Wachungaji wa makanisa nchini Rwanda watakiwa kuwa na shahada

Bunge la Rwanda limeidhinisha kwa kauli moja muswada unaowataka wachungaji wa makanisa kuwa na shahada ya theolojia.
Sheria hiyo mpya inayataka pia madhehebu yote nchini humo kuweka wazi vyanzo vya fedha za matumizi yake.
Hatua dhidi ya makanisa nchini Rwanda inakuja baada ya serikali kufunga makanisa 1000 mwanzoni mwa mwaka huu, kwa kushidwa kutimiza vigezo na kanuni za ujenzi.
Mwandishi wa BBC mjini Kigali Yves Bucyana anasema kipengele cha 20 kuhusu ulazima kwa anayetaka kufundisha neneo la Mungu nchini Rwanda kuwa na shahada ya teolojia kilizua mjadala mkali.

Baadhi wanahisi serikali imeingilia sana uhuru na haki ya madhehebu kwa maoni ya kwamba uwezo wa kufundisha neno la Mungu ni wito au kipaji zaidi kutoka kwa Mungu na wala si kisomo cha darasani
''kuna watu ambao wanaitikia mwito wa Mwenyezi mungu bila ya wao kupitia shule yoyote.Kama Petro hakusoma shule yoyote.Yesu alimkuta akiwa mvuvi wa samaki.Paulo alikuwa msomi,lakini Yesu Christo hakuwahi kusoma. Je waweza kuniambia chuo ambacho Yesu alisomea?''. Alisema Mchungaji ambae hakupenda jina lake litajwe.
Lakini wengine wanahisi kwamba wanahisi kwamba ni vema wachungaji wawe na elimu ya teolojia na kwamba kuwepo kwa vyuo vikuu vinavyofundisha taaluma hiyo kunadhihirisha umuhimu wake.
Sheria hii mpya inayataka mashirika ya kiroho kubainisha vyanzo vya fedha za matumizi.
Baadhi ya fedha za matumizi ya kanisa hutokana na michango ya wakristo kila wanapohudhuria ibada, lakini fedha nyingine wanasema ni misaada kutoka wahisani.

Serikali zaidi inayataka makanisa kuweka wazi misaada ipatikanayo kwa njia ya wahisani, ikiyataka makanisa kupitisha fedha hizo kwenye akaunti iliyo wazi na kubainisha pia kwamba haina uhusiano na makundi ya kigaidi.
Kipengele hiki cha sheria kimeibua mjadala mkali baadhi ya wabunge wakitaka hata fedha za michango ya wakristo zikatwe ushuru.
"Hapa Rwanda mtu yeyote aliye na kipato cha franga elfu 30 hulipa ushuru,hawa watu wa makanisa wakipokea michango ya milioni tano au 10 hawalipi ushuru.Nahoji hawa wenye kipato kikubwa kwa nini pia wao wasilipe ushuru?, ni jambo lisiloeleweka." Alisisitiza mmoja wa wabunge.
Kuhusu makanisa sheria mpya inasema kwamba kanisa litakuwa ni nyumba kubwa yenye kufuata kanuni zote za ujenzi wa kisasa, ikiwemo vidhibiti sauti kwa ajili ya usalama wa majirani na kwamba sala zinazoendeshwa kwenye mapango,milimani au jangwani haziruhusiwi.












