Magarasi.
Daraja la Nyerere huko Kigamboni
- Mfugale ambaye kwa sasa ni mtendaji mkuu wa Tanroads amesaidia ujenzi wa madaraja 1400 nchini Tanzania.
Amebuni na kusimamia barabara za kitaifa zenye urefu wa takriban kilomita 36,258.
- Ni Mwenyekiti wa kikosi cha ujenzi wa Reli ya kisasa SGR inayoendelea kujengwa.
- Ni mjumbe wa timu ya majadiliano ya miradi mikubwa ya umeme.
-2018 Alituzwa tuzo ya uhandisi ya Engineering Execellency














