Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Familia ya mwanafunzi Akwilina yataka haki itendeke
Maombolezi yanaendelea nyumbani kwa mwanafunzi Akwilina Akwilini anayedaiwa kupigwa risasi na polisi na kufariki baada makabiliano kati yao na wafuasi wa Chadema siku ya Jumamosi.
Wakizungumza na BBC, ndugu wa marehemu Damian Swai, amesema wanasubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi ili waone hatua ambayo itafaa kuchukuliwa.
Damian ameendelea kusema kuwa marehemu alikuwa na ndoto za kusoma na kufaulu na kuwa na maisha yake vizuri lakini, "ndoto yake imekatishwa."
Taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo zilifikia familia kupita Chuo cha Usafirishaji cha NIT ambapo alikuwa anasoma.
Mwili wa marehemu unategemewa kusafirishwa hadi Rombo, Moshi, Mkoani Kilimanjaro kwa wazazi wake ambapo ndipo atakapozikwa.
Hata hivyo, serikali kupitia Waziri wa Elimu imesema itagharamia mazishi ya mwanafunzi huyo.
Nae dadake marehemu ameomba "haki itendeke" ili waliohusika na kifo chake wachukuliwe hatua za kisheria.
Hadi sasa polisi 6 wamekamatwa kuhusiana na kifo cha mwanafunzi huyo.
Kumekuwa na shinikizo kutoka vyama vya upinzani kama vile chama cha ACT Wazalendo, vijana na Shirika la wanafunzi nchini limemtaka waziri wa maswala ndani nchini humo Mwigulu Nchemba kuchukua jukumu la kisiasa na kujiuzulu kufuatia kisa hicho.