Matumizi ya nishati ya jua yashamiri katika kijiji hichi Rwanda

Rwanda imekuwa ikijaribu kutatua tatizo la nishati ya umeme kwa kutumia njia mbali mbali.
Katika kile kinachoelezwa kuwa mapinduzi ya nishati ya umeme, wananchi hasa wa maeneo ya vijijini wamechangamkia kutumia nishati ya umeme inayotokana na miale ya jua.
Waanzilishi wa mradi huo wanasema nishati hiyo ni rahisi kwa matumizi, gharama ndogo na hifadhi kwa mazingira.
Katika soko la Kabarondo mashariki mwa Rwanda, wananchi wanajiandikisha kwa wingi kununua vifaa na mitambo ya umeme unaotumia miale ya jua.
Malipo pia ni papo hapo kwa njia ya simu inayofahamika kama mobile money.
Bwana Ndoramaherezo Pierre amelipia huduma hiyo na anaandamana na fundi wa kusimika vifaa na mitambo ya miale ya jua.

Baada ya kumwekea mitambo hiyo sawa sawa, tayari anaanza kutizama runinga.
''Ni furaha ya kupita kiasi kupata vifaa hivi vya umeme.ndoto yangu imetimia.Hii ni hatua kubwa katika maisha yangu na mapinduzi katika kijiji kizima.awali tulikuwa gizani,tukitegemea taa la petrol,sasa naweza kusikiza redio,kuchaji simu yangu lakini hasa kuangalia runinga nakuona dunia nzima maisha yanavyotembea.Kadhalika nataraji kuwa na wageni kwa sababu nina uhakika wanakijiji kila siku watafurika hapa kutizama runinga''

Malipo yanategemea umechukua vifaa gani, mfano daraja la juu kabisa la furushi lenye taa zaidi ya 3 ,runinga na redio linalipiwa franga elfu 14 kama dolla 15 hivi kwa mwezi hadi kipindi cha miaka 3.
Katika chumba kimoja wahudumu wanaweza kufwatilia wateja wao popote walipo vijijini na kuzungumza nao mara kwa mara kujua ikiwa wanayo matatizo yanayohitaji mafundi.
Mradi huu unaendeshwa na kampuni ya Uingereza ya BBOXX kwa ushirikiano na serikali ya Rwanda.
Mwakilishi wa kampuni hiyo Bi Monica Keza ameiambia BBC kuwa ni mapinduzi makubwa katika sekta ya nishati ya umeme.

''Kuna mabadiliko makubwa kwa sasa,nishati ya umeme tunayozoea lazima utumie vifaa na mitambo kadha wa kadha ili kufanya msimiko nyumbani kwako.Nishati ya miale ya jua haihitaji mambo yote hayo.ni teknolojia ya kisasa ninayoweza kulinganisha na matumizi ya simu za nyumbani za zamani na simu za mkononi za sasa.Teknolojia yetu hii inaendeshwa toka mbali''.
Nimeambiwa kwamba mtambo wao unaweza kuhifadhi miale ya jua na hata katika kipindi cha mvua kwa siku kadhaa.
Faida za kutumia nishati ya jua:
- Nishati endelevu: Rasilmali hii haiondoshi chochote kutoka kwa mazingira, na haihitaji uchimbaji madini, au kutoboa ardhi ili kuipata - kinachohitajika ni vifaa maalum na wataalamu wa kusimika vifaa hivyo.
- Inakata hewa chafu hewani: Nishati ya jua inapunguza kwa asilimia 96 hadi 98 ya hewa chafu hewani. Nyumba moja inayotumia nishati ya jua inaweza kupunguza hewa chafu kiasi ya tani 3 hadi 4 kwa mwaka.
- Inaimarisha afya ya umma: kwa kupunguza hewa mkaa au chafu nishati ya jua inachangia kuimarisha afya ya umma na kupunguza visa vya watu kuugua matatizo ya kupumua na ya moyo.
- Itapunguza matumizi ya ardhi: Nishati hii inahitaji chini ya 20% ya ardhi inayotumika kwa vinu vya nishati nyinginezo mfano kwa kampuni za mafuta.
- Itapunguza matumizi ya maji: Tofauti na mkaa na vinu vya nyuklia, vinavyoweza kutumia hadi geleni 60 za maji kwa kila kilowati ya umeme inayozalishwa, nishati ya jua inahitaji kiasi kidogo au wakati mwingine haihitaji kabisaa maji. Hii inasaidia kupunguza matumizi ya maji hususan yaliochafuliwa kwa kemikali za viwanda.













