Kauli ya rais Magufuli kuhusu uzazi wa mpango yaibua hisia tofauti Tanzania

Wizara ya afya Tanzania imedai kuwa kauli ya rais John Magufuli kuhusu uzazi wa mpango haikueleweka ipasavyo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wizara ya afya Tanzania imedai kuwa kauli ya rais John Magufuli kuhusu uzazi wa mpango haikueleweka ipasavyo

Wizara ya afya Tanzania imedai kuwa kauli ya rais John Magufuli kuhusu uzazi wa mpango haikueleweka ipasavyo.

Katibu mkuu wa wizara ya afya nchini humo Dkt Mpoki Ulisubisya akiongea na waandishi wa habari amesema kwamba inawezekana watu hawakumuelewa rais .

"Rais alisema watu wazae kulingana na uwezo wa kutunza famila zao na mheshimiwa rais alisema, watu wasizuiwe kuzaa na vilevile mtu asiyefanya kazi hawezi kutunza familia yake" Dkt Mpoki alifafanua hivyo.

Hata hivyo Dkt.Mpoki amesisitiza kuwa msimamo wa Sekta ya afya unaangalia mafundisho msingi ambayo yanafundishwa dunia nzima kuhusu afya ya mama na mtoto .

Mafundisho hayo yanaeleza kuwa ni vyema kwa mama kuweka nafasi kati ya ujauzito mmoja na mwingine kwa ajili ya afya ya mama na mtoto.

"Sekta ya afya haijawahi kutoa tamko au mashirika ya maendeleo hayajawahi kutoa tamko la kusema watu wazae watoto wawili au mmoja kama ilivyo katika mataifa mengine.Kitaalamu mtu akipata mtoto akiwa na umri mdogo au akizaa mara kwa mara ana uwezekano mkubwa sana kupata changamoto za kiafya",Dkt Mpoki alieleza.

Tamko hilo kutoka wizara ya afya limekuja mara baada ya rais Magufuli kutoa kauli inayosema kwamba watu wanaotumia dawa za kupanga uzazi ni wavivu.

"Wanawake sasa wanaweza kuacha kutumia dawa za kupanga uzazi, Ukiwa na chakula cha kutosha zaa." Rais wa Magufuli alisema.

Na kauli hiyo ambayo ameitoa siku ya jumapili katika mkoa wa Meatu, haikuwa mara ya kwanza kwa sababu rais Magufuli aliwahi kunukuliwa mara kadhaa akisema 'fyatueni tu na serikali itawasomesha', jambo ambalo waziri wa Afya aliwahi likanusha kwa kudai kuwa alikuwa anatania.

rais tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Tanzania ,John Pombe Magufuli kuwataka wanawake amedai wanaotumia njia za uzazi wa mpango ni wavivu

"Tunachotakiwa watanzania, ni kuchapa kazi ili kusudi watoto utakaowazaa uwalishe. Kama huwezi kufanya kazi, hapo ndipo utumie mpango wa uzazi, wale ambao hawafanyi kazi, wavivu ndio wanajipangia watoto" Rais Magufuli alieleza.

Kauli hii imepokewaje na raia Tanzania?

Aidha kauli ya rais Magufuli imeweza kuibua hisia mbalimbali kwa watanzania, huku kila mmoja akitafsiri kwa aina yake na haya ni baadhi ya maoni ya wananchi nchini humo;

''Naitwa Sara, mimi kauli hiyo naona ni sawa tu,Kama mtu Mungu amekujaalia uwezo wa kuweza kujifungua bila matatizo yoyote na una uhakika kuwa unaweza kuwatunza na kuwapatia huduma muhimu watoto,watanzania tuitikie huo wito tuzae tu. Nina mtoto mmoja natazamia kuzaa kama wanne tuseme.Mimi mwenyewe ni wanne,ndio maana nachakarika ila uwezo ukiruhusu wanne''.

''Kwa jina naitwa Yohana mshai, ni mkaazi wa Kawe Dar es Salaam.Hajazungumza vibaya isipokuwa tuangalie sisi kama wazazi.Majukumu ya ulezi ni ya kwetu sisi wazazi,tuzae hata kama tutazaa wengi,cha msingi tuwalee katika malezi mazuri ambayo hawatajiingiza katika vitendo viovu pengine kwa kukosa zile huduma za kijamii kutoka kwa sisi walengwa ambao ndio sisi wazazi wa hao watoto''.

Licha ya mashirika yanayohusika na kampeni za uzazi wa mpango kugoma kutoa tamko lolote juu ya mkanganyiko huko, Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA kimekosoa vikali kauli ya Rais wa nchi hiyo John Magufuli juu ya kutokuwepo kwa umuhimu wa uzazi wa mpango.

CHADEMA inasema kuwa uzazi wa mpango ni suala ambalo linapaswa kutizamwa sio tu kisiasa bali kwa namna ambayo haitaleta athari kwa wananchi.

world bank

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Utafiti uliofanywa na shirika la world bank unaeleza kuwa watu mil.23 nchini Tanzania wanaishi kwa kipato cha chini kabisa kwa siku ambacho ni dola 1.9

Na kwa upande wao wanaharakati wa masuala ya wanawake, wamepinga vikali tamko hilo na kudai kuwa linamkandamiza mwanamke.

Jean Paul Murunga kutoka Equality Now,shirika linaloangazia masuala ya mimba za utotoni wanasema kwamba kauli hiyo inapunguza uwezo wa mwanamke katika kufanya maamuzi.

"Hata kama rais alisema kuwa matamshi yake sio sheria lakini mtazamo utachukuliwa tofauti kutokana na cheo chake.

Tamko kama hilo mbele ya umma linaweza kusababisha mgogoro katika familia"Jean Paul alieleza.

Jean aliongeza kwa kusema kwamba takwimu zinasema zaidi ya asilimia 30 wanazaa kabla ya miaka 18 nchini Tanzania hivyo inamaanisha kwamba hawa watu wasipotumia kinga au njia ya uzazi wa mpango basi anaweza kuzaa hata watoto kumi.

Na ukiangalia huyu msichana hana elimu wala kazi ya kumpatia kipato kizuri hivyo basi mwisho wa siku mzigo lazima utarudi kwa serikali na suala la kuleta maendeleo likawa ni kinyume.

Hata hivyo tamko hilo linakanusha makubaliano ya kimataifa ambayo Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuweka sahihi katika mkataba kama wa Maputo.

Na miongoni mwa makubaliano muhimu ilikua suala la haki ya mwanamke.

Vilevile Shirika la world bank limefanya utafiti ambao umeeleza kuwa Tanzania ni zaidi ya watu mil.23 wanaoishi chini ya dola 1.9.

Na ukiangalia matumizi ya kawaida ya binadamu kiwango hicho cha fedha ni kidogo sana hivyo hali ni ngumu kwa wengi ambapo inaonyseha wazi kuna tatizo la maendeleo kwa idadi ya watu ni takribani million 55 kwa mujibu wa world bank.

mpango
Maelezo ya picha, Baadhi ya njia za uzazi wa mpango

Mpango wa uzazi unasaidia familia kuweza kuweka mazingira mazuri ya kimaendeleo kwa kuzaa watoto wanaowahitaji na kuweza kuwahudumia katika upande wa afya,elimu na kukuza uchumi.

Petrider Paul kutoka shirika la Women rights, yeye pia naunga mkono tamko hilo kuweza kuleta madhara kwa wanawake haswa wa vijijini.

''Elimu sio bure kabisa ,kuna mahitaji mengine mengi, Kwa sasa vijana wapo wengi lakini hawana ajira ,Wanaume wanaweza kutumia kauli ya rais kuchochea kwa wanawake kuzaa zaidi

Kampeni za uazi wa mpango zipo kwa muda mrefu na zimeweza kusaidia kwa kiwango kikubwa lakini mpango huo ukikoma basi athari kubwa itawafikia wanawake" Petrider alieleza.

Huku shirika lingine lililokataa kutajwa lilidai kuwa kuna njia za mpango wa uzazi zinazosaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi na magonjwa ya zinaa,je kwa upande huo suala limefikiriwa na kuna ulazima wa sera zipitiwe upya maana kuna utaratibu ambao unahitajika kufuatwa na serikali.

Takwimu za Idadi ya watu Tanzania

Kwamujibu wa takwimu rasmi za serikali zilizotolewa mwezi Februari 2018, Tanzania kuna watu milioni 54, na ongezeko la watu linakadiriwa kufikia milioni 1.6 kila mwaka.

Katika kupambana na ongezeko hilo kubwa la watu, Kenya wamefanikiwa kuongeza matumizi ya njia za uzazi wa mpango ambapo kwa sasa 53% ya wanandoa walikuwa wakitumia uzazi wa mpango kufikia mwaka 2014 kutoka 39% kwa mwaka 2008/2009.

Serikali ya Tanzania pia imekuwa ikiwekeza katika kuchagiza matumizi ya uzazi wa mpango ambapo kwa mwaka 2018/19 imetenga shilingi bilioni 22 kwa ajili hiyo.