Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rashid Abdalla na Lulu Hassan: Wanandoa watangazaji watakaosoma habari pamoja Kenya
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 2
Siku ya Alhamisi tarehe 12 Julai , Runinga ya Citizen nchini Kenya ilizindua orodha yake ya watangazi wa habari wa lugha za Kiswahili pamoja na Kiingereza, miongoni mwao wakiwa wanandoa maarufu Lulu Hassan na mumewe Rashid Abdalla.
Watangazaji hao wawili wamewekwa pamoja kushirikiana katika kipindi cha runinga cha kila wikendi kwa jina 'Nipashe Wikendi' kinachokwenda hewani kila Jumamosi na Jumapili kuanzia tarehe 22 mwezi Julai 2018.
Hii ni mara ya kwanza nchini Kenya kwa wanandoa kushirikiana katika matangazo ya kipindi cha habari.
Rashid Abdalla anachukua mahala pake Kanze Dena ambaye aliajiriwa na Ikulu ya rais kuwa msemaji wake mnamo mwezi Juni.
Anajiunga na wafanyikazi wengine wa runinga ya Citizen kutoka kituo cha habari cha Nation ambapo pia alikuwa mtangazaji wa habari wa NTV.
Timu mpya ya Nipashe inashirikisha mtangazaji maarufu na wa mda mrefu Swaleh Mdoe, Jamila Mohammed ambaye pia amejiunga na Citizen kutoka NTV, Mwanahamisi Hamadi, Nimrod Taabu pia kutoka NTV, Mashirima Kapombe kutoka runinga ya KTN pamoja na wanandoa hao maarufu Rashid and Lulu.
Wengi walishangazwa na tangazo la Citizen kwamba wawili hao watapeperusha habari za kila wikendi kwa pamoja.
Licha ya kwamba tangazo hilo liliwafurahisha wengi nchini Kenya ikiwemo katika mitandao ya kijamii ,maswali mengi yameulizwa kuhusu vile watakavyoweza kushirikiana.
Wengi walishindwa vile wawili hao watakavyoshirikiana kuendesha kipindi hicho iwapo wangekuwa na matatizo yao ya kinyumbani.
Lakini hayo yote yatawekwa katika kaburi la sahau wakati nyota hao watakapoendesha kipindi hicho.
Hatahivyo wengi pia walifurahishwa na tangazo hilo na wanajiandaa kuwaona wawili hao wakishirikiana katika kupeperusha habari za saa moja jioni pamoja na kushirikiana na Bi Mswafari baadaye.