Hezron Mogambi: Siasa na bomoa bomoa ya majengo nchini Kenya

Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Chanzo cha picha, Peter Njoroge

Maelezo ya picha, Siasa za Ubomoaji nchini Kenya
    • Author, Hezron Mogambi
    • Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi

Siasa zinazohusiana na ubomoaji wa mijengo ambayo haijajengwa kulingana na mahitaji ya sheria zimechukua mwelekeo mpya baada ya Rais wa Kenya kusimama kidete kuhusu swala hili.

Yamkini sasa, ubomoaji utaendelea na kuingia katika maeneo mengine ya nchi kama Kajiado, Kisii na Kisimu hivi karibuni .

Ubomoaji wa majengo jijini Nairobi umetokea majuma kadhaa baada ya ubomoaji katika mtaa duni wa Kibera ambapo maelfu ya familia ziliachwa bila makao ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa barabara kupunguza msongamano katikati mwa jiji la Nairobi. Katika sehemu nyingine za jiji la Nairobi zenye mitaa duni, wakazi wameondolewa na Kampuni ya Umeme ya Kenya (KPLC) ili "kuepuka majeruhi, vifo, na madhara mengine kwa majengo yanayohusiana na reli na nyaya za umeme."

Katika taarifa aliyoitoa, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alisema kuwa alikuwa radhi kuwapoteza marafiki wake kwa ajili ya kurekebisha hali nchini Kenya na kuhakikisha kuwa anafikia malengo yake na maendeleo ya nchi.

Hatua hii ni sehemu ya kile kinachoonekana kama njia ya Rais Kenyatta kupigana dhidi ya ufisadi ambao uliokuwa umeanza kuongezeka sana na kutojali sheria.

Itakumbukwa kuwa baada ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuamua kufanya kazi pamoja, mabadiliko mengi yanaendelea kuonekana.

Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Chanzo cha picha, Peter Njoroge

Maelezo ya picha, Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Je, ni Siasa za mwaka 2022?

Hali hii imewafanya wanasiasa wengi kuingiwa na wasiwasi hasa kuhusiana na siasa za mwaka wa 2022.

Hata hivyo, Rais Kenyatta amepinga tafsili ya aina hii na kueleza kuwa yeye alikuwa na lengo la kuhakikisha kuwa ajenda zake nne kwa nchi ya Kenya ndizo mhimili wa hatua za sasa.

Pia, Rais Kenyatta aliwasuta wanasiasa ambao walitaka kuingiza siasa za mwaka wa 2022 kwenye hatua zake za kuhakikisha kuwa Kenya iko mbioni katika hatua za kimaendeleo.

Ili kufikia azma yake, Rais Kenyatta aliunda kamati kamati inayosimamia urekebishaji na ufufuaji wa jiji la Nairobi ambayo ina jukumu la kuhakikisha kuwa jiji la Nairobi linaboreshwa na kuwa jiji la kuvutia.

Kulingana na kamati hii ambayo ina maafisa wengi wakuu wa serikali, kuna majengo yapatayo zaidi ya 4,000 ambayo yatabomolewa kwa sababu za kujengwa karibu na kingo za mito na maeneo ya barabara au umma.

Ubomoaji huu unaendeshwa na mamlaka inayosimamia Mazingira Kenya (NEMA) ikishirikiana na kamati ya kitaifa kutoka sekta mbali mbali kuhusiana na shughuli hiyo, Mamlaka ya Maji, Kaunti ya Nairobi, Wizara ya mazingira na Wizara ya ujenzi.

Mamlaka ya ujenzi nchini Kenya (NCA) nayo ina ripoti ambayo inaonyesha kwamba majengo 651 yatabomolewa kote nchini Kenya siku za hivi karibuni kulingana na ripoti yao ya uchunguzi.

Uchunguzi huu uliofanywa na NCA uligundua kuwa majengo 800 kati ya majengo 5,000 hayafai kukaa watu.

Kati ya majengo 800, mengine 149 yalipatikana kuzingatia baadhi ya maelekezo na michakato ya kukubalika ingawa yakihitaji kurekebishwa kwa njia mbali mbali ili kuepuka kubomolewa.

Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Chanzo cha picha, Peter Njoroge

Maelezo ya picha, Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Ni majengo yapi yanabomolewa?

Kulingana na afisa mkuu wa NCA, Morris Aketch, majengo yanayobomolewa sasa yalikuwa yametambuliwa miaka miwili iliyopita wakati ambapo uchunguzi kuhusu mijengo hiyo ilipokamilika na kwamba swala la ufisadi katika shughuli yote nzima haliwezi kutupiliwa mbali.

"Utagundua kuwa kati ya majengo 10 ambayo yalichunguzwa jijini Nairobi, manne yalipatikana kutokuwa salama."

Majengo yanayobomolewa yalikuwa yamepewa makataa ya miezi mitatu kabla ya ubomoaji huo kuanza.

Ubomoaji huo ambao ulianzia maeneo ya Kileleshwa jijini Nairobi ambapo kituo cha mafuta ya Petroli cha Shell na mkahawa wa Java vilibolewa ikifuatiwa na jingo Southend Mall na baadaye kituo cha Ukay Centre.

Majumba mengine yanatarajiwa kubomolewa ni pamoja na na katika sehemu za Kamukunji, ambapo kuna mijengo ambayo imejengwa karibu na mto Nairobi karibu na soko kuu la Gikomba katika shughuli inayoendelea nchini Kenya.

Pia, sehemu za Lang'ata, Nairobi West, na South C ambazo zimekuwa zikikumbwa na mafuriko wakati wa mvua kubwa zitashughulikiwa hasa katika maeneo ya chemichemi na kingo za mito.

Hatua ya sasa ya ubomoaji inatokana na athari zinazotokana na mvua inaponyesha, jambo ambalo wataalam wamelimbikizia lawama kwa majengo yanayotatiza njia za maji.

Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Chanzo cha picha, Peter Njoroge

Maelezo ya picha, Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Sheria ya Bunge ya mwaka wa 2012 inafafanua "riparian reserve" kama ardhi iliyoko karibu na bahari, ziwa, mito, mabwawa na njia za maji kama inavyoelezwa na sheria ya ukadiriaji ardhi (Cap. 299) ama sheria nyingine yoyote iliyoandikwa.

Majengo mengi yanayolengwa katika ubomoaji wa sasa yalikuwa yatari yameshalengwa kupitia kwa kamati ya bunge la Kenya inayohusiana na mazingira na mali asili.

Katika ripoti yake iliyotoa mnamo Juni mwaka huu, majengo kadhaa katika jiji la Nairobi yalikuwa yameorodheshwa kuwa katika sehemu chepechepe.

Sehemu zilizoorodheshwa katika ripoti hiyo na ambazo majengo yatabomolewa ni pamoja Limuru Road, Spring Valley estate, Globe Cinema Round-About, Parklands, Fuata Nyayo estate katika mtaa wa South B, Village Market, Kitusuru, Umoja, Roysambu, South C, na Githurai.

Jijini Nairobi, majengo tisa yapo kwenye maeneo chepechepe pamoja na mtaa wa makazi duni wa Fuata Nyayo, Plot No 209/12227 kutoka barabara ya Mbagathi Way, Riverside Lane, kutoka barabara ya Riverside Drive, LR No 209/12184 , katika barabara ya Lower Kabete, LR No 209/18650 katika barabara ya Chiromo Road/Arboretum Drive, katika Riverside Drive Taj Apartment, katika Village Market katika kiwanda cha maji chafu, eneo la kuegesha magari katika majumba ya Westgate na jumba la Nakumatt Ukay.

Kuibuka kwa Siasa

Huku ubomoaji huu ukiendelea, baadhi ya wanasiasa wameanza kupinga hatua hii ya serikali. Gavana wa Kaunti ya Kiambu Ferdinard Waititu amepinga ubomoaji huo na kusema kuwa shughuli yenyewe ilikuwa inaharibu uchumi na kuharibu mali ya watu binfasi.

Badala yake, Gavana Waititu amependekeza kubadilishwa kwa nyanda za mito na sehemu mnamopitia maji nyakati za mvua.

Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Chanzo cha picha, Peter Njoroge

Maelezo ya picha, Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Mkewe Gavana Waititu, Susan Wangare, pamoja na watu wengine 14 walishikwa kuhusiana na ujenzi bila kibali katikati ya jiji la Nairobi.

Ubomoaji wa majengo ambayo yamejengwa katika maeneo chepechepe pamoja na sehemu za barabara jijini Nairobi kama njia ya kupigana dhidi ya ufisadi na hali kufanya bila hofu ya kuadhibiwa ni mpango wa Rais Uhuru Kenyatta wa kuhakikisha kuwa amefaulu zaidi katika hatamu yake ya mwisho kama Rais wa Kenya.

Pia, baadhi ya wachanganuzi na wanasiasa nchini Kenya wamekuwa wakiziona hatua za hivi karibuni za Rais Kenyatta kama mpango wa siasa za mwaka wa 2022 na atayerithi kiti chake cha Urais.

Kwa mfano, Mkurugenzi wa Mamlaka ya NEMA, Geoffrey Wahungu, amefika mahakamani kuzuia kushikwa na kushtakiwa kwake kutokana na mkasa wa Bwawa la Solai ambao uliopelekea vifo vya Wakenya 48.

Bwana Wahungu anadai kuwa anaadhibiwa kwa sababu yeye ni mmojawapo wa maafisa ambao wamekuwa katika mstari wa mbele katika ubomoaji wa majengo ambayo imejengwa katika sehemu chepechepe jijini Nairobi.

Aidha, mkurugenzi huyu anadai kuwa ameshangaa kungunduia kuwa mkurugenzi wa mashtaka nchini, Noordin Haji, anataka kumshtaki kwa madai ya makosa ya jinai kwa mamlaka ya NEMA kukosa kuzuia mauaji katika mkasa wa bwawa la Solai.

Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Chanzo cha picha, Peter Njoroge

Maelezo ya picha, Siasa za Ubomoaji nchini Kenya

Itakumbukwa kuwa baada ya mvua kubwa jijini iliyopelekea mafuriko jijini Nairobi, jumba liliporomoka katika mtaa wa Huruma na kuwaua watu 52. Mwaka mmoja kabla ya hapo, jingo linguine lilikuwa limeporomoka na kuwaua watu wawili na kuwajeruhi wengine wengi.

Katika visa hivi viwili, kilichosababisha kilisemekana kuwa ujenzi karibu na mto jambo lililonyesha kwamba sheria za ujezi hazikufuatwa.

Tatizo kubwa katika visa vingi vya majengo kuanguka ni kutokana na ukosefu wa nyumba na mahali pa kuishi kwa wakaazi wa jiji la Nairobi ambao wanaongezeka kukicha.

Siasa za kutumia mamlaka vibaya na ufisadi ndizo zimeongeza chumvi kwenye kidonda na kuharibu hali.

Prof. Hezron Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: [email protected]