Watafiti wamepata mabaki ya pombe ya zamani zaidi duniani mjini Haifa, Israel

Wataalamu wa vitu vya jadia wakiwa ndani ya pango moja karibu na milima ya mji wa Haifa kaskazini mwa Israel

Chanzo cha picha, DANI NADEL/AFP/Getty

Maelezo ya picha, Wataalamu wa vitu vya jadi wakitafuta ushahidi wa vyakula vya mimea baada ya kugundua mabaki ya pombe

Watafiti wamefichua kiwanda cha pombe kilicho na mabaki ya pombe yaliodumu takriban miaka 13,000 iliopita katika pango la zamani karibu na mji wa Haifa nchini Israel.

Walifikia ugunduzi huo wakati walipokuwa wanafanya uchunguzi kuhusu eneo la makaburi ya jamii ya wafugaji wa kuhama hama ambao walikuwa wawindaji.

Utengenezaji wa pombe unadhaniwa kuwepo tangu miaka 5,000 iliopita lakini ugunduzi huu huenda ukabadili historia ya utengenezaji wa kinywaji hicho.

Ugunduzi huo pia huenda usiashirie kuwa kileo hicho kilitumika kuoka mikate kama ilivyodhaniwa.

Wanasayansi wanasema hawana uhakika ni kitu gani kilivumbuliwa kwanza kati ya pombe na mkate.

Picha iliyopatikana katika na AFP katika Chuo kikuu cha Haifa inamuonyesha mtaalamu wa vitu vya jadi akiwa ndani ya pango la Raqefet,katika Milima ya Carmel, kaskazini mwa Israeli

Chanzo cha picha, DANI NADEL/AFP

Maelezo ya picha, Vitalu vya vifuniko vilipatikana kwenye pango la Raqefet katika Milima ya Carmel, kaskazini mwa Israel

Pombe hiyo ya zamani,ambayo ilikuwa inafanana na uji, inadhaniwa kuwa na tofauti kubwa na pombe ya sasa.

Kundi hilo la wanasayansi limefanikiwa kutengeneza tena pombe hiyo ya zamani ili kulinganisha na mabaki waliopata

Utafiti huo unasema,hatua ya kwanza ya kutengeneza pombe hiyo, ilihusisha kuotesha mbegu ya nafaka ili kupata wishwa na unga unaohitajika.

Mchanganyiko huo baadae ulipashwa moto na kusindikwa kwa kutumia hamira ya kienyeji.

Inasemekana pombe ya zamani ilisindikwa lakini ilikuwa haileweshi kama pombe ya kisasa.