Teknolojia mpya inayomaliza mashimo barabarani Nairobi

Mashimo barabarani huwa ni kero kwa wenye magari na pia abiria.
Nchini Kenya, barabara nyingi mbaya jijini Nairobi zinawaletea hasara wenye magari na kuleta mahangaiko kila uchao.
Lakini teknolojia mpya ya kuziba mashimo kwa muda mfupi huenda ikaleta afueni.
Mwandishi wa BBC Ferdinand Omondi alitembelea viungani mwa jiji la Nairobi, barabara mbaya yenye mashimo ni kawaida. Alijionea madhila ambayo wanaotumia barabara zilizo katika hali mbaya hupitia, ikiwa ndiyo njia pekee wanayotumia baadhi ya watu kila siku kuenda kazini au nyumbani.
"Nikiwa ndani ya gari nahisi ni kama nimeshikwa shati na mtu ananitikisa huku na huku bila kikomo. Inahangaisha mno," alisema baadaye.

Wenye magari haswa ndio wanaoingiwa na uchungu kifedha kugharamia kuyakarabati magari yao.
Hata hawa wenye pikipiki wanaofanya biashara ya uchukuzi wa abiria, maarufu kama boda boda, kupata faida imekuwa shida.
"Ni hali mbaya," anasema Eric Miruni, mwendeshaji pikipiki.
"Ni vile tu tuna uzoefu mwingi, tunajaribu. Lakini mtu ambaye hajazoea barabara, bila shaka atamwangusha abiria.'
Lakini huenda hali ikabadilika hivi karibuni. Kwenye barabara moja kaskazini mwa jiji kuu la Nairobi, mashine ya kuziba mashimo inanguruma huku wakazi wakichungulia.
Ni mashine ambayo bado ni mpya nchini Kenya.
Inaweza kuziba shimo kwa muda wa dakika tatu tu.
Ni muda mfupi sana ukilinganisha na kutumia mafundi na watu wa mikono.
Teknolojia hii huliziba shimo kwa awamu tatu, anavyoeleza mkuu wa mradi Michael Murage.

"Kwanza kwenye hilo shimo tunatumia mtambo wa kupuliza, tunapuliza upepo kwa kasi ya hadi kilomita 100 kwa saa, hiyo inaondoa mchanga na changarawe kwenye shimo hilo na ndipo tunaingia hatua ya pili.
„Hatua ya pili pili, kuweka ile saruji maalum ya kushikanisha saruji ya kuziba shimo na ardhi, ili tukiweka saruji kamili, iweze kunata vyema.
"Hatua ya tatu sasa ni kujaza shimo na mchanganyiko wa saruji na lami.
"Tunajaza kokoto, saruji na lami. Tunatoa dhamana kwamba kazi yetu itadumu kwa zaidi ya mwaka mmoja."
Serikali ya Kaunti ya Nairobi inapania kununua mashine hizi ili kuharakisha shughuli za kuziba mashimo barabarani.


Lakini Orodi Odhiambo, mtaalamu wa kiteknolojia katika Chuo Kikuu cha Nairobi, anaonya kuwa changamoto za kushughulikia barababara bora sio za kimitambo tu.
"Mashine inaweza kuwepo, lakini vile vitu ambavyo vinahitajika kufanya kazi na mashine hiyo viwe hazipo."
"Serikali ya Nairobi lazima iweke vile vitu ambavyo vinahitajika tayari, ili wakati unahitaji hiyo mashine ifanye kazi, kutakuwa na fedha, kutakuwa na watu, kutakuwa na bidhaa, ambayo itatolewa ili iende ikatumiwe, ili ifanye kazi."
Watumizi wa barabara jijini Nairobi bila shaka watafurahia ikiwa mashimo barabarani yatapotea kwa haraka zaidi.
Lakini kibarua kikubwa kipo katika kuyashughulikia kila wakati.












