Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
John McCain: Seneta, shujaa wa vita vya Vietnam na mgombea urais aliyeshindana na Barack Obama afariki dunia akiwa na miaka 81
Seneta John McCain, shujaa wa vita vya Vietnam aliyehudumu kwa muda mrefu kama seneta nchini Marekani na aliwahi kuwania urais, amefariki dunia akiwa na miaka 81.
Bw McCain, ambaye jina lake kamili ni John Sidney McCain III, alifariki dunia Jumamosi akiwa amezungukwa na jamaa zake, kwa mujibu wa taarifa fupi iliyotolewa na afisi yake.
Alikuwa amegunduliwa kuwa na saratani hatari ya ubongo iliyokuwa inasababisha uvimbe kwenye ubongo wake 2017.
Amekuwa akipokea matibabu tangu wakati huo.
Familia yake hata hivyo ilitangaza kwamba seneta huyo ambaye aliondoka Washington Desemba na kuacha majukumu ya useneta kwenda kupokea matibabu aliamua kuacha kupokea matibabu Ijumaa.
Bintiye McCain, Meghan amesema jukumu kuu alilo nalo maishani sasa litakuwa ni "kuishi kwa mfano wake (McCain), kutimiza matarajio yake na kufikia kiwango chake cha upendo."
"Siku na miaka ijayo haitakuwa vile tena bila baba yangu - lakini zitakuwa siku njema, zilizojaa uhai na upendo, kwa sababu ya mfano mwema aliokuwa maishani mwake," ameandika kwenye Twitter.
Seneta huyo aliyehudumu bungeni kwa mihula sita aliwania urais mwaka 2008 kupitia chama cha Republican lakini akashindwa na mgombea wa chama cha Democratic, Barack Obama.
Madaktari waligundua alikuwa anaugua saratani ya ubongo walipokuwa wanamfanyia upasuaji kuondoa damu iliyokuwa imeganda kichwani juu ya jicho lake la kushoto Julai mwaka jana.
McCain alikuwa mwana na mjukuu wa maafisa wakuu katika jeshi la wanamaji nchini Marekani alikuwa rubani wa ndege za kivita wakati wa vita vya Vietnam.
Ndege yake ilitunguliwa vitani na akakaa miaka mitano kama wateka wa wakati wa vita.
Akiwa mateka, aliteswa sana jambo lililomfanya kulemaa, ulemavu ambao aliishi nao maisha yake.
McCain: Simba aliyepigana vita hadi mwisho
Na Anthony Zurcher, mwandishi wa BBC Amerika Kaskazini
John McCain alizaliwa mnamo 29 Agosti, 1936 Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikiwa vimekaribia, mwanzoni mwa 'Karne ya Marekani', wakati ambapo Marekani ilikuwa kileleni kisiasa, kijeshi na kitamaduni.
Ni kuanzia wakati huo ambapo Marekani ilianza kuwa taifa kuu duniani hasa baada ya vita hivyo.
Amefariki katika kipindi ambacho kinatazamwa kama mwanzo wa mwisho wa ubabe wa Marekani, wakati ambao taifa hili linaanza kujifikiria ndani badala ya nje, linafikiria kujenga ukuta kuwazuia wahamiaji wasiingie ndani, na kimsingi linatafakari kujikinga dhidi ya ulimwengu.
Maisha ya seneta huyo kutoka Arizona yanaakisi safari hii ya Marekani.
Aliteseka, na taifa lake liliteseka, kutokana na vita vya Vietnam.
Kama mwanasiasa wa umri mdogo, alijaribu kushawishiwa na mamlaka na pesa, na alipatikana katika sakata ya kujipatia ushawishi na umaarufu ambayo karibu ikatishe maisha yake ya kisiasa.
Mara ya kwanza alipojaribu kuwania urais mwaka 2000, alijaribu kutumia wimbi la watu kutoridhishwa na watala na watu waliodhibiti siasa kwa muda mrefu. Alijaribu kuvutia hisia za Wamarekani za kutaka uhalisia, mtu aliyeakisi matamanio yao.
Hilo lilitimia katika kuchaguliwa kwa Donald Trump mwaka 2015.
Mwaka 2008, aliteuliwa na chama cha Republican kuwania urais, lakini hakuweza kuhimili wimbi la Barack Obama, mgombea wa kwanza mwenye asili ya Afrika, pamoja na hali kwamba uchumi wa Marekani ulikuwa unaporomoka.
McCain hakufanikiwa kushinda urais alivyotamani.
Maishani mwake, alikuwa anaitetea Marekani ambayo inashiriki kikamilifu katika shughuli za dunia.
Miaka yake ya mwisho, alitofautiana vikali na Trump kuhusu mwelekeo wa chama cha Republican na maadili yaliyofaa kukumbatiwa na chama hicho.
Ni swali wazi kuhusu iwapo mtazamo kama wake una matumaini katika chama hicho.
McCain hata hivyo alilipigania lile aliloamini lilikuwa kweli na la haki. Kubaliana naye au usikubaliane naye, lakini huo ni ujumbe tosha kuwa kwenye kaburi lake.
Salamu za rambirambi zilianza kutumwa punde taarifa za kifo chake zilipotangazwa.
Donald Trump, ambaye McCain alimshutumu sana, aliandika kwenye Twitter: "Pole zangu za dhati na heshima kwa familia ya seneta John McCain. Roho zetu ziko pamoja nanyi na kwa maombi yetu pia!"
Sarah Palin, aliyekuwa mgombea mwenza wa Bw McCain mwaka 2008, alisema dunia imempoteza "Mmarekani halisi", na akapakia picha yake na mwanamume huyo ambaye alimwita rafiki yake.
Salamu za rambirambi zilitumwa pia kutoka kwa chama cha Democratic.
Barack Obama aliyemshinda kwenye uchaguzi wa urais mwaka 2008 alisema licha ya tofauti kati yake, walikuwa na mambo ya pamoja waliyoyaamini, "maadili ambayo vizazi vya Wamarekani na Wahamiaji wamekuwa wakivipigania, kuandamana kuyatetea na kujitoa kafara."
"Ni wachache sana miongoni mwetu wamejaribiwa kama alivyojaribiwa John, au wakatakiwa kuonyesha ujasiri aliouonyesha," Bw Obama amesema.
"Lakini sote tunaweza kutamania na kuonyesha ujasiri kwa kuweka maslahi ya mambo mema mbele ya maslahi yetu binafsi."
"John alipokuwa hai, alituonyesha maana ya hilo."
Makamu wa rais wa zamani na mpinzani wa McCain kisiasa ingawa alikuwa rafiki wa muda mrefu Joe Biden amesema ushawishi wa mwanasiasa huyo "kwa Marekani haujafikia kikomo".
"Maisha ya John McCain ni ithibati tosha kwamba baadhi ya kweli hudumu," amesema kupitia taarifa. "Sifa nzuri. Ujasiri. Maadili mema.
"Maisha ambayo mtu ameishi akikumbatia maadili haya, huwa yanatoa kivuli (kuwa na ushawishi) kirefu. John McCain bila shaka kivuli chake kitakuwa kirefu sana."