Indonesia: Watu 82 wafariki katika tetemeko la ardhi kisiwa cha Lombok

Wagonjwa wakipata matibabu katika hosptali za nje
Maelezo ya picha, Wagonjwa wakipata matibabu katika hosptali za nje

Mamlaka nchini Indonesia inasema zaidi ya watu 82 wamefariki baada ya tetemeko kubwa la ardhi kukipiga kisiwa cha Lombok.

Maafisa wa idara ya kudhibiti majanga wanasema mamia ya watu wamejeruhiwa vibaya kwa tukio hilo lililotokea Jumapili.

Tetemeko hilo lenye nguvu ya 7 kwenye vipimo vya Richter limeharibu vibaya miundombinu ya umeme na barabara sambamba na nyumba.

Tetemeko hili lilisababisha watu kuchanganyikiwa
Maelezo ya picha, Tetemeko hili lilisababisha watu kuchanganyikiwa

Katika kisiwa jirani cha Bali picha za video zimeonyesha watu wakikimbia majumbani mwao huku wakipiga kelele za msaada.

Tetemeko hili limekuja wiki moja baada ya jingingine kuipiga sehemu hiyo ya Lombok, kisiwa maarufu kwa shughuli za utalii ambapo watu 16 waliuawa.

Hatari ya kuwepo kwa kwa kimbunga ilitangazwa kisiwani hapo lakini ikaondolewa saa chache baadae.

Msemaji wa idara ya kudhibiti majanga ya Indonesia amesema nyumba nyingi zimeathirika vibaya, ambapo nyingi kati ya hizo zilijengwa kwa kutumia nyenzo duni.

Waziri wa mambo ya ndani wa Singapore Kasiviswanathan Shanmugam alikua ziarani katika kisiwa hicho ambapo ametuma picha kwenye mitandao ya kijamii akionyesha namna chumba chake kilivyoathirika.

Muonekano wa tetemeko hilo katika picha za rada
Maelezo ya picha, Muonekano wa tetemeko hilo katika picha za rada

Mtu huyu ambaye hakutaja jina lake anasema alikua katika shughuli zake wakati tetemeko hilo likitokea.

''Wakati natembea nilisikia mingurumo, taratibu, taratibu, aada ikawa mikubwa na watu wakaanza kukimbia wakisema ''tetemeko'' kila mmoja wetu alichanganyikiwa na kutoka nje ya nyumba, maafisa usalama wakasema kila mtu atoke ndani.''

Daktari Ketut Sudartana, wa Hospitali ya Sanglah Mjini Bali anasema wameamua kuwatibia wagonjwa nje ili kuhakikisha usalama wao.

''Kwa wakati huu tutawatibua wagonjwa hapa nje, na kwenye sehemu ya wazi ya mazoezi. Tutaweka mahema ya dharura nje kwa msaada a BPBP ili kuwahihadhi wagonjwa wote pale, ili madaktari na manesi wetu waweze kuwahudumia vizuri zaidi.''

Maelezo ya video, Mzee aliyeishi miaka 146 afariki dunia Indonesia

Rais wa Indonesia Joko Widodo amesema serikali yake inafanya jitihada za kutosha kunusuru maisha ya majeruhi huku akituma salam za rambirambi kwa familia za wafiwa.