Kwa nini idadi kubwa ya wanawake hujiua nchini Afghanistan

Wanawake wanaongoza kujihusisha na vitendo vya kujiua

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanawake wanaongoza kujihusisha na vitendo vya kujiua

''Sikutaka kuishi tena.Ndio sababu nilijaribu kujiua kwa sumu''.

Jamila (jina la kubuni) alijaribu kujiua baada ya kujisikia kutelekezwa na kusalitiwa na mchumba wake- aliyeamua,baada ya uchumba wao wa miaka sita,kuwa hakuwa akitaka tena kumuoa kwa kuwa ''hakuwa binti tena''.

Jamila ana miaka 18 na familia yake iliandaa sherehe ya uchumba wao akiwa na miaka 12.Alipelekwa hospitalini mjini Herat na mama yake na kutibiwa baada ya kula sumu mwezi uliopita.

Jamila ni mmoja kati ya maelfu ya wanawake wa Afghanistan wanaojaribu kujiua kila mwaka.

Wanawake wengi zaidi hujiua kuliko wanaume

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanawake wengi zaidi hujiua kuliko wanaume

Takriban raia 3,000 wa nchi hiyo hujaribu kujiua kila mwaka, hii ni kwa mujibu wa tume huru ya haki za binaadamu nchini Afghanistan.Jimbo la Herat hutokea karibu zaidi ya nusu ya matukio nchini nzima.

Kwa mujibu wa maafisa wa afya, watu 1,800 walijaribu kujiua mwaka 2017 pekee, miongoni mwao 1,400 walikuwa wanawake na 35 walijikatisha uhai.

Takwimu hizi ni karibu mara mbili zaidi ya mwaka uliopita, wakati majaribio ya kujiua 1000 yaliporekodiwa.

Duniani, kuna vifo vingi vya wanaume kutokana na kujiua kuliko vya wanawake-lakini nchini Afghanistan inakadiriwa asilimia 80 ya majaribio ya kujiua hufanywa na wanawake.

Wanawake nchini Afghanistan wanasema umasikini, kukosa haki zao na ajira ni miongoni mwa matatizo yanayowakabili

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanawake nchini Afghanistan wanasema umasikini, kukosa haki zao na ajira ni miongoni mwa matatizo yanayowakabili

Tume ya haki za binaadamu nchini humo inasema namba ya wanawake kujiua inaweza kuongezeka hata zaidi, ''kwa kuwa matukio haya hayaripotiwi kwa mamlaka kutokana na sababu mbalimbali''.

Watu wengi hufanya matukio haya kuwa siri za familia,wakiyachukulia matukio haya kuwa kinyume na uislamu.

Sababu zinazoelezwa na tume hiyo ni ''matatizo ya akili ,unyanyasaji majumbani, ndoa za kulazimishwa na mazingira mengine ya kijamii hufanya wanawake kuchukua hatua za kujiua

Maisha nchini Afghanistan ni magumu sana kwa wengi hasa wanawake.

Kwa mujibu wa Unicef, wasichana wa Afghanistan huolewa kabla ya umri wa miaka 18

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kwa mujibu wa Unicef, wasichana wa Afghanistan huolewa kabla ya umri wa miaka 18

Shirika la afya duniani linakadiria kuwa zaidi ya raia milioni moja wa Afghanistan wanasumbuliwa na mifadhaiko kutokana na waliyoyapitia kwenye miaka 40 ya mgogoro

Unyanyasaji dhidi ya wanawake umeenea.Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia idadi ya watu limesema asilimia 87 ya wanawake wameathirika na vitendo vya unyanyasaji wa kingono, kisaikolojia na asilimia 62 wamekuwa wakikabiliwa na unyanyasaji wa aina mbalimbali.

Ndoa za kushinikiza ni moja kati ya mambo yanayosababisha vitendo vya kujiua na kutoroka.

Umasikini na kukosa ajira ni changamoto zinaziripotiwa na wanawake.

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema vifo vitokanavyo na kujiua havitapungua iwapo hakutakuwa na mpango wa kupambana na vitendo hivyo.

Maafisa wa afya mjini Kabul wamesema wameweka mpango ukiwemo kuweka vituo vya kuwasaidia wale wanaopata matatizo ya kiakili na kiafya.