Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Polisi wa Kenya: Je, mabadiliko ya idara ya polisi Kenya yatasaidia kuleta sifa mpya?
- Author, Hezron Mogambi
- Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi
Swali linaloendelea kuzua mjadala nchini Kenya kuhusiana na mabadiliko yaliyofanyiwa kikosi cha polisi nchini Kenya majuzi ni: Je, mabadiliko hayo yatasaidia kuleta sura mpya katika kikosi hiki?
Katika mabadiliko hayo, kikosi cha polisi sasa kimepewa sare mpya za kazi ambazo ndizo zilizozua mjadala mkubwa zaidi mtandaoni.
Hatua pia imechukuliwa kuwaruhusu maafisa wa ngazi za chini waliokuwa wakiishi katika makaazi duni kuishi pamoja na raia kwa kuwapa pesa za kulipia kodi ya nyumba pamoja.
Aidha, kumefanywa mabadiliko katika usimamizi na mfumo wa usimamizi wa kikosi kizima kuanzia ngazi za kitaifa hadi mashinani.
Mabadiliko hayo yamekuwa yakisubiriwa na Wakenya kwa muda mrefu ili kuboresha huduma, lakini baadhi ya Wakenya wamepokea tangazo la hatua zilizochukuliwa kwa kutilia shaka manufaa yake.
Aidha, baadhi wamekuwa wakibeza sare hiyo mpya ya polisi ya rangi ya samawati ambayo kwao inaonekana kufanana sana na sare za polisi wa China na kuzua hisia kwamba Kenya imeamua kukumbatia mshirika wake mpya kutoka Mashariki, 'kikamilifu' kwa kuiga hata sare.
Itakumbukwa kuwa kikosi cha polisi nchini Kenya kimekuwa kikikumbwa na matatizo na lawama nyingi kiasi cha kutowaridhisha Wakenya katika utendakazi wake.
Kimsingi, hali ambayo kikosi hiki kimekuwa kikifanyia kazi ni hali ambayo imekuwa ikibadilika kila kukicha. Hali ya kijamii nchini Kenya kutokana na watu kuhama kutoka sehemu za mashambani na kuelekea mjini, simu za rununu, tamaduni mpya kutokana na uhamaji, mitandao ya kijamii, makundi ya kigaidi na masuala mengine ya kitaifa na kimataifa yanaendelea kuathiri jinsi polisi wanavyofanya kazi yao katika miktadha mbali mbali.
Kazi ya vikosi vya polisi ambavyo sasa vimejumuishwa katika kikosi kimoja imeendelea katika miktadha tofauti tofauti isiyolingana. Kuna jamii za kuhamahama ambazo zinaishi katika sehemu kame za Kenya hasa kwenye mpaka wa maeneo ya kaskazini mashariki.
Maeneo haya hayahudumiwi vyema na polisi kwa sababu ya uchache wao. Katika sehemu hizi, jamii zinakumbana na visa vya utovu wa nidhamu na ujambazi wa hali ya juu.
Kuwepo kwa silaha haramu mikononi mwa makundi haramu pamoja na wizi wa mifugo wa kila mara kunaharibu mambo pamoja na vikosi vya polisi vinavyoshughulikia hali yenyewe kwa kutumia nguvu kupita kiasi.
Katika miji mikuu na mitaa yake, kuna changamoto nyingi zinazokumba usalama na kikosi cha polisi pia. Katika sehemu hizi, visa vya uhalifu unaofanywa kupitia kwa teknolojia kama vile uundaji wa bidhaa ghushi, wizi wa kimitandao, na wizi wa hakimiliki ni mambo yanayotatiza vikosi vya polisi. Ushambuliaji wa watu wanapokwenda ama kutoka kazini ni visa vinavyoongezeka.
Pia, Kenya ni nchi iliyo na watu wa kutoka nchi mbali mbali: kuna mabalozi, watalii, wakimbizi, na wageni wengine.
Wageni hawa huishi katika maeneo maalum hata kama ni katika mitaa ya miji na huhitaji huduma maalum za kikosi cha polisi.
Huduma za polisi za kiwango cha juu ni ngumu sana kutolewa katika hali kama hii. Hii ni kwa sababu itahitaji upangaji mzuri wa jinsi ya kuzishughulikia jamii kama hizi na matarajio yao ikikumbukwa kuwa sio matarajio yao yote yanatashughulikiwa.
Kubadili mfumo na utamaduni
Ni kweli kwamba kumekuwepo na mabadiliko siku za hivi karibuni katika kikosi cha polisi nchini Kenya hasa baada ya kubadilika kwa katiba: kuongezeka kwa maafisa wa polisi kwenye kikosi kizima, matumizi ya vifaa vya kisasa, na kuanzishwa kwa maendeleo mapya katika kikosi kupitia kwa mifumo ya kuwajuimisha wananchi ikiwemo mfumo wa nyumba kumi.
Hata hivyo, tatizo kuu katika mabadiliko haya ni kuwa kati ya mikakati hii ya mabadiliko iliyotumika, hakuna hata moja iliyolenga kubadili kabisa mifumo ya kimsingi ya ulinda usalama nchini Kenya pamoja na utamaduni wa utendaji kazi katika idara hiyo.
Ni dhahiri kuwa maono ya Serikali ya Kenya kuhusu mabadiliko katika kikosi cha polisi ni kukifanya kikosi chenyewe kuwa kikosi chenye taaluma na utendakazi mzuri ambacho Wakenya wanaweza kuwa na imani kwamba watahakikishiwa usalama wao.
Kutumia vibaya mamlaka
Mabadiliko ambayo kikosi chenyewe kimefanyiwa yanaonyesha ari ya serikali kufikia lengo hili kwa kuwa pesa nyingi zimetumiwa katika kufikia baadhi ya hatua hizi.
Hata hivyo, katika kufikia baadhi ya hatua hizi, kikosi cha polisi kimekuwa kikilaumiwa kwa kukosa kufikia malengo yake katika maeneo na jamii mbali mbali.
Baadhi ya tetesi zimekuwepo tangu nyakati za ukoloni hadi sasa hasa katika sura mbaya na jina na sifa za kikoloni na utumiaji mbaya wa mamlaka.
Hata katika kuundwa kwa huduma ya kitaifa ya polisi, misingi mipya ya huduma za polisi kwa wananchi ili kuchukua ile ya zamani ya 'kuchunga, kulinda na kuangalia' ni jambo ambalo halijafikiwa hadi sasa.
Kwa raia wengi nchini Kenya, mabadiliko katika kikosi cha polisi yanamaanisha jambo tofauti kabisa. Kwao, mabadiliko yanafaa kukibadilisha kikosi cha polisi na lengo lake ili kuboresha usalama na hali ya watu na jamii mbali mbali. Wangependa kuona polisi wakifanya kazi na makundi mbali mbali katika jamii kwa njia ambayo ni wazi kwa wote pamoja na kufikia na kubuni njia za kuzuia uhalifu.
Wanataka kuona polisi wakifanya kazi yao kwa namna ambayo inasaidia mshikamano, usawa na heshima katika jamii.
Mabadiliko katika kikosi cha polisi yamehusisha, kwa kiasi kikubwa, mabadiliko makubwa sana katika sekta ya umma, kama ugatuzi.
Fedha nyingi zimetumika katika kuboresha vifaa vya utendakazi vya kikosi hiki kama uundwaji wa huduma ya kitaifa ya polisi, tume ya huduma za polisi, na taasisi nyingine kama vile kitengo cha mambo ya ndani, na mamlaka simamizi ya polisi (Independent Policing Oversight Authority). Misingi ya mabadiliko imefikiwa lakini changamoto na matatizo bado ni tele.
Huku mabadiliko yakiendelea kufanywa katika kikosi cha polisi, kuna mambo ambayo yamefanywa ambayo yanaonyesha kuwa hatua nzuri zinaendelea kufikiwa.
Taasisi zote ambazo zinatakiwa ili kutekeleza mabadiliko ya awali tayari zinafanya kazi na sera na maelekezo mapya pamoja na uajiri, kupandishwa vyeo, nidhamu, usalama katika jamii, polisi wa akiba, uhamisho kwenye kikosi, ni baadhi ya mambo ambayo yameshughulikiwa na taasisi hizi mpya.
Kwa upande mwingine, kikosi cha polisi bado kinaonekama kuwa chenye kujishughulisha na udhibiti wa usalama badala ya kutoa huduma kwa umma.
Ukosefu wa ushirikiano
Bado kikosi chenyewe hakijafikia hali ya kulenga kuzuia uhalifu kabla ya kutokea badala ya kushughulika baada ya tukio. Hili linatokana na kutokuwepo kwa ushirikiano miongoni mwa wadau mbali mbali katika jamii ikiwemo polisi.
Hapajakuwepo na mkakati wa kuzuia uhalifu kabla ya kutokea ambao unawahusisha wote katika kuzuia uhalifu na polisi huwa hawawahusishi umma katika kutoa ushauri kuhusu uhalifu. Kwa sababu hii, katika baadhi ya maeneo, visa vya uhalifu bado vinaendelea kuongezeka na kutoripotiwa.
Hali hii inatokana na umma kukosa kuwa na imani na kikosi cha polisi na mfumo mzima wa haki.
Aidha, ufisadi bado ni tatizo huku ukosefu wa maadili na hatua za kufikia hali hii ikionekana kuwa changamoto kubwa.
Hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa dhidi ya maafisa wa polisi kama vile kuwafumania wakila mlungula kisiri, bado hazijasaidia.
Mfumo wa kikosi, mabadiliko, usimamizi usiokubali ufisadi, uongozi bora, mpangilio na bajeti, na kuratibu na kufuatilia utendakazi ni baadhi ya changamoto nyingine.
Mabadiliko katika kikosi cha polisi nchini Kenya bado hayajaleta sifa ambazo umma wa Kenya unatarajia.
Hata hivyo, pamoja na changamoto na matatizo, kikosi cha polisi nchini Kenya kinafaa kulenga nafasi yake katika usalama wa umma na jamii.
Sifa mbaya na tabia miongoni mwa maafisa wa polisi ambazo zinaaathiri utendakazi wa kikosi zinafaa kuangaziwa zaidi ili kuunda kikosi thabiti kinachohudumia jamii na nchi ifaavyo.
Prof. Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: hmogambi @ yahoo.co.uk