Mkutano wa Uhuru Kenyatta na Donald Trump White House, Marekani utaangazia nini?

Chanzo cha picha, TIZIANA FABI
Rais wa Marekani Donald Trump leo atakutana na mwenzake wa Kenya Uhuru Kenyatta katika ikulu ya White House, katika mkutano ambao unatarajiwa kuangazia zaidi masuala ya usalama na biashara.
Kenyatta anatarajiwa pia kutetea Kenya ipewe fursa zaidi ya kuuza bidhaa zake katika soko la Marekani, kando na kutafuta fedha za kufadhili miradi mikubwa ya miundo mbinu.
Marekani inatarajiwa kutumia fursa hiyo kujaribu kupunguza ushawishi wa China ambayo imekuwa ikifadhili miradi mingi ya miundo mbinu Afrika miaka ya karibuni.
Kenyatta atakuwa rais wa tatu wa nchi ya Afrika kukutana na Bw Trump kwa mazungumzo ya kina nchini Marekani baada ya kukutana na Abdel Fattah Al Sisi Septemba mwaka jana na baadaye akakutana na Muhammadu Buhari wa Nigeria.

Asubuhi, Rais Kenyatta atakutana na wakuu wa kampuni mashuhuri nchini Marekani chini ya Baraza la Kibiashara la Uelewano wa Kimataifa kabla ya kwenda Ikulu ya White House kwa mashauriano na mwenyeji wake Rais Trump.
Kiongozi huyo wa Kenya anatarajiwa kukutana na Bw Trump katika afisi yake maarufu kama Oval Office katika ikulu ya White House kwa dakika 20.
Baadaye wawili hao wanatarajiwa kufululiza hadi kwenye Chumba cha Mikutano ya Mawaziri ambapo mazungumzo yatawashirikisha wajumbe waliosafiri na Bw Kenyatta na maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani.

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya
Marekani ndiyo chanzo kikuu cha watalii wanaozuru Kenya na taifa hilo la Afrika Mashariki linatarajia kutumia fursa ya safari za moja kwa moja za ndege za Kenya Airways kati ya mataifa hayo mawili ambazo zitaanza Oktoba 28 kuimarisha idadi ya watalii wanaofika kenya.
Kibiashara, Kenya ni ya 85 kwa kuiuzia Marekani bidhaa duniani na wa jumla biashara kati ya mataifa hayo mawili huwa ya thamani ya jumla ya dola 1.5 bilioni za Marekani kwa mujibu wa Wizara ya Biashara ya Marekani.
Kenya imekuwa ikitafuta ufadhili wa ujenzi wa barabara mpya kuu ya kutoka Mombasa hadi Nairobi, mradi unaotarajiwa kugharimu takriban dola 4.5 bilioni za Marekani.
Kenya hutazamwa kama mshirika muhimu wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi Afrika Mashariki na katika Upembe wa Afrika.
Mataifa yote mawili yana majeshi Somalia yakikabiliana na wapiganaji wa al-Shabaab.

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya
Suala la kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usalama litakuwa moja ya ajenda kuu katika mkutano wa wawili hao Washington, DC.
Rais Kenyatta atakutana pia na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May jijini Nairobi Alhamisi.
Bi May atazuru Afrika Kusini na Nigeria kabla ya kufika Kenya.
Mkutano wa Rais Kenyatta na Trump una maana gani?
Waziri wa Mashauri ya nchi za Kigeni Bi Monica Juma anasema ziara ya Rais nchini Marekani ni muhimu sana katika kuboresha nyanja mbali mbali zikiwemo usalama, biashara, uwekezaji na uongozi bora.
"Ziara hii inadhihirisha umuhimu wa uhusiano kati ya Kenya na Marekani, uhusiano wa kihistoria ambao umeendelea kukua kwa mapana na marefu na kushughulikia nyanja mbali mbali ikiwemo usalama na udumishaji uongozi bora, biashara na uekezaji," alisema kwenye mahojiano na waandishi wa habari kabla ya ziara hiyo.
Kwa mujibu wake, ziara hiyo hii inatoa fursa kwa Kenya kuboresha uhusiano wake na nchi yenye uwezo mkubwa zaidi ulimwenguni kwa wakati huu.
Anasema moja ya masuala yatakayojitokeza na kupewa kipau mbele wakati wa mkutano wa kihistoria kati ya Rais Kenyatta na mwenyeji wake Rais Trump ni jinsi taifa la Kenya litakavyoweza kuongeza kiasi cha mauzo yake ya bidhaa chini ya Mkataba wa AGOA.
"Mnatambua vyema kufikia wakati huu sisi tumenufaika sana na Mkataba wa AGOA. Hata hivyo pia ni kweli kabisa kuna baadhi ya masuala katika mkataba huo tunayopaswa kulainisha zaidi. Na bila shaka kutakuwa na mazungumzo kuhusiana na suala hili," anasema.
"Tunatumaini tutaanzisha majadiliano kuhusu hali ya baada ya kumalizika kipindi cha mkataba huu wa AGOA."
Balozi wa Kenya nchini Marekani Njeru Githae anasema Kenya inatilia mkazo sana masuala ya kiuchumi kuliko diplomasia ya kisiasa.
Ana matumaini kwamba ziara hiyo itafungua ukurasa mpya wa uhsirikiano kati ya Kenya na Marekani.














