Tanzania: Mwanasiasa Tundu Lissu aruhusiwa kutoka hospitalini Ubelgiji

Tundu Lissu akihutubia wanahabari 5 Januari, 2018 Nairobi

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu ameruhusiwa kutoka hospitalini alikokuwa anapokea matibabu Ulaya na sasa ataendelea kupata nafuu akiwa nyumbani.

Mbunge wa Singida Mashariki kupitia chama cha Chadema amekuwa akipokea matibabu Leuven nchini Ubelgiji tangu kuhamishwa kwake kutoka jijini Nairobi Kenya mwezi Januari.

Amekuwa akiishi hospitalini akipokea matibabu.

Taarifa ambayo inadaiwa kutoka kwake imesema: "Hello Friends of Me!!! Good afternoon to y'all. Kwa mara nyingine nawaleteeni habari njema. Leo Agosti 7 ni miezi 11 toka siku niliposhambuliwa na watu wanaojulikana sana kama 'watu wasiojulikana."

"Septemba 7 mwaka jana sikulala nyumbani kwangu. Agosti 7 ya leo, miezi 11 kamili baadae, nimeamkia nyumbani kwangu ... wote mlikuwa na hofu kubwa kama ningemaliza siku hiyo au siku chache zilizofuata, nikiwa hai. Miezi 11 kamili baadae, professor Dk Wilhelmus Jan mertsemakers daktari wangu tangu nilipokuja University Hospital Leuven, amesema sina sababu ya kitabibu ya kuendelea kukaa hospitali," gazeti la Mwananchi limenukuu taarifa hiyo.

Bw Lissu amesema ametakiwa kumuona daktari kila baada ya wiki mbili ingawa atakuwa akiangaliwa na wauguzi nyumbani kwake kila siku kwa muda usiojulikana.

Amesema kwamba bado ana chuma kikubwa kwenye paja.

"Hongereni sana kwa kazi nzuri ya kuniuguza na kuniponya na chochote mtakachokula au kunywa siku ya leo mnibakishie. Siko mbali," amesema.

Bw Lissu aliyekuwa pia rais wa Chama cha Wanasheria (TLS) alipigwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana mnamo tarehe 7 mwezi Septemba baada ya kuhudhuria vikao vya bunge Dodoma.

Alisafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu zaidi.

Maelezo ya sauti, Tundu Lissu: Kushambuliwa kwangu kulichochewa na siasa Tanzania

Alipokuwa akizungumza na wanahabari Nairobi kwa mara ya kwanza tangu kuondoka hospitalini Januari mwaka huu, Bw Lissu alisema dalili zinaonesha watu waliomshambulia kwa risasi mjini Dodoma walikuwa na uhusiano na serikali.

Mbunge huyo wa Singida Mashariki alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati akisema hali nchini Tanzania imebadilika sana.

"Tanzania imebadilika na kuwa taifa ambalo hakuna aliye salama. Mawakili wanaweza kurushiwa mabomu kwa kuwawakilisha wateja wao. Nchi ambayo afisi za mawakili zinaweza kuvamiwa, na mawakili kufungwa jela," alisema Lissu.

Maelezo ya sauti, Fatuma Karume: Tutaendelea kuikosoa serikali na kutetea haki Tanzania

Serikali imekanusha tuhuma hizo.

Makamu wa Rais wa Tanzania Bi Samia Suluhu alimtembelea hospitalini mwezi Novemba mwaka jana alipokuwa ziarani Nairobi.