Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kampuni ya Petra Diamonds matatani kifedha
Kampuni moja ambayo ni miongoni mwa kampuni kubwa za uchimbaji madini ya almasi Afrika, Petra Diamonds, imetangaza kwamba inakumbwa na matatizo ya kifedha.
Kampuni hiyo, ambayo huendesha shughuli zake Afrika Kusini na Tanzania, imesema kwamba kuna uwezekano ikashindwa kulipa mikopo yake kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Ni pigo kubwa kwa Petra, ambao wameathiriwa na mzozo kuhusu wafanyakazi katika migodi yake Afrika Kusini na kukazwa kwa sheria za uchimbaji madini Tanzania.
Shughuli nyingi za Petra huwa Afrika Kusini ambapo wanamiliki miongoni mwa migodi mingine, mgodi maarufu wa Cullinan.
Lakini mgomo wa wachimbaji madini umeathiri sana shughuli katika migodi yake Afrika Kusini, hata ingawa mkataba wa miaka mitatu kuhusu ujira ulitiwa saini wiki iliyopita.
Mapema mwezi uliopita, maafisa wa serikali nchini Tanzania walitwaa kipande cha almasi kutoka kwenye mgodi wa Williamson, wakisema thamani yake kamili haikuwa imefichuliwa.
Serikali ya Tanzania imekuwa ikitoa madai sawa na hayo karibuni, hasa kuhusu migodi ya dhahabu nchini humo.
Wachanganuzi hawajashangazwa na tangazo la Petra kwamba huenda wakashindwa kutimiza wajibu wao katika kulipa mikopo.
Lakini hisa za kampuni hiyo katika soko la hisa la London zilishuka thamani kwa asilimia tano Jumatatu asubuhi.
Petra wameahidi kutoa maelezo zaidi kuhusu hali yao watakapotangaza matokeo ya kifedha ya kila mwaka wiki ijayo.