Je kufutwa kwa matangazo kuhusu uzazi wa mpango Tanzania kutakuwa na athari gani?

Wanawake zanzibar

Chanzo cha picha, Majority World

Maelezo ya picha, UNFPA linasema ni haki ya wanawake na wasichana kufanya maamuzi yao ya uzazi wa mpango

Siku moja baada ya wizara ya afya nchini Tanzania kupiga marufuku matangazo ya redio na televisheni kuhusu uzazi wa mpango, hisia mbali mbali zimeendelea kutolewa.

Stelia Atanus Muhenzi mfanyi biashara katika jiji la Dar es Salaam anasema, ''Ni bora wasifute matangazo hayo ili kila mmoja anayetumia hizo dawa ajue na atambue jinsi zinavyotumika''.

Anasema kuna baadhi ya watu wanaoishi vijijini ambao hawajui uzazi wa mpango ni nini, kwa hiyo wanapaswa kuelewa kupitia matangazo ya redio ama televisheni.

Hata hivyo kuna wengine wanaunga mkono kauli ya rais John Magufuli kwamba watu wazaane.

Mmoja wao ni Iddi Mahamoud Fanga, ambaye anasema ''Watu wazaane tu vya kutosha''.

Marufuku hiyo inayawacha wapi mashirika yaliowekeza katika uzazi wa mpango?

Mpaka sasa mashirika ya kimataifa yanayoendesha mikakati ya uzazi wa mpango Tanzania hayajatoa tamko lolote.

Hata hivyo, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA)

  • Ni haki ya wanawake na wasichana kufanya maamuzi yao ya uzazi wa mpango ni muhimu na msingi wa maendeleo endelevu.
  • Wanamazingira nao wanasema dunia ina wajibu wa kuwapa nguvu wanawake kusimamia afya yao ya uzazi.
  • Njia moja ya kupunguza msongamano na kung'ang'ania raslimali chache zilizobakia duniani.

Hapo jana Wizara ya Afya nchini Tanzania imesema kwamba, imekuwa ikiendesha zoezi la kusaili ubora wa matangazo yote kuhusu uzazi wa mpango.

Matangazo hayo ni pamoja na yale yanayotolewa katika redio na televisheni nchini humo.

Akizungumza na BBC mkurugenzi msaidizi wa kitengo cha afya ya mama na mtoto kutoka wizara ya Afya, Dr Mohamed Makuani, amesema zoezi hilo limekuwa likiendelea hata kabla ya tamko la hivi karibuni la raisi John Pombe Magufuli.

Wanawake zanzibar

Chanzo cha picha, Majority World

Maelezo ya picha, Kwa mujibu wa UNHabitat upngaji wa uzazi ni njia moja ya kupunguza msongamano na kung'ang'ania raslimali chache zilizobakia duniani

''Kimsingi hili ni suala ambalo tulikuwa tushapanga toka siku nyingi na hata kabla rais kulizungumzia suala hili''.

Baadhi ya mbinu ya uzazi wa mpango kama vile mipira kondomu, inasaidia kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV na magonjwa menengine ya zinaa.

Uzazi wa mpango pia unapunguza visa vya utoaji mimba hasa kwa njia isiokuwa salama.

Inawapatia watu uhuru wa kuamua idadi ya watoto wanaotaka na kupanga muda watakaozaliwa.

Takwimu za Idadi ya watu Tanzania

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali zilizotolewa mwezi Februari 2018, Tanzania kuna watu milioni 54, na ongezeko la watu linakadiriwa kufikia milioni 1.6 kila mwaka.

Katika kupambana na ongezeko hilo kubwa la watu, Kenya wamefanikiwa kuongeza matumizi ya njia za uzazi wa mpango ambapo kwa sasa 53% ya wanandoa walikuwa, wakitumia uzazi wa mpango kufikia mwaka 2014 kutoka 39% kwa mwaka 2008/2009.

Serikali ya Tanzania pia imekuwa ikiwekeza katika kuchagiza matumizi ya uzazi wa mpango ambapo kwa mwaka 2018/19 imetenga shilingi bilioni 22 kwa ajili hiyo.

Tangu aingie madarakani mwaka 2015 raisi Magufuli ametoa mapendekezo kadhaa ya sera yanayotazamwa kuwa na utata.